MOYO wangu ulijaa hamu kubwa ya kufikisha ujumbe kwa Mtukufu Aga- Khan, tena mbele ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba hospitali yake ilikuwa ikiteleza katika utoaji wa huduma, hasa kitendo cha kukataa kupokea wagonjwa waliotumia Bima ya Afya ya Taifa (NHIF).
Wakati ninampa maelekezo Katibu Mhutasi wangu kuandaa bango ambalo ningeenda nalo Uwanja wa Ndege wa Mwalimu JK Nyerere wakati wa mapokezi ya Aga-Khan, ilikuwa ni mchana wa siku ya Oktoba 10, 2017, siku iliyofuata ndiyo Aga-Khan angewasili nchini saa nne asubuhi!
“Hakikisha bango hilo linakuwa tayari kufikia kesho saa moja asubuhi, umenisikia Glory?”
“Nimekusikia.” Alinijibu kwa njia ya simu kutokea mapokezi.
Ukiwa na siri nzito moyoni, kuna mambo hutakiwi kumshirikisha mtu yeyote, hata mkeo au mtu mwingine anayekupenda au kukutakia mema, nikalala mpaka asubuhi ingawa usingizi wangu ulikuwa wa mang’amung’amu, kichwani nikifikiria ambacho kingetokea uwanja wa ndege, pale ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania angenishuhudia katikati ya watu, peke yangu tu nikiwa nimeshika bango lenye maandishi: “Mr President ask Aga-Khan, why doesn’t he accept NHIF Insurance at his main hospital, while he doesn’t pay us tax?”
Kama kawaida ya binadamu unapowaza, kuna upande utakueleza unachokifanya siyo sahihi, mara nyingi upande huu huonekana kuwa na nguvu zaidi ya ule unaokuambia ni sahihi, ndivyo ilivyokuwa, nilianza kusikia sauti zikiniambia: “Rais atakasirika.” Niliamua kuzipuuza sauti hizo kwa sababu niliamini katika kitu nilichokuwa nikikipigania, nikasema: “Litakalokuwa na liwe!”
Niliamini na mpaka sasa ninaamini kitendo cha Hospitali ya Aga-Khan, kubwa na yenye vifaa vya kisasa kuliko hospitali nyingi nchini Tanzania, haitendi haki kwa Watanzania inapogoma kupokea na kutibu wagonjwa wenye bima za afya! Hilo ndilo nililokuwa nikilipigania.
Nilijua na ninajua kwamba Hospitali ya Aga-Khan inaweza kujitetea kuwa inapokea wagonjwa wa bima ya afya kwenye hospitali zake za pembeni, ambazo kwa hakika hazina vifaa wala madaktari bingwa wa kutosha, hawafanyi hivyo kwenye hospitali yao kubwa yenye vifaa vyote na madaktari wa kutosha, najua pia wanapokea wagonjwa wa bima ya afya wa daraja la juu kama wabunge n.k.
Nilichokuwa ninakipigania hapa kwanza ni usawa, haki ya kupata matibabu na kuishi ni ya kila Mtanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzisha Mfuko wa Bima ya Afya ili wananchi wake waweze kupata matibabu popote, sasa iweje Aga-Khan wakatae kwenye hospitali yao kubwa na kuwasukumia wagonjwa kwenye vihospitali vyao vya pembeni visivyo na huduma nzuri?
Ziko hospitali nyingi tu binafsi hapa nchini, zinazokubali wagonjwa wa huduma ya afya, miongoni mwa hospitali hizo ni TMJ, Regency, Tumaini na Burhan, kwa nini Aga-Khan wakatae? Kibaya zaidi wakati wanawakataa wagonjwa wa bima ya afya hawatulipi kodi yoyote ile kwa kisingizio kwamba ni shirika la kidini lisilotengeneza faida yoyote.
Lisilotengeneza faida? Huu ni uongo wa karne, ukitaka kuthibitisha hili kipimo kama MRI (Magnetic Resonance Imaging) katika Hospitali ya Aga- Khan kinatozwa shilingi za Kitanzania 720,000 ukiongeza na dawa ya kufanya picha itoke vizuri, yaani ‘contrast’ utalipa 200,000 zaidi, lakini kipimo hicho hicho kwenye hospitali inayotulipa kodi, ya TMJ iliyoko Mikocheni jijini Dar es Salaam ni shilingi 670,000 na kwa Muhimbili ambayo ni hospitali ya serikali ni shilingi 320,000, sasa iweje Aga-Khan wadai hawapati faida wakati Hospitali ya TMJ inayolipa kodi serikalini inatoza kiasi kidogo.
Mheshimiwa Rais, Waziri wa Afya, Naibu, Katibu Mkuu wa Wizara na Watanzania wote, wakati umefika serikali yetu kuzichunguza taasisi za kidini, kwani inaonesha baadhi zinajificha kwenye neno “Taasisi ya Dini” na kukwepa kodi za mabilioni ambayo yangesaidia maendeleo ya taifa letu, sikubaliani kabisa mtu akiniambia eti hospitali kama Aga-Khan haipati faida, wakati gharama zake ni kubwa kuliko hospitali zinazolipa kodi, kujifungua tu katika Hospitali ya Aga-Khan ni shilingi milioni mbili za Kitanzania, halafu wanadai hawapati faida na tukubaliane nao, no way!
Nilipoingia ofisini asubuhi ya Oktoba 11, 2017 kichwani mwangu nilikuwa nikifikiria kitu kimoja tu; safari ya uwanja wa ndege, dereva alikuwa tayari na nilikuwa nimeomba waandishi wa habari wa Global TV Online niongozane nao ili warushe tukio hilo live, cha kwanza nilichokifanya ni kumuuliza Katibu Mhutasi wangu kama bango lilikuwa tayari.
