The House of Favourite Newspapers

USIOMBE Yakukute! Mama na Mwanaye Wakiona Chamoto – Video

 

DAR ES SALAAM: Mkazi wa Bunju B Kwa Baharia jijini Dar, Barbara Agustino na mama yake mzazi, Jumatatu iliyopita walikiona cha moto kufuatia wananchi wa eneo hilo kutaka kuwapiga baada ya kumtuhumu Barbara kumfanyia ukatili msichana wake wa kazi ‘house girl’ aliyefahamika kwa jina la Olivia Mwekonde ‘18’ jambo lililowakera wakazi hao.

 

Imedaiwa na chanzo chetu kuwa bosi huyo mwanamke amekuwa akimshushia kipigo mdada huyo wa kazi mara kwa mara na kabla ya Jumapili iliyopita alimpa kipigo kilichosababisha binti huyo apoteze fahamu na kuzinduliwa na majirani baada ya kupelekwa chooni ambako alimwagiwa maji na kupewa huduma ya kwanza.

 

Haikuishia hapo, Jumapili bosi huyo amedaiwa kumshushia tena kipigo kikali binti huyo ambapo majirani waliompa huduma ya kwanza na kumzidua pamoja na wananchi wengine walikusanyika na kutaka kumpa kichapo bosi huyo na mama yake aliyefika kumtetea.

Hata hivyo wakaamua kwenda kumpa taarifa mjumbe wa nyumba 10 wa shina namba 19 Tawi la Kizita Kwa Baharia, Kenneth Mushi ambaye ni ‘mjeda’ mstaafu wa JWTZ.

 

Baada ya wananchi hao kumfikishia mjumbe malalamiko hayo mjumbe huyo haraka alikwenda kumuokoa binti huyo na kumuamrisha bosi na mfanyakazi wake huyo waongozane mpaka Kituo cha Polisi Mabwepande.

Mara tu baada ya mjumbe kuwafikisha kituoni hapo na kuchukuliwa maelezo, jalada la kujeruhi mwili lilifunguliwa na kupewa kumbukumbu namba MBP/RB/905/2018.

Hata hivyo, kuna madai kwamba kesi hiyo imemalizwa na bosi huyo kimtindo kituoni hapo.

 

Baada ya kesi hiyo kumalizwa kimtindo na polisi shauri hilo ilirudi mtaani baada wa wapambe kumvujishia umbeya Mjumbe Mushi kuwa bosi huyo alimnanga kuwa njaa ndiyo inayomsumbua na ndio iliyomfanya amfikishe polisi lakini tayari ameshaifuta kesi hiyo na hakuna wa kumfanya lolote kwa kuwa mumewe ana pesa nyingi na ni mfanyabiashara mkubwa mwenye duka la vifaa vya ujenzi mtaani hapo.

Wapambe hao walizidi kumjaza ‘upepo’ mjumbe kuwa, sambamba na hayo bosi amesema hakuna wa kumtisha kwa kuwa baba yake ni Afisa wa Usalama wa Taifa.

Mjumbe Mushi baada ya kupenyezewa laivu ubuyu huo alimpigia simu mume wa Barbara na kumueleza jinsi mkewe alivyomdhalilisha kwa kusema ana njaa na mambo mengine aliyoambiwa na wananchi wa eneo lake.

 

Habari zinasemna mume huyo alipoambiwa maneno hayo alipigwa na butwaa, hivyo alimpigia simu mkewe Barbara na kumwambia kwa nini ametoa majigambo hayo ya kumdhalilisha mjumbe lakini alikanusha kutoa tambo hizo.

Inaelezwa kuwa Barbara aliamua kumfuata mjumbe ili akamuambie nani aliyempelekea maneno hayo aliyodai ya uongo.

 

Baada ya kufika kwa mjumbe alikutana na mjumbe akiwa na wananchi pamoja na msichana wake wa kazi ambaye alikuwa akimuomba mjumbe amsaidie ili apate nauli ya kurudia kwao Kijiji cha Chagongwe, Wilayani Gairo, Mkoa wa Morogoro.

Barbara kusikia hivyo, alisababisha malumbano makali kati yake na wananchi waliokuwa wakimtuhumu kuwa ana roho mbaya na anaweza hata kuua.

 

Malumbano yalizidi kuwa makali na kusababisha kundi la watu liongezeke na kuanza kumzomea yeye na mama yake aliyekwenda naye kwa mjumbe huyo, na nusura wale kichapo kutoka kwa watu.

Baada ya hali kutulia Barbara aliulizwa na Amani juu ya mzozo huo akakiri kwamba kulikuwa na hali ya kutoelewana na mfanyakazi wake huyo lakini walishayamaliza polisi.

“Ni kweli hilo la kutofautiana na kumpiga huyu mfanyakazi wangu silikatai lakini hayo tulishayamaliza polisi,” alisema.

 

Naye mfanyakazi huyo akizungumzia chanzo cha kupigwa na bosi wake huyo alisema ni baada ya kuzianua nguo na kusahau kuzikunja. Mjumbe Mushi akizungumza na Amani alisema amechoshwa na kesi za Barbara za kumfanyia ukatili mfanyakazi wake na kusema anatarajia kufanya mazungumzo na mwenye nyumba wake ili amuhamishe asije akamletea kesi ya mauaji mtaani kwake.

Stori: Richard Bukos, Amani

SHUHUDIA VIDEO YA TUKIO HILO

Comments are closed.