The House of Favourite Newspapers

Van Persie Amlilia Gyan

0

MCHEZAJI wa zamani wa Manchester United na Arsenal, Robin van Persie ametuma salamu za rambirambi na kutoa heshima kwa mchezaji mwenzake wa zamani Christian Attah Gyan aliyefariki siku ya Jumatano.

Beki huyo wa zamani wa Ghana na klabu ya Feyenoord alifariki dunia Jumatano asubuhi baada ya kuugua saratani kwa miaka kadhaa.

Gyan, mwenye umri wa miaka 43, alifariki katika hospitali moja nchini Uholanzi ambako ameishi kwa muda mrefu.
Gyan alijiunga na klabu ya Feyenoord mwaka 1996, mwaka mmoja baada ya kushinda Kombe la Dunia la FIFA U-17 nchini Ecuador akiwa na Ghana.

Akiwa na klabu ya Feyenoord, Gyan alicheza pamoja na Van Persie, wawili hao wakishinda Kombe la UEFA mwaka 2002 baada ya kuifunga klabu ya Borussia Dortmund mabao 3-2 kwenye fainali. Pia walishinda Kombe la KNVB na Johan Cruyff Shield pamoja katika klabu ya Rotterdam.

Van Persie kupitia ukurasa wake wa Twitter ametoa heshima kubwa kwa beki huyo kwa kuandika. “Nafsi nzuri haisahauliki kamwe. Ulikuwepo kwa ajili yangu katika siku za mwanzo za kazi yangu na uliniunga mkono kama kaka mkubwa.

“Nitashukuru milele kwa kumbukumbu hizo. Pumzika kwa amani Christian…” Gyan alipitia kipindi kigumu baada ya kustaafu mwaka 2010, Mnamo Septemba 2017, mashabiki wa Feyenoord walikusanya €35,500 ili kusaidia gharama zake za matibabu na mambo mengine.

Leave A Reply