The House of Favourite Newspapers

Uso kwa uso na mtoa roho!-3

0

ILIPOISHIA:

“Sasa pale si walikuwa wawili? Huyo mwingine ni nani?”

“Si yule mwalimu wenu, Mwashambwa?”

“Mwalimu wetu Mwashambwa anayetufundisha hesabu naye ni mchawi?” niliuliza kwa mshangao mkubwa huku mdomo nikiwa nimeuacha wazi.

SASA ENDELEA…

“Ndiyo, hata ule mguu wake anaochechemea nasikia alikutana na kombora la kichawi ndiyo likampa ulemavu wa kudumu, siyo mtu mzuri kabisa, we turudi nyumbani utasikia chochote kuhusu watu hao wawili,” baba alisema kwa kujiamini, ukimya mrefu ukatanda kati yetu, hakuna aliyezungumza chochote.

Niliendelea kutembea huku nikiwa na furushi langu la dawa kichwani pamoja na panga, baba yeye alikuwa ametangulia mbele, naye akiwa amebeba dawa na jembe tulilokuwa tunalitumia kuchimbia dawa.

Ili kufika nyumbani kwetu, ilikuwa ni lazima upite nyumba kadhaa za nyasi na nyingine za bati zilizokuwa pembezoni mwa kijiji ndiyo uelekee nyumbani. Miongoni mwa nyumba hizo, ilikuwepo pia na nyumba ya mzee Mwankuga ambaye muda mfupi uliopita baba alikuwa akinisimulia mambo yake kwamba ni mchawi.

Tulipokaribia nyumbani kwa mzee huyo, baba alinionesha ishara kwamba nisimame, nikafanya hivyo, tukawa tunasikia sauti za watu wengi wakilia kutoka nyumbani kwa mzee huyo, baba akanionesha ishara kama anayesema ‘unaona?’ nikashika mdomo kwa mshangao. Sikutaka kuamini kwamba kweli mzee Mwankuga alikuwa amefariki dunia.

Baada ya kusimama pale njiani kwa dakika kadhaa, baadaye tuliendelea na safari lakini bado mawazo mengi yalikuwa yakiendelea kukisumbua kichwa changu. Kwanza ilikuwa ni kile kilichotokea kuanzia kule porini na yale niliyokuwa nayashuhudia muda huo. Sikutaka kuamini kwamba mwalimu wetu, Mwashambwa alikuwa mchawi.

Kutokana na uwezo wangu mkubwa darasani, hasa katika somo alilokuwa anatufundisha la hesabu, nilikuwa kipenzi kikubwa cha mwalimu huyo. Mara kwa mara alikuwa akiniita ofisini kwake na kama kuna kazi alikuwa anataka kusaidiwa, alikuwa ananitumia mimi. Taarifa kwamba alikuwa mchawi, zilinishangaza mno.

Tulifika nyumbani na kutua mizigo yetu, mimi bado moyo wangu ukawa hautaki kuamini kama kweli Mwankuga amekufa. Nilichokifanya, ilikuwa ni kuondoka nyumbani kimyakimya kwa lengo la kwenda tena kwa mzee Mwankuga kuhakikisha. Japokuwa tulikuwa tukikatazwa kabisa kwenda kwa mzee huyo, siku hiyo niliamua kuvunja masharti ya baba.

Nikatembea harakaharaka na hatimaye nikatokezea nyumbani kwa mzee huyo ambapo nilikutana na umati mkubwa wa watu wenye nyuso za huzuni, wakiwa wamekaa nje ya nyumba hiyo kama ilivyo kawaida ya mila za Kitanzania kunapotokea msiba.

Kitendo cha mimi kuonekana tu eneo hilo, nilishangaa watu wakiacha kila walichokuwa wanakifanya na kunikodolea macho. Hata wale waliokuwa wanalia, wote walinyamaza, wakawa wananitazama. Sikuelewa kwa sababu gani hali hiyo imetokea, hofu kubwa ikatanda ndani ya moyo wangu.

Kwa mbali nikaanza kusikia minong’ono huku watu wakiendelea kunitazama. Mzee mmoja ambaye naye siku za nyuma nimewahi kusikia kwamba ana tabia ya kuwaibia watu fedha kwa uchawi wa ‘chuma ulete’, alisimama na kuongea kwa jazba.

“Baba yako alichokifanya ameona hakitoshi ameamua kukutuma na wewe uje kuendeleza uchawi wenu hapa. Mwaka huu mtaisoma namba, kamwambie anajikaanga kwa mafuta yake mwenyewe, mwisho wake umekaribia,” alisema mzee huyo na kusababisha watu karibu wote pale msibani wamuunge mkono, zogo kubwa likatokea huku wengine wakiinuka na kutaka kuja kunishushia kipigo.

Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini watu walikuwa wakinitazama kwa macho ya chinichini nilipofika msibani hapo. Kumbe walikuwa wanahisi baba amenituma mwenda kufanya uchawi! Maskini, nilibaki natetemeka kwa hofu kubwa kwa sababu sikuwa najua chochote kuhusu uchawi wala kuroga.

Ili kuokoa maisha yangu, ilibidi nitimue mbio, wakaendelea kunisindikiza kwa maneno makali wakimtuhumu baba na sisi familia nzima kwamba tunahusika na mambo ya kishirikina.

Je, kilifuatia nini? Usikose kufuatilia katika Gazeti la Risasi Jumatano wiki ijayo.

Leave A Reply