The House of Favourite Newspapers

Vijue vyakula vya kuongeza wingi wa damu

UPUNGUFU wa damu ni ile hali ya kiasi cha damu mwilini kuwa kidogo kuliko kinachotakiwa na mwili kulingana na hali ya mtu na jinsia yake. Hali hiyo hupimwa maabara na hospitali kwa kuangalia kiasi cha Haemoglobin, (HB).  Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha upungufu wa damu ila kwa leo nitazungumzia jinsi ya kupandisha kiwango cha damu kwa haraka kwa kutumia vyakula au matunda.

Katika hali ya kawaida mwanaume hutakiwa kuwa na damu kati ya 13.5 hadi 17.5 (g/dl) na wanawake hutakiwa kuwa na damu kati ya 12.0 hadi 15.5 na kwa mjamzito kikawaida kiasi cha damu inatakiwa kuwa kati ya 11-12g/dl. Tofauti hiyo husadikiwa kwamba huletwa na hedhi ambayo wanawake hupata kila mwezi na hivyo kuwa na damu pungufu kidogo ukilinganisha na ya wanaume. Vitu vya kupandisha damu bila kutumia dawa ni:

  1. JUISI

Sio juisi zote huongeza kiwango cha damu, unashauriwa kunywa juisi ya nyanya, walau kila siku glasi mbili lakini pia juisi za rozella, tikitimaji na karoti. Aina hizi za juisi huongeza kiwango cha damu kuliko hata vidonge.

2.VYAKULA:

Kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya chuma, vyakula hivyo ni kama nyama, maini, maharage na viazi vitamu.

  1. MATUNDA

Kama ilivyo kwa vyakula na juisi, sio matunda yote yanaongeza damu, tunakushauri utumie matunda yafuatayo katika kuongeza damu. Maembe, machungwa, strawberries, cabeji zabibu, nyanya pamoja na spinach huongeza damu. Tunakushauri pindi unapokua na upungufu wa damu usitumie vyakula vyenye iron blocker; vyakula au vinywaji hivi huzuia madini ya chuma yasiweze kufyonzwa mwilini.

Vyakula hivyo ni pamoja na: kahawa, maziwa, siagi na chocolate. Utafiti unaonyesha takribani wajawazito asilimia 15 hadi 25 hupatwa na upungufu wa damu mwilini yaani anemia. Wengine huwa na ukosefu au upungufu wa virutubisho vya vitamini aina ya foleti. Foleti hupatikana katika mboga za majani kama matembele, malimao, ndizi, parachichi, machungwa, mapapai, maharage na karoti.

Pia kuna upungufu wa vitamini B12, ambayo ni muhimu kwenye uzalishaji wa chembe nyekundu za damu zenye kazi ya kusafirisha oksijeni kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu. Hata hivyo, tofauti na ukosekanaji wa aina hizo, kuna sababu nyingine huchangia upungufu wa damu.

Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na matatizo kwenye mfumo wa chakula unaosababisha kupoteza damu hasa kwa kipindi cha muda mrefu, nyingine ni maradhi kama malaria, Ukimwi, tatizo la seli mundu linalofahamika kwa jina la ‘sikoseli’, minyoo hasa ile inayonyonya damu katika mfumo wa chakula.

Sababu zinazosababisha mjamzito kupata tatizo la upungufu wa damu ni pamoja na kubeba mimba zinazofuatana katika kipindi kifupi baada ya kujifungua. Upungufu wa lishe yenye madini ya chuma, ujauzito wenye mapacha, kutokuwa na damu nyingi katika hedhi kabla ya ujauzito pamoja na kutapika sana wakati wa homa za asubuhi.

DALILI ZA UPUNGUFU WA DAMU

Tatizo hili la upungufu wa damu huambatana na dalili za maumivu ya kifua, kukabwa na

pumzi, uchovu usio wa kawaida, maumivu ya kichwa hasa upande wa mbele, mapigo ya moyo kwenda haraka kwa sababu katika kipindi hicho hemoglobin ya kusafirisha oksijeni mwilini huwa chache kutokana na upungufu wa madini ya chuma.

Hali hiyo husababisha moyo kupampu damu kwa haraka zaidi ili kuhakikisha oksijeni inasambaa katika sehemu mbalimbali za mwili kukidhi mahitaji, kupauka kwa ngozi na kucha, mikono na miguu kupatwa na ubaridi, kutoweza kufikiria kwa makini, kwa sababu ubongo unakuwa unahitaji oksijeni wakati wote.

Madhara ya upungufu wa damu kwa wajawazito ni pamoja na kuongeza uwezekano wa kujifungua mtoto chini ya uzito wa kawaida, kuathiri ukuaji wa mtoto, matatizo katika ukuaji wa ubongo na uti wa mgongo, mimba kutoka kabla ya wakati na mtoto kupoteza maisha akiwa tumboni.

Uwezekano wa mama kupoteza maisha wakati wa kujifungua unaongezeka kama atapoteza damu nyingi wakati huo, husababisha pia matatizo ya moyo na mapafu na huongeza hatari ya kushambuliwa na maradhi mbalimbali. Wakati wa ujauzito ni muhimi kuhudhuria kliniki kwa ajili ya ushauri.

USHAURI

Ni vyema kula vyakula na matunda tuliyoshauri na tatizo likizidi kamuone mtaalamu wa afya.

Unashauriwa ili kuwa na kinga dhidi ya tatizo hili epuka kuwa na minyoo, kula lishe bora inayojumuisha madini ya chuma ikiwamo nyama, kuku, samaki, mayai, maharage, mboga za majani kama spinachi na vyakula vyenye vitamin C kama juisi ya machungwa.

Comments are closed.