Matukio ya kuuawa kwa viongozi wa juu wa nchi duniani yamekuwa yakipingua kasi katika miongo ya hivi karibuni, lakini hata kwa uchache wake bado yanatokea.
Kifo cha jana Rais wa Haiti Jovenel Moïse aliyeuawa kwa kushambuliwa kwa risasi akiwa kwenye makazi yake, katika mji mkuu, Port-au-Prince ni mfano mmoja tu wa viongozi wakuu wa nchi zaidi ya 100 kuuawa katika kipindi cha miongo 10 iliyopita.
Ripoti moja iliyochapishwa mwaka 1998 nchini Marekani ya Military Medicine (Vol. 163), inaonesha kati ya mwaka 1965 mpaka 1996 viongozi wakuu wa nchi 261 walifariki, kati yao viongozi 118 walifariki wakiwa madarakani huku asilimia 44% ya viongozi hao waliuawa. Kati ya Viongozi 144 waliofariki baada ya kutoka madarakani, asilimia 11% waliuawa.
Matukio ya kuuawa kwa viongozi hao yanatokea duniani kote, lakini mara nyingi zaidi hutokea katika nchi za masharki ya kati, Asia ya Kusini na nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.
Ukiacha viongozi wengi huko nyuma kama John Kennedy wa Marekani, Park Chung-hee wa Korea Kusini, Francois Tombalbaye wa Chad, Hafizullah Amin wa Afghanistan, Anwar Sadat wa Misri na Thomas Sankara wa Burkina Faso, BBC inakuletea baadhi tu ya marais hasa kutoka Afrika ambao waliouawa kwa kushambuliwa kwa risasi wakiwa madarakani.
1: Idriss Deby – Chad
Deby ameiongoza Chad kwa miaka 30 mpaka Aprili 2021, alipouawa wakati akiongoza majeshi ya nchi hiyo kukabiliana na waasi waliokuwa wanataka kumuondoa madarakani.
Kifo chake kilitokea siku moja tu baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa 2021, akipata asilimia 80% ya kura zote katika uchaguzi huo wa April 11, 2021.
Deby aliingia madarakani kwa mapinduzi na kumfurusha aliyekuwa Rais na mkubwa wake jeshini, Hissene Habre. Hata hivyo uhusiano wao ulianza kuyumba mapema tu baada ya Habre kumtuhumu Deby kutaka kumpindua. Deby akatimkia Libya baadae Iraq alipokusanya nguvu na kurudi nchini Chad mwaka 1989 na kumfurusha Habre.
Hata hivyo uasi kwa mika kenda na kenda unaitafuna Chad, ambayo ni moja ya nchi masikini kabisa duniani, ambapo zaidi ya nusu ya watu wake milioni 15.8 wanaishi kwenye umasikini wa kutupwa.
Kulikuwa na vikundi vya waasi vilivyoendesha mapigano ya kumuondoa madarakani Deby, ambavyo vilifanikiwa kumchapa risasi walipoukaribia mji wa Djamena na kumjeruhi kabla ya kupoteza maisha.
2: Sheikh Abeid Aman Karume – Zanzibar
Alikuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar na makamu wa kwanza wa Rais wa Tanzania. Anaheshimika sana visiwani humo kwa jitihada zake za kuileta Zanzibar pamoja, lakini pia kuviunganisha visiwa hivyo na Tanganyika na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania.
Sheikh Karume aliuawa kwa kupigwa risasi katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro-Shirazi (ASP) visiwani mjini Zanzibar mnamo tarehe 7 Aprili, 1972.
Anatajwa mmoja wa walinzi wake kufanya shambulio hilo ingawa hakuna uhakika wa hilo mpaka leo, kutokana na kutowekwa wazi kwa taarifa rasmi ya kifo cha kiongozi huyo ambaye hawezi kusahaulika katika historia ya ukombozi wa visiwani humo kutokana na misingi aliyowajengea Wazanzibar.
