The House of Favourite Newspapers

Wahitimu Victory Secondary Waaswa Kulinda Maadili Wakifanya Mahafali

0
Wahitimu wakionesha kipaji kwenye kucheza.

Shule ya Sekondari Victory iliyopo Mwandege mkoa wa Pwani imefanya mahafali ya kumi na tatu ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne ikiwa na jumla ya wanafunzi 113 ambao kati yao 54 ni wavulana na 59 ni wasichana wanaotarajia kuhitimu mwaka huu.

Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ponsiano Mlelwa amesema kuwa amewashukuru wote kwa kuhudhuria mahafali hayo na ameahidi shule hiyo kufanya vizuri zaidi ili kuboresha huduma ya elimu shuleni hapo.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha siku hii muhimu na pia nichukue fulsa hii kumshukuru Mkurugenzi wetu, Dkt Thadeo Mutembei ambaye ndiye mmiliki wa shule hizi ikiwemo Victory, St. Matthew’s, Ujenzi, St. Mark’s na Image Vosa kwa kuwekeza kwenye sekta ya elimu ambayo ndio msingi wa maendeleo ya nchi yetu.

“Shule yetu imekuwa ikipiga hatua mwaka hadi mwaka kitaaluma ikiwa na viwango vya juu vya ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne, miaka mitatu mfululizo ambapo mwaka 2017 wanafunzi 179 walifanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne ambapo wanafunzi 178 walifaulu. Ufaulu huo ni sawa na asilimia 99.4, mwaka 2018 walifanya mtihani wanafunzi 155 na waliofaulu ni 154 sawa na asilimia 99.4 na mwaka 2019 walifanya mtihani wanafunzi 152 na wakafaulu wote sawa na asilimia 100.

“Uongozi na usimamizi wa mkurugenzi wetu shule yetu umeweza kujenga miundombinu mbalimbali ambayo imekuwa kichecheo cha taaluma hapa shuleni kwetu.

Mwalimu Mkuu Ponsiano Mlelwa akisoma risala kwa wahitimu.

Mfano shule ina majengo ya kujitosheleza na pia kuna maabara tatu za kisasa za masomo ya Biolojia, Kemia, Fizikia na kompyuta na zote zina vifaa vya kutosha kwa ajili ya kujifunzia”.

Mwalimu Mlelwa ameendelea kuwaasa wanafunzi hao kutambua kwamba elimu waliyoipata ni ndogo na ndio mwanzo wa safari.

“Mnatakiwa muwe na mtazamo wa kujiendeleza zaidi kwani elimu haina mwisho epukeni matumizi ya dawa za kulevya ambayo yanaharibu na kupoteza nguvu kazi ya taifa letu. Pamoja na dawa hizo pia jiepusheni na vitendo vya ngono zembe ambavyo vinaweza kuwasababishia maradhi ya Ukimwi ambao upo na unaua sana hivyo basi mjiepushe.

“Dunia hii imejaa anasa vilevile mwisho niwasisitize kulinda nafsi zenu dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ambayo inaweza kuwaharibia mambo yenu”. Alimaliza kusema Mwalimu Mlelwa.

Leave A Reply