The House of Favourite Newspapers

Vilio, Simanzi Vyatawala Mazishi ya Mtoto Mourine Aliyetekwa Arusha

0
Maofisa wa Usalama wakiwa msibani hapo.

VILIO na simanzi vimetawala leo katika Jiji la Arusha huku maelfu ya waombolezaji wakijitokeza kuuzika mwili wa mtoto Maureen David (6) aliyetekwa na kisha kuuawa kwa kutupwa ndani ya shimo la maji taka akiwa na mwenzake Ikram Salim(3).

 

Akiongoza Ibada ya mazishi hayo yaliyofanyika katika Makaburi ya Mbauda Jr, Kata ya Sombetin, Padre wa Parokia ya Tokeo la Bwana Burka, Lawrence Boniphace  aliwataka wazazi wa marehemu kuhakikisha wanamsamehe kila mtu aliyeshiriki katika mauaji ya mtoto wao na kujitayarisha kuanza kuishi maisha mapya bila kuwa na kinyongo.

 

 

Ibada ya kuaga mwili wa marehemu ikiendelea.

 

“Katika maisha yetu tunakutana na watu ambao hawajali maisha ya binadamu kwa hivyo ninaomba wazazi wa marehemu msamehe kwasababu mnaposamehe mnaanza maisha mapya”alisema Padre Lawrence .

Akizungumza mara baada ya zoezi la kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema serikali mbali na kutoa rambirambi ya jumla ya kiasi cha Sh. Milioni 2, aliwataka wakazi wa Arusha kuwa watulivu katika kipindi hiki na kusema  serikali ilifanya jitihada zote kuwasaka na kuwakamata wahalifu katika tukio hilo.

 

 

Waombolezaji wakiaga mwili wa marehemu.

 

Gambo, aliyekuwa ameambatana na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha alisema kuwa jitihada za kumtia nguvuni mhalifu zilifanikishwa na vyombo vya ulinzi vya mkoani Arusha kwa kushirikiana na vilivyoko mkoani Geita na kuwataka wakazi wa Arusha kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wahalifu mbalimbali.

Hatahivyo, alisema kwamba kutokana na ukubwa wa kata ya Olasiti serikali kwa kushirikiana na Mutahaba watajitahidi kuhakikisha wanahamasisha ujenzi wa Kituo kikubwa cha Polisi ndani ya kata hiyo kama njia mojawapo ya kuzuia matukio ya uhalifu .

 

 

Waombolezaji wakihuzunika.

 

Baba mzazi wa marehemu, David Njau alisema  ya kwamba tukio la kufiwa na mwanaye linasikitisha kwa kuwa hivi karibuni mtoto wake wa kwanza aitwaye, Jenipher David ambaye ni mhitimu wa darasala saba katika shule ya Lucky Vincent alinusurika katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Karatu.

 

“Ninasikitika sana na hata kuishiwa nguvu kwakuwa ni hivi karibuni tu mtoto wangu wakwanza aitwaye Jenipher alinusurika katika ajali ya gari iliyoua wanafunzi kule wilayani Karatu yeye gari lao halikupata ajali kwa kuwa lilitangulia mwanzoni” alisema David.

 

Ibada ikiendelea.

Alisema ya kwamba jeshi la polisi lilikuwana uwezo wa kuzuia kifo cha mwanaye kwa kuwa kwa takribani wiki nzima alikuwa akiwasiliaana na wahalifu wakimtaka awapatie kiasi cha fedha ili wamrejeshe mwanaye lakini pamoja na kutoa taarifa kwa jeshi hilo lakini halikuweza kuwakamata wahalifu.

“Nina uhakika kabisa kama polisi wangeweza kutoa ushirikiano wa kutosha wahalifu wangekamatwana mtoto wangu asingefariki katika mazingira ya ajabu nilijitahidi kuwapa taarifa zote za wahalifu lakini sikupewa ushirikiano,” alisema David.

Hatahivyo,alisisitiza ya kwamba tukio hilo linapaswakuwa funzo  kwa jeshi la polisi pindi wanapopewa taarifa kuhusu wahalifu wanapaswa kuchukua hatua za haraka kabla ya kusubiri majanga yajitokeze.

 

Joseph Ngilisho, Global Publishers, Arusha.

 

Leave A Reply