The House of Favourite Newspapers

Vanitha: Mume Wangu kwa Mchemsho, Hajambo!

0

Na Imelda Mtema | RISASI JUMAMOSI | MPAKA HOME

Mambo vipi mpenzi msomaji wangu wa safu hii ya Mpaka Home? Kama ilivyo kawaida, tunatinga kwenye nyumba za mastaa mbalimbali Bongo na kuyaibua maisha yao halisi ya kila siku wanayoishi nje ya kazi zao.

Leo nyota wetu ni Vanitha Omary ‘Vanny’ ambaye ni muigizaji wa kitambo sana aliyeibuliwa na Kundi la Fukuto Arts kwenye tamthiliya iliyokuwa ikitamba sana kipindi cha nyuma ya Jumba la Dhahabu huku akiwa amecheza filamu nyingine nyingi.

Vanitha akimlaza mwanaye.

Maisha yake halisi staa wetu huyu anayafanya maeneo ya Mwananyamala jijini Dar akiwa kama mama na mumewe mpenzi aitwaye Paul ambaye pia naye ni muongozaji mkubwa wa filamu.

Safu hii ilizungumza naye mambo mengi na ili kujua yote, twende sasa kwa pamoja hapa chini.
Mpaka Home: Vipi Vanitha, niambie maisha ya kistaa na ya kawaida yana utofauti gani?

Vanitha: Unajua kama mimi japo ni staa lakini maisha yangu hayajawahi kubadilika kwa sababu sijataka kujiweka hivyo maana nilijua wazi huko mbele kuna vitu vingenishinda.

Mpaka Home: Wewe ni mama na pia msanii, unaweza vipi kugawa muda wako ili vyote uvifanye kwa umakini?
Vanitha: Hiyo ni rahisi tu, ni jinsi wewe utakavyojipanga. Mimi hilo halinisumbui kwa sababu najua kupangilia mambo yangu.

Mpaka Home: Kila mtu ana kitu anachopenda kukifanya kama mama wa familia, wewe unapenda nini?
Vanitha: Napenda sana mambo ya jikoni na kwa sababu hiyo hakuna kitu kinachonipiga chenga kinachohusiana na jiko.
Mpaka Home: Ni chakula gani unapenda kumpikia mumeo?

Vanitha: Mume yeye anapenda sana mchemsho hivyo lazima nihusike kuandaa mwenyewe maana msichana wa kazi marufuku kupika chakula cha mume wangu.
Mpaka Home: Wewe ni msanii, mumeo pia msanii, je mngependa watoto wenu wafuate nyayo zenu?

Vanitha: Hapana, wana uhuru wa kujichagulia wenyewe lakini pia mpaka sasa sijaona hata mmoja ambaye anataka kuwa kama sisi.

..Akiwa na familia yake.

Mpaka Home: Muda wako wa kulala ni saa ngapi na pia unapendelea kunywa maji lita ngapi kwa siku?
Vanitha: Mara nyingi mimi na mume wangu muda wetu wa kulala ni saa 5 usiku lakini pia kwa upande wa maji ni mnywaji mzuri, napiga kama lita tatu kwa siku.
Mpaka Home: Ni wageni wa aina gani unapenda wafike nyumbani kwako?

Vanitha akiwa na mumewe.

Vanitha: Sichagui mgeni ilimradi tu awe wa heri kwangu.
Mpaka Home: Hapo mnapoishi ni nyumba yenu au mmepanga?
Vanitha: Hapa tumepanga lakini Mungu akitujalia karibuni tu tutahamia kwetu.

Mpaka Home: Naona kuna mtoto mchanga, ni wako? Kama ni wako, unao wangapi?
Vanitha: Ndiyo, nimejifungua miezi miwili iliyopita na nina wengine wawili, msichana na mvulana hivyo nina watatu sasa.
Mpaka Home: Nakushukuru sana Vanitha kwa ushirikiano.
Vanitha: Karibu tena.

HOTUBA YA RAIS MAGUFULI UZINDUZI WA MABWENI MAPYA UDSM

Leave A Reply