The House of Favourite Newspapers

Uwoya Ataja Sababu Kumfanyia Dua Sharo Milionea

0

STAA wa filamu za Kibongo, Irene Uwoya ametaja sababu ya kuamua kumfanyia dua aliyekuwa mwanamuziki na muigizaji marehemu Hussein Ramadhan ‘Sharo Milionea’ ingawa walikuwa hawajuani kabisa.

 

Akizungumza na Amani, Uwoya alisema aliamua kufanya dua hiyo maalumu kwa ajili ya kumuombea Sharo Milionea kwa sababu wasanii baada ya kumzika Sharo Milionea walimsahau kabisa, pia mama yake ikizingatiwa anaishi mkoani na aliyekuwa anamtegemea ndiyo huyo ameondoka.

 

“Enzi za uhai wa Sharo nilikuwa sina hata ukaribu naye, lakini kwa vile alikuwa msanii mzuri, nikaona siyo vyema kabisa kusahaulika kirahisi namna hiyo, ndiyo maana nikafanya mawasiliano na mama yake. Tukamkumbuka kwa kumfanyia dua nyumbani kwao Tanga,” alisema Uwoya.

 

Uwoya aliendelea kusema kuwa alizungumza na msanii mwenzake, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ wakawaambia wasanii wengine ambao aliongozana nao na kufanikisha kufanya dua hiyo kwa gharama zangu ambazo siwezi kuweka wazi ni kiasi gani.

 

“Ninamshukuru sana Mungu kwa kuwa nilichokuwa nimekipanga ndani ya moyo kimetimia. Tumemsomea dua mwenzetu na mama yake kafurahi sana na hilo ndilo nililolitaka,” alisema Uwoya.

Sharo Milionea alifariki miaka saba iliyopita kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha maeneo ya Segera, Muheza mkoani Tanga.

Stori: Imelda Mtema, Amani

Leave A Reply