3: Muammar Gaddafi – Libya
Anakumbukwa kwa ubabe wake wa vita uliomsaidia kuingia madarakani mwaka 1969. Alikamatwa na kuteswa kiasi kabla ya kuuawa Oktoba 20,2011, kufuatia mapigano yaliyoitwa ‘Battle of Sirte, kati ya wanajeshi wanaomtii na wanajeshi wa NTC wasiomtii kiongozi huyo.
Alikutwa amejificha kwenye kalavati dogo kuwakwepa wanajeshi hao. Zilisambaa video zikiwaonyesha waasi wa NTC wakimpiga kiongozi huyo ambao baadae walimmaliza kwa kumpiga risasi kadhaa. Baade kukaja ripoti ambayo haijathibitishwa kwamba alijiua mweyewe kwa bastola yake. Ripoti inayopingwa na waliokuwa walinzi wake.
Pango alikomatwa Gaddafi
Waziri mkuu wa NTC , Mahmoud Jibril, ndiye aliyetangaza kifo chake akisema amefariki kwa majeraha ya risasi, ingawa hakusema risasi hizo zimepigwa na nani.
Mwili wake ulihifadhiwa kwenye jokofu maalumu na kwa siku kadhaa ili kuwapa nafasi raia washuhudie kwamba kiongozi huyo hayuko hai tena.
4: Laurent-Desire Kabila – DR Congo
Alikuwa Rais wa tatu wa DR Congo wakati huo inaitwa Zaire. Aliongoza nchi hiyo kuanzia mwaka Mwaka 1997 mpaka alipouawa Januari mwaka 2001. Baada ya kuingia madarakani kwa kumfurusha Mobutu Seseseko, Kabila alibadilisha katiba na kurejesha jina la DRC na kulifuta jina la Zaire.
Alipigwa risasi ofisini kwake January16 2001 na kukimbizwa Zimbabwe kwa matibabu. Kifo chake kilitangazwa January 18, ingawa waziri wa afya wa wakati huo, Leonard Mamba aliyekuwa chumba cha pili cha ofisi wakati shambulio likitekelezwa alieleza kwamba Kabila alifariki papo hapo.
Wanajeshi wakibeba mwili wa Kabila
Wiki moja baadae mwili wake ulirejeshwa DRC kwa ajili ya mazishi ya kitaifa, kabla ya mtoto wake Joseph Kabila kumrithi na kuwa Rais wa nchi hiyo siku 10 tu tangu baba yake Kabila auawe. Zaidi ya watu 130 walihusishwa na njama za kifo chake akiwemo mmoja wa wapwa zake na kuhukumiwa adhabu mbalimbali.
5: João Bernardo Vieira – Guinea Bissau
Vieira aliongoza Guinea-Bissau kwa vipindi vitatu tofauti, alianza mwaka 1980 mpaka1984, akaendelea kipindi cha pili 1984 mpaka 1999, na kipindi cha tatu ilikuwa mwaka 2005 mpaka 2009. Baada ya kuingia madarakani mwaka 1980, Vieira aliiongoza Guinea-Bissau kwa miaka 19 mna akashinda uchaguzi mkuu wa vyama vingi wa mwaka 1994.
Hata hivyo vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1998-1999 vilisitisha utawala wake na kutimkia ng’ambo. Akarejea kwenye siasa mwaka 2005 na kushinda uchaguzi wa rais.
Hata hivyo miaka mine baadae (Machi 2, 2009) akauawa na wanajeshi wake , masaa machache baada ya kuuawa kwa mkuu wa majeshi Jenerali Batsta Tagme Na Waie. Ripoti za kifo chake haziko wazi sana, wapo wanaoamini kauawa kwa bomu na wengine kauawa kwa risasi na baadae bomu.
Vieira Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Vieira, alisema kiongozi huyo alipigwa vikali kabla ya kumalizwa kwa risasi.
Hata hivyo Jeshi la nchi hiyo lilikana kuhusika na kuuawa kwake, baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba, Jeshi lililipiza kisasi baada ya baadhi ya wanajeshi kumtuhumu Rais Vieira kuhusika kuuawa kwa Jenerali Waie. Wakati wa utawala wake Vieira aliitambulisha kama zawadi ya Mungu “God’s gift” kwa nchi ya Guinea-Bissau.
