Usilie eti umri unakwenda huolewi

NI Jumanne tena, mikikimikiki ya siasa ndiyo habari ya nchi kwa sasa. Pole nyingi kwa familia ya Christopher Mtikila kwa kuondokewa na mwanasiasa huyo maarufu nchini.

Mada yangu ya leo ni; usilie eti umri unakwenda huolewi’. Kilio cha kutoolewa ni kikubwa kwa wasichana (wanawake) kuliko cha kuoa kwa wavulana (wanaume).

Sikumbuki kama nimewahi kukutana na mwanaume akadai anateswa na kutooa. Kama yupo maana yake anateswa kwa sababu haoni mwanamke wa kumuoa. Lakini nimewahi kukutana na wanawake kibao wanaoteswa na kutoolewa, tena wengi wakisema umri unakwenda wanahofia kuzeeka bila ndoa.

“Kaka yaani mimi nakwambia hakuna jambo linaloniumiza kama kutoolewa. Sasa hivi nina miaka 28, lakini wachumba hakuna. Uzee ndiyo huo unaingia. Hili jambo linaniuma sana,” mdada aitwaye Rehema aliwahi kuniambia kwenye chumba cha habari cha magazeti ya Global.

Mwingine yeye alisema wazi: “Mimi najua siolewi tena maana umri umeshakimbia sana (miaka 32), lakini watoto wangu wawili wananitosha kabisa. Bahati nzuri mmoja wa kiume. Kwa hiyo yeye namwona kama ndiyo mume wangu.”

VILIO HUZAA WATOTO HAWA

Matokeo ya vilio hivi kwa ninavyojua mimi ni msichana kujikuta anaamua kuzaa ili apate mtoto hata kama hajaolewa.

Wasichana wengi wanaamini kwamba, kuendelea kusubiri mwanaume wa kumuoa huku umri unakwenda, wanaweza kulala kapa, waume wasipatikane na watoto pia.

Nawaona warembo wengi mjini (ma-miss na wasanii wa filamu) wameamua kuzaa angalau ‘katoto kamoja’ tu ili kujihakikishia umama wake.

Kuna msanii mmoja wa filamu aliwahi kuniambia: “Mimi kwa kumzaa mtoto wangu huyu sina shida. Niolewe, nisiolewe kwangu sawa tu.”

KWAKO WEWE SASA

Sasa kama wewe ni msichana, umri unaona unakwenda. Umeshapiga 27, hakuna cha mchumba wala mwanaume aliyewahi kukutania kuhusu uchumba, usilie.

Kila binadamu amepangiwa maisha yake na Mungu. Tabia ya kulia eti kisa hujaolewa, wengi wamelizwa zaidi baada ya kuolewa.

Unaweza kusema ‘mimi kwa nini siolewi…mimi kwa nini siolewi’ matokeo yake akijitokeza mwanaume akatangaza nia, unajiingiza mzimamzima bila kumchunguza na mwishowe ni kujikuta umetumbukia kwenye ndoa yenye maisha ya majuto tangu harusi hadi uzeeni.

KWA NINI UJUTIE?

Sijajua ni kwa nini baadhi ya watu wanalilia kuolewa! Ninavyojua mimi kuolewa ni agizo la Mungu. Sasa yeye ndiye mwenye maamuzi ya kukupa nani akuoe. Wakati mwingine anapokunyima mume, ameshakuangalia mateso utakayoyapata ndani ya ndoa. Hivyo mshukuru Mungu pia.

JICHUNGUZE MWENYEWE PIA

Lakini katika yote, pia kuna kitu cha kujichunguza wewe mwenyewe unayelialia kutoolewa. Je, tabia yako ni njema? Unafaa kuwa mke mwema? Maana unaweza kuwa unalia kumbe wanaume wanakukwepa kutokana na sifa yako!

Ni kweli wapo wanaume siku hizi hawamchunguzi mwanamke kabla ya kuoa, lakini ndani ya uhusiano wenu wa siku hizi wa u-girlfriend na u-boyfriend, mwanaume anaweza kukusoma kwamba akikuoa imekula kwake. Matokeo yake siku zinapita jamaa hagusii ndoa.

Ukigusia wewe anakushangaa maana uhalisia, mwanaume ndiye anayetafuta wa kumuoa na si mwanamke kutafuta wa kumuoa.

Kwenye hili eneo la kujichunguza ndiyo msingi wa maana na kama utalijua vizuri hutahangaika kwani utakuwa unajua kwa nini huolewi! Tabia kama ni nzuri usilie, Mungu amekunusuru.


Loading...

Toa comment