“Bado halijaletwa.”
“Lazima unanitania, tangu jana?”
“Wanadai wanamalizia na watalileta muda si mrefu.”
“Sawa.”
Mpaka saa tatu kamili, bango lilikuwa halijaletwa, nikaanza kuishiwa na uvumilivu, lakini ilipohitimu saa tatu na nusu ndiyo nikaletewa bango ofisini, tayari nilishachelewa, nisingeweza kuwahi uwanja wa ndege tena, nikampigia simu Mtangazaji wa Channel Ten, Said Makala kumuuliza kilichokuwa kikiendelea uwanja wa ndege, akanieleza Aga- Khan alishawasili na tayari alikuwa njiani kuelekea mjini, Waziri wa Elimu, mama Ndalichako na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ndiyo waliompokea.
Nikafungua mlango wa gari na kulitupa bango ndani yake kisha kupandisha tena ofisini kwangu nikiwa nimevunjika moyo, mtu fulani alikuwa amekwamisha kazi niliyotaka kuifanya, bila shaka huyo alikuwa ni Katibu Mhutasi wangu na kijana aitwaye Sebastian Mkude ambaye ana kampuni ya kuchapisha mabango.
“Lakini Mungu anajua kwa nini jambo hili limetokea, pengine ningepewa kipigo mpaka kufa, acha nitafute njia nyingine ya kuwasiliana na rais pamoja na Aga-Khan bila kushikilia bango mkononi!” Niliwaza.
Uamuzi huu ndiyo ulifanya wiki iliyopita nianze kuandika kuwasilisha ujumbe wangu juu ya Hospitali ya Aga-Khan kwa serikali na pia viongozi wa juu wa taasisi, waliosoma wiki iliyopita niliandika: “Hospitali ya Aga-Khan lazima ibadilike, vinginevyo itaendelea kuchafua sura ya kiongozi wao wa dini!”
Sina tatizo lolote na Mtukufu Aga-Khan, mtu huyu amefanya mambo mengi sana kwa ulimwengu huu, hasa Afrika, ameokoa maisha ya watu wengi! Lakini hakuna kizuri kisicho na kasoro, wala sina chuki binafsi na Hospitali ya Aga-Khan, Dar es Salaam, imekwishasaidia familia yangu mno, hasa mama yangu, ninachokifanya hapa ni kutaka hospitali hii ibadilike na kuwa bora.
Mimi kuwa na uwezo wa kumudu kulipia matibabu ya Hospitali ya Aga-Khan, haitoshi, kuna Watanzania wengi wasio na uwezo huo, lakini wanahitaji kuishi, hatuwezi kukubali wawekwe pembeni, binadamu wote ni sawa, maisha yangu mimi hayawezi kuwa bora kama ya mwingine hayajawa! Hii ndiyo sababu ninapiga kelele, nikitaka Hospitali ya Aga-Khan ipokee wagonjwa wa bima ya afya, sitanyamaza mpaka jambo hili litokee.
Jioni ya siku aliyowasili Mtukufu Aga-Khan, nikiangalia taarifa ya habari nyumbani, nilimshuhudia Rais John Pombe Magufuli, rais wa wanyonge, akiongea bila kupindisha kilekile kilichokuwa kichwani mwangu kwamba, Hospitali ya Aga-Khan ilikuwa hailipi kodi na bado gharama zake za matibabu zilikuwa juu kupindukia, moyo wangu ulijawa na furaha baada ya rais kutamka maneno hayo.
Matumaini yangu ni kwamba kauli ya rais haitachukuliwa kwa wepesi na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu pamoja na Naibu Waziri, Faustine Ndugulile, rais amekwishatamka, wanachotakiwa kufanya sasa ni kuifuatilia hospitali hii ili kuhakikisha gharama zake zinakuwa nafuu na wananchi wote wanatibiwa hapo, kutotekeleza jambo hili ni kumpuuza kiongozi wa juu jambo ambalo hakika si jema.
Kama rais ameweza kuwabana Acacia ambao kwa miaka mingi walipigiwa kelele wakidaiwa kuliibia taifa letu, inashindikanaje kuibana hospitali kama Aga-Khan ili itende haki? Au inaogopwa kwa sababu Mtukufu Aga-Khan alikuwa rafiki wa Mwalimu Nyerere? Au kwa sababu anamiliki vyombo vya habari hivyo anaweza kuipeleka nchi huku au kule apendavyo?
Ndugu zangu, kila zama na wafalme wake, utawala uliopo ni lazima uhakikishe kila kitu kinakwenda sawa na kwa Aga- Khan ni kuhakikisha tu matibabu yake yanakuwa na gharama za kawaida na pia apokee wagonjwa wa bima ya afya, nalisema hili kwa faida ya Watanzania walio wengi, wasio na uwezo wa kumudu gharama za hospitali kama hiyo.
Tuachane na hofu, tutende haki, tutetee wanyonge kama jinsi rais wetu anavyofanya, wapo wazalendo wengi wanaoweza kusimama na nchi yao kama ilisimama nao wakati wa dhiki, Waziri Ummy Mwalimu, Naibu wake, Faustine Ndugulile, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Mpoki Ulisubisya, hamshindwi kulisimamia jambo hili, msaidieni Rais, msipofanya hivyo, kwa Jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, msishangae siku moja mtakaponiona na bango langu kwenye lango kuu la kuingia wizarani kwenu.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu mbariki Rais wetu John Pombe Magufuli,
Mungu tubariki Watanzania wote. Ahsanteni kwa kunisoma.
Itaendelea wiki ijayo.