The House of Favourite Newspapers

Uso kwa uso na mtoa roho!

0

Jina langu naitwa Togolai Mahimba ni mtoto wa mwisho kati ya watoto saba wa baba yetu, Sinai Mahimba ambaye kwa sasa ni marehemu. Baba yetu alifariki miaka mitatu iliyopita baada ya kuugua ghafla.

Kifo chake kilitawaliwa na utata mkubwa na hata siku ya mazishi yake, kulitokea mambo mengi ya ajabu ambayo mpaka leo siwezi kuyaeleza. Ninayo mambo mengi ambayo ningependa kukusimulia ndugu msomaji lakini kwa kuanzia, naomba nikueleze mambo machache yaliyotokea kabla ya kifo cha baba yetu ambaye mimi ndiyo nilikuwa mtoto anayenipenda zaidi.

Kabla hajafikwa na mauti, baba yetu alikuwa mtu maarufu sana kijijini kwetu, Makongorosi, Chunya mkoani Mbeya tulikokuwa tukiishi. Kilichofanya awe maarufu kiasi hicho ni kazi yake ya uganga aliyokuwa anaifanya ambapo mbali na mambo mengine, alikuwa akiwafanyia matambiko wachimbaji wengi wa dhahabu ili wakiingia mgodini, wapate dhahabu kwa urahisi sambamba na wafanyabiashara wengine.

Umaarufu wa baba ulisababisha hata sisi watoto wake tuwe maarufu sana, hasa mimi ambaye muda mwingi nilikuwa nikiongozana naye kila alikokuwa anakwenda, kuanzia kwenye matambiko maporini, kwenye mazindiko migodini, kuchimba dawa msituni mpaka kilingeni kwake alikokuwa akifanyia shughuli zake za uganga.

Wengi walikuwa wakifupisha jina langu kwa kuniita Togo na hilo ndiyo lililokuwa maarufu kuliko hata jina langu halisi. Nakumbuka maisha yangu ya utotoni yalikuwa ya raha sana kutokana na jinsi baba alivyokuwa akinipenda. Hata ndugu zangu wengine tuliozaliwa pamoja, walikuwa wakinionea gere kwa jinsi nilivyokuwa nikipendwa.

Maisha yaliendelea vizuri, nikawa naendelea kukua huku pia nikijifunza mambo mengi aliyokuwa akiyafanya baba katika kazi zake. Mambo yalianza kubadilika siku moja tukiwa msituni na baba kutafuta dawa.

Baba akiwa ameinama akichimba mizizi ya mti wa mtangetange ambao ulikuwa ukitumika kwa kutibu magonjwa mengi, hata yale yaliyoshindikana hospitalini, ghafla alivamiwa na kundi la popo waliokuwa wanapiga kelele kwa nguvu. Baba akawa anahangaika kujaribu kuwazuia popo hao ambao waliendelea kumzonga hasa sehemu za kichwani.

Akiwa anaendelea kupambana nao, nilimshuhudia akifanya tukio ambalo sikuwahi kumuona baba akilifanya hata mara moja. Kwa kasi ya kimbunga, aliyeyuka na kupotea eneo hilo, nikabaki nimepigwa na butwaa, nikiwa siamini.

Ghafla wale popo baada ya kuona baba amepotea kimiujiza, walitawanyika na kupotea eneo hilo huku wakiendelewa kupiga kelele kwa nguvu. Nikawa nageuka huku na kule kumtazama baba bila mafanikio, hofu kubwa ikatanda kwenye moyo wangu.

“Unashangaa nini Togolai,” sauti ya baba ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, nikashtuka kwa nguvu. Cha ajabu, baba alikuwa amesimama palepale alipokuwepo, akiendelea na kazi yake ya kuchimba mizizi ya mtangetange kama hakuna kilichotokea.

“Baba mbona sielewi?”
“Huelewi nini tena?”
“Popo.”
“Popo? Wamefanya nini?”
“Hawajakuumiza?”

“Mbona sikuelewi Togo?” alisema baba huku akiacha kazi aliyokuwa anaifanya na kunisogelea. Sikutaka kuamini kama kweli baba alikuwa haelewi nilichokuwa nakizungumza, akanisogelea na kunishika begani.
“Uko sawa?”

“Ndi..yo baba, niko sawa,” nilibabaika kidogo, nikamuona baba akigeuka huku na kule kama anayeangalia kitu fulani. Na mimi nikawa nageuka kufuata usawa wa macho yake, ghafla macho yetu yakaganda eneo moja, nilipigwa na butwaa kubwa kwa nilichokuwa nakiona, nikajikuta nikianza kutetemeka.

Wanaume wawili waliokuwa uchi wa mnyama, walikuwa wakining’inia kwenye tawi la mti mkubwa uliokuwa mita chache kutoka pale tulipokuwa, wote wakitukodolea macho yao mekundu.

“Unawaona wale washenzi?” baba alisema huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya wasiwasi. Nikatingisha kichwa kama ishara ya kumjibu ‘ndiyo nawaona’.
“Wale ni wachawi wanaosumbua watu kijijini kwetu, naona wametangaza vita na mimi, hawanijui hawa,” alisema baba.
Je, kiliendelea nini? Usikose Jumatano ijayo hapahapa.

Leave A Reply