The House of Favourite Newspapers

Vilio vya Maombi ya Corona Vyatawala

0

SIKU tatu za maombi maalum kwa ajili ya kudhibiti Virusi vya Corona, zimetimia juzi huku vilio kutoka kwa waumini na viongozi wa madhehebu mbalimbali nchini vikitikisa katika kumlilia Mungu ili aliepushe Taifa na janga hilo.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais Dk John Magufuli ‘JPM’ kuwataka Watanzania kutenga muda wa siku tatu, kuanzia Aprili 17 hadi 19, mwaka huu kufanya maombi maalum ya kudhibiti virusi hivyo nchini.

Maombi ya aina hiyo yamefanyika kwa mara ya kwanza tangu janga hilo kupiga hodi katika nchi za Afrika na kiongozi an chi kutaka wananchi wake kutenga muda wa siku hizo kwa ajili ya kufanya maombi dhidi ya Corona.

 

HALI ILIVYOKUWA

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilitinga katika makanisa mbalimbali jijini Dar na kushiriki maombi hayo maalum wakiwemo wananchi waliojumuika na Mchungaji Kiongozi, Dk Getrude Rwakatare wa Kanisa la Mlima wa Moto, Mikocheni B.

Waumini hao walimlilia Mwenyezi Mungu ashushe uponyaji kwa Watanzania na dunia kwa jumla kwa kuwa pigo lililotokea sasa, limetosha kuwa funzo kwa watu wote.

 

Vivyo hivyo kwa upande wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Dk Josephat Gwajima aliendelea kunukuu mstari wa Biblia uliotumiwa na Rais Magufuli kuhamasisha Watanzania kuliombea Taifa.

“Rais alisema Mambo ya Nyakati wa pili, 7: 14, Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu, wakijinyenyekeza na kuomba na kuziacha njia zao mbaya, nitawasikia kutoka mbinguni, nitawasamehe makosa yao na kuiponya nchi yao.

 

“Hofu iliyo nyuma ya Corona ni kubwa kuliko Corona yenyewe, pili ni kujua kuchukua tahadhari zinazotolewa na wizara ya afya. Pia ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo. Mambo yote tunayoyafanya ni kujaribu kuzuia, alisema.

 

Kwa upande wake Askofu Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), naye alionya kuwa tunapoelekea kumuomba Mungu atuepushe na janga la Corona, tuwakumbuke kipekee wahudumu wa afya ambao wako mstari wa mbele kusaidia wale walioathirika. Hawa ndiyo mashujaa wetu kwa sasa.

 

“Lakini pia tuwakumbuke mamlaka za nchi ili Mungu awajaalie hekima ya kuweka mikakati ya kukabiliana na janga hili. Katika umoja na mshikamano wetu tutavuka, Bwana uturehemu,” alisema.

 

Maombi hayo yaliyoshushwa kwa njia mbalimbali ikiwamo mitandao ya kijamii, redio na televisheni na wachungaji, wananchi pamoja na mashehe na Waislam.

Dk Eliona Kimaro wa Kanisa la KKKT-Kijitonyama, kwa upande wake alitoa neno kuu kutoka katika kitabu cha Biblia cha Jeremia 30: 17.

“Biblia inasema; Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako zote, asema Bwana.”

 

Alisema maombi ya Watanzania yalenge kuwarudishia afya wale ambao wanaishi na magonjwa sugu.

“Mungu awarudishie afya. Pia aponye majeraha yote ya ndani na nje, ya kisaikolojia na ya kawaida hasa majeraha ya kiuchumi na kifedha.

“Nimefuatilia hali ya uchumi wa dunia wakati huu wa Virusi vya Corona, Marekani imepoteza ajira 5,000 ambazo zilitengenezwa kwa muongo mmoja sawa na miaka 10,” alisema.

 

Kwa upande wake, Nabii Esther Bukuku wa Kanisa la Prophetic Ministry International (PMIC) aliendesha Ibada kwa siku tatu ambapo waumini walipaza sauti kumuomba Mungu ili amzime shetani wa Corona.

“Baada ya maombi haya, sasa Corona ipo nyang’anyang’a, sisi kama kanisa tunasubiria majibu kutoka kwa baba yetu aliye mbinguni.

 

Aprili 16, mwaka huu, Rais Magufuli alituma ujumbe kwa njia ya akaunti yake ya Twitter na kuwataka Watanzania watenge muda wa siku tatu kwa ajili ya dua na sala zao kwa Mwenyezi Mungu ili apate kuliepusha taifa na janga hilo la Corona lililopiga hodi kwa mara ya kwanza nchini Machi 16 hadi Aprili 18 watu 147 wamethibitishwa kuambukizwa.

STORI: MWANDISHI WETU, DAR

CORONA UPDATE, ONGEZEKO LA WAGONJWA WA CORONA | VIFO VYAONGEZEKA, MAJALIWA KUONGOZA MAOMBI

Leave A Reply