The House of Favourite Newspapers

Utoaji wa Namba Kilimanjaro Marathon Waanza kwa Kishindo

0

MAMIA ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walijitokeza katika viwanja vya Mlimani City mwishoni mwa wiki kuchukua namba zao za kushiriki mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2022.

Waandaaji wa mbio hizo walisema muitikio ulikuwa mkubwa kwani washiriki wengi walifika kwa muda na kufanya zoezi liende vizuri.

Wengi waliochukua namba ni washiriki wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager km 42 na Tigo km 21 half marathon huku pia wa km 5 wakijitokeza na wengine wakiendelea kujisajili.

“Usajili kwa ajili ya mbio za km 42 na 21 tayari umefungwa lakini bado tunauza namba za Km 5, walisema waandaaji.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi alisema zoezi hilo lilienda vizuri kwani washiriki walipata namba bila kusubiri muda mrefu.

“Zoezi lilikuwa limepangiliwa vizuri kwani tumeshuhudia washiriki wakiingia na kuondoka kwa haraka,” alisema huku akitoa wito kwa wakazi wa Arusha wajitokeze kwa wingi kwa ugawaji wa namba utakaoanza Jumanne.

Zoezi hilo litafanyika katika Hoteli ya Kibo Palace Jumanne Februari 22, 2022 na Jumatano Februari 23, 2022 kuanzia saa nane kamili hadi saa moja kwa siku hizo mbili.

Zoezi hilo litamalizikia Moshi ambapo namba hizo zitatolewa katika viwanja vya Chuo Kikuu Cha Ushirika Alhamisi Februari 24, 2022 kuanzia saa sita mchana hadi saa kumi na mbili jioni, Ijumaa Februari 25, 2022 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni na Jumamosi February 26, 2022 kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni.

“Washiriki waliojisajili wanatakiwa kuzingatia muda wa zoezi hili katika vituo husika ili kuepusha usumbufu na zoezi likishafungwa hakutakuwa na ugawaji wa namba siku ya mashindano,” walisema waandaaji hao.

Waliongeza kuwa usajili kwa ajili ya mbio za kilomita 5 bado unaendelea kwa njia ya Tigo Pesa kwa kubonyeza *149*20# na kwamba usajili pia utafanyika katika vituo vya kutolea namba.

Wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2022 ni Kilimanjaro Premium Lager (Mdhamini Mkuu) Tigo (21km) na Grand Malt (5km).

Wadhamini wa meza za maji ni pamoja na Absa Tanzania, Unilever Tanzania, TPC Sugar, Simba Cement na Kilimanjaro Water. Wasambazaji rasmi ni GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles na Surveyed Plots Company Ltd (SPC) na Bodi ya Utalii (TTB).

Katika hatua nyingine, Kwa mujibu wa waandaaji wa Kilimanjaro Marathon, kwa mara ya kwanza kutakuweko na maonesho yanayojulikana kama Kili Expo (The People’s Expo) ambapo wadhamini na wadau wengine wa mbio hizo watapata fursa ya siku tatu za kuonyesha bidhaa na huduma wanazotoa, maonyesho ambayo yanatarajiwa kufanyika kati ya Februari 24-26, 2022, katika viwanja vya MoCU.

“Maonyesho haya pia linakusudiwa kuwapa umma uzoefu wa muda mrefu wa mbio za Kili Marathon; pia kwa mwaka huu wanaotarajia kushiriki mbio hizo watapata fursa ya kuchukua namba zao za ushiriki eneo la chuo kikuu cha Ushirika badala ya eneo la hotel kama ilivyokuwa miaka ya nyuma”, ilisema taarifa hiyo ya wandaaji.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 27, 2022, katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ambapo zimeandaliwa na taasisi ya Kilimanjaro Company Limited na kuratibiwa na wadau wa hapa nchini kampuni ya Executive Solutions Limited.

Leave A Reply