The House of Favourite Newspapers

Wakazi wa Razaba Bagamoyo Waomba Kurasimishiwa Maeneo Wanayoishi

0
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo akiongea kwa uchungu kufuatia hofu ya kuondolewa kwenye makazi hayo.

 

 

 

Wakazi wa eneo la Razaba Kata ya Makurunge, Bagamoyo mkoani Pwani wameiomba serikali iwarasimishie eneo lao wanaloishi kwa muda mrefu sasa baada ya kuingiwa na hofu ya kupewa mwekezaji.

Sehemu ya wakazi wakifuatilia kiumakini yanayozungumzwa kwenye mkutano huo.

 

 

 

Wakazi hao wanaoishi kwa shughuli za kilimo wameiomba serikali kuwarasimishia eneo ambalo nusu yake tayari ameshapewa mwekezaji.

Diwani wa Kata ya Makurunge, Hamisi Mohammed maarufu Mbonde alipokuwa akizungumza na wakazi hao.

 

 

 

Kufuatia hofu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakazi hao walifanya kikao na diwani wa kata hiyo Hamisi Mohammed maarufu Mbonde ambaye aliwaahidi wakazi hao kuzidi kulipigania eneo hilo ili waweze kurasimishiwa.

 

 

Katika kikao hicho wakazi hao walimbana diwani huyo ili awaeleze kinachoendelea ili waondokane na hofu ya kuvunjiwa nyumba zao kuondolewa kimabavu kwenye mashamba wanayoendeshea maisha yao na kugeuka kama wakimbizi.

 

 

 

“Wewe ndiye diwani wetu unayetuwakilisha sisi kama wananchi wako sasa leo tunataka utueleze hatima yetu maana mpaka muda huu tunajiona kama wakimbizi kwenye nchi yetu”, alisema mmoja wa wananchi kwenye mkutano huo. Miongoni mwa mambo yaliyoonesha kuwasikitisha wakazi hao ni baada ya baadhi ya viongozi wa ngazi za chini kumuambia Waziri Wa Ardhi na Makazi, William Rukuvi kuwa eneo hilo halina wakazi na wanaoishi ni wavamizi.

 

 

 

Ukweli usiofichika ni kwamba miaka mingi iliyopita kabla ya kuingia wakazi hao eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya ranchi ya mifugo ya Zanzibar (Razaba). Wakazi hao wameomba kupaza sauti zao kwa kusisitiza kuwa eneo lina wakazi wanaotambulika na kuna huduma za kiserikali zinazoendelea ikiwemo vituo vya kupiga kura nyakati za uchaguzi na wameshawachagua viongozi mbalimbali wakiwa eneo hilo.

 

 

 

“Kama sisi huku hatutambuliki mbona huwa tunaletewa masanduku ya kupiga kura ya kuwachagua viongozi wetu na kuwekewa vituo hukuhuku, chondechonde tunaiomba serikali itutambue na kuturasimishia hili eneo ambalo wengine mpaka babu na bibi zetu tumewazika eneo hilo,” aliomba mwananchi mmoja aliyekuwa kwenye mkutano huo”.

 

 

 

Akihitimisha kikao hicho diwani Mbonde aliwaomba wakazi hao kuendelea kuwa watulivu na kuwaahidi kulifuatilia kiumakini suala hilo na kuwaambia huenda angeshalimaliza lakini hii ndiyo awamu yake ya kwanza tangu achaguliwe hivyo hakuanza nalo muda mrefu. HABARI/ PICHA : RICHARD BUKOS NA ISSA MNALLY /GPL

Leave A Reply