6: Samuel Doe – Liberia
Samuel K. Doe alikuwa Rais kuanzia Aprili 12, 1980 akiongoza mapinduzi ya kijeshi ya Monrovia yaliyomuondoa madarakani William Tolbert.
Samuel Kanyon Doe, mwanajeshi na nguli la vita, aliyeingia madarakani kwa mtutu wa bunduki akiwa na wanajeshi wenzake 17 tu na kuwa rais kwa miaka 10 kati ya mwaka 1980 na 1990. Anatambulika kwa utawala wake uliogubikwa na giza kuhusu vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu.
Alitajwa kukandamiza zaidi wapinzani wake kiasi cha kuzua kasheshe la kupingwa na kukataliwa wazi hali iliyotikisa sana serikali yake.
Uchaguzi wa mwaka 1985 alioshinda ulitajwa kuwa wa udanganyifu mkubwa na kuanzia hapo akaanza kuandamwa na wapinzani wake akiwemo Yormie Johnson na Charles Taylor aliyeongoza kundi la National Patriotic Front ili kumuondoa madarakani.
Kukazuka vita kati ya kundi la Taylor na Doe, vita iliyowakimbiza maelfu ya raia kwenda kutafuta usalama nchi jirani ya Ivory Coast.
Akiwa njiani kukimbia nchi Septemba 9, 1990 akiwa na walinzi wake karibu 60 lilivamiwa na kundi la Yorme Johnson na akauawa siku iliyofuata. Ukawa mwisho wa Doe aliyetajwa kuwa mmoja wa viongozi madikteta Afrika katika utawala wake wa miaka 10 uliosababisha vifo vya raia wengi wa Liberia.
7: Jenerali Ibrahim Baré Maïnassara- Niger
Maïnassara aliiongoza Niger kwa miaka mitatu kabla ya kuuawa mwaka 1999. Maïnassara, mwanajeshi anayetokea kabila la dogo la Maouri katika jamii yenye watu wengi ya Hausa aliyeitawala Niger kwa miaka mitatu kati ya mwaka 1996 mpaka 1999.
Kupitia katiba iliyoondoa utawala wa kijeshi mwaka 1991, kufika mwezi Machi mwaka 1995 Maïnassara akawa Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo.
Uchaguzi wa bunge wa Januari 1995 ulisababisha mvutano mkubwa kati ya Rais wa wakati huo Mahamane Ousmane na bunge lililokuwa na wabunge wengi wa upinzani chini ya waziri mkuu Hama Amadou.
Uhasama wa viongozi hawa ukasababisha serikali kudorora na kuwa hoi bin taabani, na hapo ndipo Maïnassara kama mkuu wa majeshi akachukua madaraka na kuwa rais kuanzia January 27, 1996.
Maïnassara alisema , hawezi kuona nchi inadorora kwa sababu Rais na waziri wake mkuu wanasigana, akashika hatamu mpaka alipouawa na walinzi wake Aprili 9, 1999, akielekea kupanda helkopta katika jiji la Niamey kuelekea nje ya nchi.
Ikalezwa kwamba ni Jeshi lilimuua na kufanya mapinduzi ya kiungozi. Ingawa ripoti zingine zinasema aliuawa kwa bahati mbaya hakuwa mlengwa wa shambulio hilo.
Baada ya kifo chake Waziri mkuu Amadou na viongozi wengine wa juu walijitagaza marais, ndipo kiongozi wa kijeshi Daouda Malam Wanke akaingilia kati na akajitangaza Rais Aprili 11, 1999 katika hatua iliyotajwa kama mapinduzi ya makusudi yaliyopangwa.
Hata hivyo Wanke aliyekuwa anasumbuliwa na maradhi na kujikuta akitumia muda mwingi nje ya nchi kwa maatibabu aliachia madaraka miezi tisa baadae kwa kiongozi wa kuchaguliwa Mamadou Tandja, ilikuwa Deceber 1999.
MTOTO AKATWA MGUU BABA AILILIA HOSPITALI – “WALISHINDWA KUTUPA MSAADA WA AMBULACE, SHIDA MIL2”