The House of Favourite Newspapers

Walikuwa maskini kama wewe, sasa ni matajiri wa kutupwa

0

Oprah-Winfrey3OPRAH WINFREY.

Hakuna anayezaliwa na fedha, binadamu wote wamekuja duniani wakiwa mikono mitupu kabisa, tena bila nguo. Watu wanapokua, wengi wanakuwa hawana vitu hivyo na hata kula yao wakati mwingine ni ya shida mno.

Wanapofanikiwa, huwa hawakai kimya, wanatamani na wengine wafanikiwe ndiyo maana wengine wamekuwa wazi na kusema: “Kuzaliwa maskini si kosa lako, ila kufa maskini, hilo ni kosa lako.”

Hawa hapa chini ni matajiri wakubwa kwa sasa, ila kabla ya hapo, walikuwa maskini kama wewe na inawezekana wao walikuwa maskini zaidi yako, ila walijifunza mengi, wakatamani kupata fedha, wakapambana maishani, hawakukata tamaa na mwisho wa siku, wakafanikiwa na kuwa matajiri wakubwa.

KENNY TROUTT (UTAJIRI SH. TRILIONI 2):
Huyu jamaa ni tajiri wa Marekani mwenye utajiri wa zaidi ya Sh. trilioni 2, hakuzaliwa kwenye familia ya kitajiri, wazazi wake walikuwa maskini, mama yake alifariki dunia hivyo aliishi na baba yake ambaye alikuwa mhudumu wa baa. Maisha hayakuwa mepesi hata kidogo ila fedha alizozipata baba yake ndizo zilizomsomesha Troutt.

from-dirt-poor-to-a-7-billion-fortune--the-incredible-rags-to-riches-story-of-ralph-laurenRALPH LAUREN.

Alipotakiwa kwenda kusoma katika Chuo cha Southern Illinois Marekani, hakuwa na hela, hivyo alichokifanya ni kuuza bima yake ya afya ili apate hela, kweli akapata na kuanza chuo. Kwa kuwa akili yake ilikuwa inachaji vizuri, mwaka 1988 akaanzisha kampuni ya simu iitwayo Excell Communication ambapo mwaka 1996 ilijulikana zaidi.
Miaka miwili baadaye, akaiuza kampuni yake kwenye Kampuni ya Telegrobe kwa dola bilioni tatu.

Leo unapomzungumzia Troutt, unamzungumzia bilionea mkubwa anayemiliki Timu ya Kikapu ya Titan, anayemiliki shamba kubwa la farasi huko Marekani.

HOWARD SCHULTZ (UTAJIRI SH. TRILIONI 4):
Hebu jiangalie, wewe ni maskini? Huna hata hela ya kula milo mitatu kwa siku? Usikate tamaa, unaweza kufanikiwa. Schultz ni tajiri wa Kimarekani mwenye utajiri wa zaidi ya Sh. trilioni 4 ambaye alikuwa maskini wa kutupwa, hakuwa na fedha, alikulia katika familia ya kimaskini mno lakini kupambana kwake kumemfanya awe tajiri.

Kwa maisha ya kuungaunga, akajikuta akianza masomo yake katika Chuo cha Northern Michigan nchini Marekani, alipomaliza akaenda kufanya kazi katika kampuni ya kutengeneza mashine za fotokopi za Xerox. Baadaye akaamua kuachana nayo, akaanzisha duka dogo la kuuza kahawa aliloliita Starbucks. Utajiri ukaanzia hapo, kupitia duka moja, akapata maduka 60. Baadaye, akapata sehemu zaidi ya elfu kumi na sita za kusambazia kahawa yake.

OPRAH WINFREY (UTAJIRI SH.TRILIONI 5):
Ni mwanamke tajiri wa Marekani aliyepitia maisha ya shida huko Mississippi nchini Marekani, hakubahatika kuzaliwa kwenye familia ya kitajiri. Katika kipindi cha maisha yake, kuna siku aliwaambia watu kwamba angekuwa na fedha sana baadaye, wengi walimpuuzia lakini baada ya kufanikiwa kumaliza masomo katika Chuo cha Tennesse, akafanikiwa kuwa mwandishi wa kwanza wa televisheni Mmarekani mwenye asili ya Afrika akiwa na miaka 19 tu.

Mwaka 1903 akaelekea jijini Chicago kwenda kufanya kipindi cha mdahalo kwenye televisheni moja, kipindi hicho alikiita AM Talk Show ambacho baadaye kikabadilishwa na kuwa The Oprah Winfrey Show ambacho kila siku kilimuingizia fedha na umaarufu hadi akafikisha utajiri wa zaidi ya Sh. trilioni 5.

JOHN PAUL DEJORIA (UTAJIRI SH. TRILIONI 8):
Miongoni mwa watu waliokulia katika umaskini ni huyu jamaa. Mara baada ya kufikisha umri wa miaka kumi, alianza harakati za kuuza kadi za Krismasi na magazeti kwa ajili ya kuisaidia familia yake iliyokuwa maskini wa kutupwa.

Baada ya kutoka jeshini, akaamua kufanya kazi kivyakevyake kutafuta fedha kwani wakati huo familia yake ilikuwa mbaya kiuchumi hivyo akaamua kukopa benki kiasi cha dola mia 7 (zaidi ya shilingi milioni 1.4).

Jamaa huyo alianzisha biashara ya kuuza ‘shampoo’ tena huku akiishi katika gari lake chakavu. Baadaye alianzisha wiski iitwayo Patron Tequila ambayo mpaka leo inamuingizia kiasi kikubwa cha fedha na kumfanya kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa.

RALPH LAUREN (UTAJIRI SH. TRILIONI 14):
Watu wengi tunapuuzia sana kufanya biashara ndogondogo kwa kuamini kuwa hatuwezi kupata mafanikio. Ila kwa Ralph ambaye ni tajiri wa Marekani, alianza kiutaniutani tu, maskini wa kutupwa asiyekuwa na chochote lakini leo ni bonge la tajiri akiwa na utajiri wa zaidi ya Sh. trilioni 14.

Alisoma elimu ya sekondari huko Bronx, New York nchini Marekani ila baadaye akaamua kuachana na shule akaenda zake jeshini. Baadaye alikuwa karani katika Kampuni ya Brooks Brothers ambapo alijiuliza kama angeweza kuwafanya wanaume kupendeza kwa kuvaa tai zenye kung’aa, alipopata jibu kwa kuona inawezekana, akaamua kutengeneza tai hizo.

Aliamini katika ndoto hiyo na hatimaye mwaka 1967, aliikamilisha ndoto yake kwa kuuza tai zilizokuwa na thamani ya dola 500,000 (zaidi ya Sh. bilioni 1). Mwaka uliofuata, akaanzisha kampuni yake ya mavazi iliyoitwa Polo inayomuingizia utajiri mkubwa.

Leave A Reply