The House of Favourite Newspapers

Usidharau Mitihani Midogo, Inakujenga

0

Ni dhahiri kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka jana ni janga kwa elimu ya Tanzania lakini hata kwa wanafunzi ambao mwisho wa siku ni watumishi ambao wataenda kwenye jamii na kuwalisha wananchi kilekile walichokipata kipindi wanasoma. Binafsi naamini moja ya kitu kilichosababisha wanafunzi wengi kufeli ni kitendo cha kudharau mitihani midogo na akili yao kuielekeza zaidi katika mitihani ya mwisho.

Ni lazima ufahamu kuwa kila kitu ili kifanikiwe ni lazima kianze na kidogo, ndiyo maana kuna msemo unaosema; “Hata mbuyu ulianza kama mchicha.” Nakubaliana na msemo huo, ili mmea ukue ni lazima mbegu ipandwe sehemu sahihi, ipate maji, hewa, mbolea na chakula ili iweze kustahimili.

Mwanafunzi unapokuwa shuleni ni kama mmea unaotakiwa kukua. Ili uweze kuwa mwanahabari, mwanasayansi, rubani, injinia na mjasiriamali hauwezi kufikia hatua hiyo bila kujipanga. Ni lazima ushiriki katika mitihani midogo ambayo itakujenga katika masomo yako.

Kamwe usidiriki kuidharau mitihani hiyo ambayo baadhi ya shule uifanya mara kwa mara ili kupima uwezo wa mwanafunzi,  usiridhike kuwa mitihani inayokupasa ni ile ya mwisho kwa maana ya kumaliza darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita, au mtihani wa mwisho wa chuo, ukifanya hivyo ni kosa sana. Unapaswa kujiandaa mapema kwa changamoto za mitihani hiyo midogo ambayo ndiyo itakujenga katika mtihani wa mwisho na hatimaye uweze kufanya vizuri.

Unaposhiriki kikamilifu katika kufanya mitihani hiyo midogo itazidi kukujenga na somo au mada husika itakuwa imekuingia vizuri akilini mwako na kutulia katika sehemu ya ubongo inayohusika kutunza kumbukumbu ili muda wa kukitumia kile ulichotunza ukifika basi unakumbuka tu na kuweka jibu lako lililo sahihi.

Usijidanganye kama unaweza kufikia malengo yako kimasomo, maisha na hata kutimiza ndoto zako kwa kudharau au kutojishughulisha na vitu vidogo, siku zote vidogo hivyo ndivyo vinavyozalisha vikubwa na hii ndiyo falsafa ya  maendeleo ulimwenguni, hata ukibahatika kukutana au kukaa na wasomi wakubwa ambao wewe unapenda kuwa kama wao watakwambia kuwa kujifunza kitu hakuhitaji dharau, unaweza kupata kitu kikubwa katika kitu kidogo, unaweza kufaulu mtihani mkubwa kwa kufanya mazoezi ya mitihani midogo.

Leave A Reply