The House of Favourite Newspapers

ALIYEJIFUNGUA NA KUAMBIWA MTOTO KAFA, UTATA WA MAITI WAIBUKA!

0
Anita Shayo

Mwanamke mmoja, Anita Shayo, mkazi wa Tabata aliyejifungua hivi karibuni kwenye Hospitali ya Amana jijini hapa, kisha mtoto wake ambaye alikuwa hajatimiza siku za kuzaliwa (njiti) kudaiwa kufariki dunia amezua utata baada ya kuikataa maiti na kuomba apewe mwanaye la sivyo ataendelea kukaa wodini.

 

Tukio hilo limetokea hivi karibuni baada ya Anita, kujifungua mwanaye huyo akiwa na miezi saba mwenye uzito wa kilogramu moja, kisha kuambiwa mtoto huyo anatakiwa akahifadhiwe kwenye chumba maalum, katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili.

 

Akisimulia mkasa huo kwa masikitiko, Anita alikuwa na haya ya kusema:

“Nilifika Hospitali ya Amana nikiwa na uchungu wa kujifungua na kweli nilijifungua mtoto ambaye ni njiti, akiwa na miezi saba tu na uzito wa kilo moja, lakini nilikuwa na furaha ya kujifungua.”

 

AONESHWA MTOTO

“Baada ya kujifungua nilioneshwa na manesi mtoto wa kike na wakaniambia anatakiwa apelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhifadhiwa kwenye chumba maalum kutokana na kutokamilika siku zake ikiwa ni pamoja na uangalizi zaidi,” alisema Anita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni.

 

KONDO LASHINDWA KUTOKA

Mwanamke huyo alizidi kueleza kuwa, baada ya kujifungua ule mfuko wa nyumba ya uzazi (kondo), ulishindwa kutoka hivyo alihitajika kufanyiwa upasuaji maalum, jambo ambalo alikubaliana nalo.

 

AHAKIKISHIWA USALAMA WA MWANAYE

“Nilimuuliza daktari kuhusu mtoto wangu, akanijibu kuwa yu salama kabisa nisiwe na wasiwasi hata kidogo, nikawa na amani kabisa moyoni mwangu,” aliongeza Anita.

 

AOMBA MUMEWE AKAMUONE MTOTO

“Kutokana na kuwa katika hali ya ugonjwa nilishindwa kuwa karibu na mwanangu, niliomba japo mume wangu aruhusiwe kwenda Muhimbili ili akamuone mtoto kabla ya taratibu nyingine kuendelea, lakini katika hali ya kushangaza daktari alimkatalia mume wangu kumuona kwa maelezo kuwa nitaenda mimi kumuona nikishapona,” alisema Anita kwa uchungu.

 

UTATA WAANZA

“Nilipopata nafuu na kuona naweza kutembea vizuri, niliomba tena nipelekwe kwa mwanangu, ambapo waliniambia niongozane na nesi hadi Muhimbili nikiwa na kadi, lakini tulirudishwa kwa sababu sikuwa na namba ya mtoto ambayo hufanana na aliyowekewa mtoto, hivyo sikupewa wala kumuona mwanangu na nikarudi tena Amana.

 

“Nilirudi nikiwa na hasira za kuchoka na kusumbuliwa, siku iliyofuata nilienda na nesi mwingine ambaye aliulizwa maswali kadhaa pale mapokezi na kushindwa kuyajibu kwa ufasaha, ikabainika kuwa Amana walikosea utaratibu mzima hivyo taarifa zangu zilijazwa upya na nikaruhusiwa kwenda kwenye wodi ya watoto kumchukua mwanangu, lakini hatukumuona licha ya kutafuta kwa muda mrefu,” alidai Anita.

 

Akaongeza: “Tulipomkosa tulirudi Amana, lakini nilikua na uchungu kupindukia na kujiuliza inawezekana vipi mwanangu apotee katika mazingira kama haya? Nilijiambia hapana ni lazima nipambane kuhakikisha najua mbivu na mbichi kuhusu mtoto wangu.”

 

TAARIFA ZA KUFARIKI KWA MWANAYE

“Katika hali ya kushangaza, zikiwa zimepita takriban siku 12 ndipo nilipopewa taarifa kuwa mwanangu alifariki siku hiyohiyo niliyojifungua, sasa maswali yakawa ni mengi kwa wakati mmoja, kama alifariki siku nimejifungua, walishindwa nini kunieleza siku hiyo?

 

“Kwa nini walikuwa wananisumbua kwenda Muhimbili mara kwa mara? Kwa kweli niligoma kuondoka hospitalini hadi nipewe maelezo ya kutosha, ambapo mganga mkuu wa hospitali na yule wa wilaya walisema watalishughulikia suala hilo.”

 

ADAI MWANAYE AU MAITI

“Ninavyojua mimi mwanangu yuko hai na kama amekufa basi maiti ninayoambiwa ni ya mwanangu ipimwe vinasaba (DNA) vyake na vyangu kuona kama vinashabihiana.

 

SOO LATINGA KWA DC

Kuona hivyo, Anita alisema, mumewe, Jamal Kiumba alikwenda kutoa taarifa hizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sofia Mjema ambaye aliahidi kulishughulikia suala hilo.

Hata hivyo, jitihada za gazeti hili kumpata mkuu wa wilaya huyo ziligonga mwamba na badala yake msaidizi wake aliyefahamika kwa jina moja la Audax alimwambia mwandishi wetu kuwa kiongozi huyo ana taarifa hizo na sasa anasubiri maelezo kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ambaye gazeti hili lilishindwa kumpata ofisini kwake.

 

MSIKIE MGANGA MKUU

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwela alisema mjamzito huyo alijifungua mtoto ambaye baadaye alifarilki dunia akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako ndiko faili lake lilipo hadi sasa.

Hata hivyo, Amani liliwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, ACP Salum Hamduni na kumuuliza kama analijua sakata hilo ambapo alieleza kuwa hajalipata lakini akasema mlalamikaji alitakiwa kutoa taarifa kwenye kituo chochote cha polisi kilicho karibu na mazingira ya tukio badala ya kuchukua hatua za juu alizochukua.

“Lakini nitafuatilia tukio hilo kwa ukaribu zaidi,” aliahidi kamanda huyo.

 

MWANDISHI WETU | AMANI | DAR ES SALAAM

Leave A Reply