The House of Favourite Newspapers

Vipimo Kwa Wasioshika Mimba

0

pregnant-black-womanBAADA ya kusoma sababu za wanawake na wanaume kushindwa kushika mimba, leo tutaangazia vipimo vya kubaini tatizo. Lengo la kufanya vipimo ni kujua sababu zinazoweza kumfanya mwanamke asishike mimba na mwanaume ashindwe kutungisha mimba.

Ili kugundua hitilafu au ugonjwa na kuutibu, ni vyema kukaa na wanandoa na kuwasikiliza na baadaye kuwajulisha kinachowasibu na kuwapa ushauri nasaha.

Wanandoa wakishafikisha mwaka mmoja ndani ya ndoa huku wakifanya tendo la ndoa bila kutumia kinga kama vile kondomu mara kwa mara au uzazi wa mpango lakini bado mwanamke akashindwa kubeba ujauzito, basi wanatakiwa waongozane wote wawili wakamuone daktari mwenye utaalamu huo.

Watafanyiwa vipimo vya msingi kama vile kupima mbegu za kiume (semen analysis), kujua na kupima muda wa kupevuka mayai ya mwanamke, kitaalamu confirmation of ovalution pia kuchunguza afya ya kizazi na mirija.

Ni lazima wanandoa wakaongozana ili wakachukuliwe maelezo yao baada ya kuulizwa maswali ya kitabibu kuhusiana na uzazi, kwa mfano, kama kuna mmoja wao au wote wawili waliwahi kuwa na ujauzito kwa mwanamke na kumshikisha ujauzito mwanamke kwa mwanaume.

Vipimo hufanyika kwa kila mmoja kwa wakati wake, yaani atapimwa peke yake na wote wataulizwa kama wamewahi kupata magonjwa ya zinaa.

Mwanaume ataulizwa kama amewahi kuumwa tezi za sikio (mumps) kipindi ana balehe au kama amewahi kupata ugonjwa wa kisukari au kuumwa kwa kujirudiarudia ugonjwa wa kifua kikuu (TB).

Mwanaume pia ataulizwa kama aliwahi kufanyiwa upasuaji wa mirija ya uzazi pia atahojiwa kama anatumia pombe au kuvuta sigara.

Mgonjwa atachunguzwa na daktari kuanzia kichwani hadi miguuni lakini vipimo vingine vya awali kama kipimo cha mkojo na kupima damu kugundua kama ana tatizo la kisukari vitafanyika.

Atapimwa pia vipimo vya ndani kama damu kwenye vichocheo (hormones) kama FSH, LH, Testosterone, Prolactin na TSH. Vipimo hivi hufanywa hospitalini, tena zile kubwa. Kipimo cha Ultrasound pia kinaweza kutumika  kwa akina mama au hata akina baba daktari akiona inafaa.

Daktari pia atachunguza kama wana maambukizi na vijidudu (infections) katika uke na mdomo wa kizazi (cervix). Pia hupimwa kwa kufanyiwa laparoscopy.

Kwa kawaida, baada ya vipimo vyote itafahamika kwamba tatizo lipo wapi. Wengi huwa wanaamini kwamba matatizo ya kutoshika mimba yanawahusu wanawake pekee lakini dhana hii si sahihi.

Inaweza kutokea pia kwamba mwanamke akawa hana tatizo kwa maana kwamba anachavusha (ovulate) mayai yenye ubora na sifa zinazotakiwa lakini mwanaume akawa anazalisha mbegu za kiume (sperms) ambazo zinashindwa kutungisha mimba ndiyo maana inapotokea tatizo kama hili, inabidi wanandoa wote washirikiane.

Pia ni makosa kukata tamaa kwa sababu ya kuchelewa kupata ujauzito au kukimbilia tiba za mitishamba bila kujua tatizo la kitaalamu linalowakabili. Wapo wanandoa ambao walikaa wengine mpaka miaka kumi bila mtoto lakini baada ya kuamua kushirikiana kutafuta suluhu ya matatizo yao, leo wanalea watoto wao.

Kwa hiyo hata wewe msomaji ikiwa una matatizo kama hayo, hutakiwi kukata tamaa kwa sababu kila kitu kinawezekana. Fuata taratibu nilizozieleza kuanzia mwanzo wa makala haya naamini utafanikiwa.

Dk. Marise anapatikana Marise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta.

Semina Kubwa ya Eric Shigongo Ilivyowafungua Akili Vijana: Part 1

Semina ya Eric Shigongo Iliyowainua Vijana Kiuchumi, Part 2

Leave A Reply