The House of Favourite Newspapers

Uso kwa uso na mtoa roho!-9

1

ILIPOISHIA:

Huku nikitetemeka, nilisogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amelala, akiendelea kukoroma kwa nguvu, mimi nikamshika miguuni na baba akamshika kichwani, tukaanza kumkokota kumtoa nje ya eneo letu, tukaenda kumbwaga pembeni kabisa kwenye vichaka kisha tukarudi ndani. Ile tunaingia ndani tu, tukasikia mlango ukigongwa kwa nguvu.

SASA ENDELEA…

 

Nani!”

“Fungua!”

“Sifungui mpaka mjitambulishe na mueleze shida yenu.”

“Ni mimi mzee Sifuni, mwenyekiti wa kijiji.”

“Unaonekana hauko peke yako!”

“Ndiyo, nimeongozana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji, fungua tafadhali,” baada ya mwenyekiti huyo kusema hivyo, baba alinioneshea ishara kwa mkono kwamba niende ndani kwa sababu alishahisi wale watu wamekuja kwa shari. Nikatii nilichoambiwa na kwenda chumbani lakini bado nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona kinachoendelea.

Baba alipofungua tu mlango, nilisikia wakimuamrisha jambo:

“Upo chini ya ulinzi.”

“Kwa kosa gani?”

“Kwa kumshambulia mganga wa kienyeji aliyekuwa anatimiza majukumu yake hapa kijijini kwetu.”

“Hivi nyie mna wazimu nini? Mbona mnanifuatafuata sana? Sasa anayejiona mbabe aniguse,” nilimsikia baba akifoka kwa jazba. Yule mwenyekiti akawa anaawamrisha mgambo wamkamate baba, lakini kila mmoja akawa anamtupia mpira mwenzake kwa hofu.

Nadhani lile tukio la ‘kumzimisha’ mganga ambaye kila mmoja alikuwa akimuona kama ni kiboko, liliwajaza hofu kubwa ndani ya mioyo yao. Baadaye niliwasikia wakiondoka huku wakitoa maneno ya kumtisha baba kwamba eti siku zake zinahesabika, wakaelekea ule upande tulikomtupia yule mganga ambaye bado alikuwa akiendelea kukoroma kama anayetaka kukata roho.

Wakamchukua na kuondoka naye ambapo taarifa tulizozipata kesho yake ni kwamba alisafirishwa usiku huohuo kuelekea nyumbani kwao, Malawi akiwa na hali mbaya sana. Siku zilizidi kusonga mbele, uhasama kati ya familia yetu na wanakijiji wengine ukazidi kushamiri pale kijijini, kila mtu akawa anatuchukia na kutusema vibaya.

Wiki kadhaa baadaye, siku hiyo nikiwa narejea kutoka shuleni, nilipata taarifa kwamba yule mganga kutoka Malawi amerejea tena na safari hii, amekuja na jeshi la waganga wengine kadhaa kwa lengo la kuja kumkomesha baba kwa alichomfanyia.

Taarifa hizo zilinishtua sana, ikabidi nimfikishie baba haraka lakini tofauti na nilivyotegemea, alizipokea kwa dharau na kuendelea kusisitiza kwamba yeye siyo mchawi bali mganga na yeyote atakayethubutu kumuingilia kwenye mambo yake, atamshikisha adabu.

Niliishiwa maneno, ikabidi nikae kimya kusubiri kuona mwisho wa hayo yote utakuwa nini. Taarifa za ujio wa waganga hao kutoka Malawi zilizidi kusambaa kwa kasi ya kimbunga, wanakijiji wengi wakawa wanaonesha kufurahia ujio wao.

Hatimaye siku moja usiku, tukiwa tumemaliza kupata chakula, kundi la wanakijiji wengi liliwasili pale nyumbani kwetu, wakiongozwa na wale waganga ambao jumla yao walikuwa watano.

Wakaizunguka nyumba yetu huku watu wakipiga kelele kwa nguvu wakitaka eti baba akomeshwe. Siyo kwamba namtetea baba yangu lakini binafsi, mpaka muda huo nilikuwa sielewi kwa sababu gani watu wanamchukia kiasi hicho wakati hakuwa mchawi kama mwenyewe alivyokuwa anasema bali mganga.

Vifo vya wanakijiji wawili, Mwankuga na Mwashambwa havikuwa vigezo vya kumuita baba mchawi kwa sababu wao ndiyo walioanza kumchokoza na mimi nilikuwepo siku hiyo. Nikawa nahisi kwamba huenda ni chuki za watu ndizo zilizosababisha yote hayo.

Anyolewe! Anyolewe!” ule umati uliokuwa nje ya nyumba yetu ulikuwa ukipiga kelele kushinikiza eti baba anyolewe uchawi. Baba akatutaka wote tutulie ndani na asiwepo wa kutoka nje hata mmoja, akaingia kwenye chumba chake cha uganga na muda mfupi baadaye, alitoka mpaka nje kulikokuwa na wale watu.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano ijayo kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

1 Comment
  1. Ahady kidehele says

    Fupi sanaaaaq

Leave A Reply