The House of Favourite Newspapers

Usichokijua Kuhusu Mzee wa Bwax na Uwoya

0

WEE nasema kisimu changu laini mbili kinanisevu mamaa… Wee japokuwa kidogodogo kinanisevu babaa…

Etii masela tambo hilooo…

Ahh new life tambo hiloo…

Nasema ukichukua simu ya Bwax na muziki utazimwa…

Nasema ukichukua simu ya Ajibu na muziki utazimwaa…

Usiniguse nimelewaa…

Usinishike nimelewaa…”

Hii ni sehemu ya mashairi matamu yanayopatikana kwenye Wimbo wa Kisimu Changu. Wimbo huu ndio uliomtambulisha jamaa kwenye uwanda wa muziki wa Singeli.

Mzee wa Bwax ndilo jina la kutafutia ugali. Wazazi wake walimuita Mohammed Rashid.

Mzee wa Bwax mwenyewe anapenda kujiita ‘Mtoto wa Nje ya Ndoa’. Ni mmoja wa wanamuziki wakali wa Singeli wenye madini, kwani anapopanda stejini, anaamsha mizuka ya kufa mtu ya mashabiki wake.

Ukiachilia mbali Wimbo wa Kisimu Changu, Bwax amepita vizuri kwenye ngoma kali kama

Kula na Mama, Unikome, Mshamba wa Kideo, Corona na kwa sasa anapasua anga na Sanamu la Michelini.

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limekaa kitako na Mzee wa Bwax ambaye anafunguka mambo kibwena ikiwemo ishu nzima ya penzi lake na staa wa Bongo Movies, Irene Uwoya;

IJUMAA WIKIENDA: Mipango yako kwa mwaka huu imekaaje?

MZEE WA BWAX: Kwanza naishukuru Serikali kwa kuruhusu kazi ziendelee baada ya Corona, nimepanga kuwafurahisha mashabiki wangu kwa kutoa kazi kila wiki.

IJUMAA WIKIENDA: Je, umejipangaje kuachia EP (Extended Playlist) au album?

MZEE WA BWAX: Mipango hiyo ninayo, ila ni kushauriana na uongozi wangu kwanza na nitakuwa msanii wa kwanza wa Singeli kuachia album.

IJUMAA WIKIENDA: Muziki wa Singeli umekuwa na ushindani. Je, umejipangaje na mapambano?

MZEE WA BWAX: Kwanza kwenye Singeli, mimi ni msanii ambaye sijashuka, nashukuru Mungu nina mwaka wa tatu sasa, nikitoa ngoma zinafanya poa na kukubalika kwa mashabiki wangu. Siwezi kushuka kwa sababu nipo makini. IJUMAA WIKIENDA:

Corona imekuathiri vipi kutokana na kuzuiliwa mikusanyiko?

MZEE WA BWAX: Corona imetuathiri sana, tumepoteza pesa nyingi kwa sababu nilitakiwa kusafiri nchini Kenya, Afrika Kusini na sehemu nyingi kwa ajili ya shoo, ila mambo hayakuwa sawa.

IJUMAA WIKIENDA: Ni kiasi gani cha pesa ulichopoteza?

MZEE WA BWAX: Siwezi kusema ni kiasi gani, ila mimi ninachoshukuru ni kwamba, bado tunapumua, pesa zinatafutwa tu, kikubwa uhai. Zimepotea pesa nyingi kwa sababu nyingine tumerudisha kwa wahusika kutokana na kutokufanya shoo.

IJUMAA WIKIENDA: Kuna tetesi zinasambaa kuwa unatoka kimapenzi na Irene Uwoya. Je, ni kweli?

MZEE WA BWAX: Uwoya ni mshkaji wangu sana. Ni kweli habari zangu na Uwoya zimesambaa na ninazisikia sana tu, lakini hazina ukweli wowote.

IJUMAA WIKIENDA: Umekuwa ukimposti sana kwenye ukurasa wako wa Instagram, kulikoni?

MZEE WA BWAX: Ni mshkaji, anasapoti kazi zangu na si uhusiano wa kimapenzi.

IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusiana na kolabo yako na Dulla Makabila?

MZEE WA BWAX: Sijawahi kuwaza kufanya kolabo na Dulla Makabila.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa nini unasema huwazi kufanya naye kolabo?

MZEE WA BWAX: Elewa tu kwamba sijawahi kuwaza kufanya naye kazi.

IJUMAA WIKIENDA: Unaizungumziaje menejimenti yako?

MZEE WA BWAX: Menejimenti yangu ni watu ambao wana upendo na mimi, wananipambania kuhakikisha Mzee wa Bwax sishuki, nazidi kuwa juu.

IJUMAA WIKIENDA: Ukaribu wako na Harmonize ukoje?

MZEE WA BWAX: Harmonize ni rafiki yangu tu na huwa tunashirikiana kwenye mambo mengi.

IJUMAA WIKIENDA: Je, kuna dalili ya wewe kusainiwa kwenye Lebo ya Konde Gang?

MZEE WA BWAX: Kuhusu kusainiwa Konde Gang, hakuna kitu kama hicho.

IJUMAA WIKIENDA: Ni changamoto gani unakumbana nazo katika kazi zako?

MZEE WA BWAX: Hakuna kazi isiyokuwa na vikwazo, hasa kwa upande wa wasanii, si kila mtu atakupenda, wapo watakaokuwekea chuki. Kwa upande wangu, changamoto sizichukulii kama ni sehemu ya kunifanya nisiendelee na muziki.

IJUMAA WIKIENDA: Ni mafanikio gani umeyapata kupitia muziki wako?

MZEE WA BWAX: Kwanza ninachojivunia ni kuwa na koneksheni kubwa, najulikana na watu wengi sana, kingine nina uhakika wa kula na nina gari la kutembelea. Hivyo, ninamshukuru Mungu.

IJUMAA WIKIENDA: Je, unatumia gari la aina gani na limekugharimu kiasi gani?

MZEE WA BWAX: Siwezi kutaja, hiyo ni siri yangu.

IJUMAA WIKIENDA: Mbali na muziki, ni kitu gani kingine kinachokuingizia pesa?

MZEE WA BWAX: Nina biashara zangu ndogondogo ambazo nimewekeza kiaina, zinanisaidia sana.

MAKALA: KHADIJA BAKARI, BONGO

Leave A Reply