The House of Favourite Newspapers

Wamekosea Timing…

UZIKI wa Bongo Fleva wa sasa umekuwa ni ajira na biashara kubwa tofauti na kipindi cha nyuma ambapo ulikuwa ukichukuliwa kama muziki wa kihuni usio na faida.

Kwa sasa zipo njia nyingi za kuingiza kipato ambazo wasanii wengi huzitumia pindi wakitoa nyimbo zao, mojawapo ni kupata mapato kupitia miito ya simu za mkononi, kuuza ‘online’ na shoo za kutosha.

Kwa mantiki hiyo, wasanii wengi huangalia muda wa kuingiza nyimbo zao sokoni ili kusikilizwa kwa wingi na hatimaye kuambulia chochote kati ya hivyo nilivyovitaja. Wengi wa wasanii hao hasa mastaa hupendelea kutoa nyimbo kwa kuachiana ‘gepu’ na kuangalia kama kuna kitu kikubwa kipo kinachoteka hisia za mashabiki wao wengi.

Mfano umeonekana miaka ya hivi karibuni ambapo kama utakumbuka Januari 27, mwaka jana, Kundi la Navy Kenzo liliibuka na Wimbo wa Kamatia Chini na hakukua na nyimbo yenye kukubalika sana wala tukio lililoteka hisia za watu wengi katika miezi hiyo hivyo kuwafanya kuwa juu na kupata dili nyingi. Pia Mei 19, mwaka huohuo mkali mwingine, Ali Kiba aliachia Wimbo wa Aje na katika kipindi hicho nacho hakukuwa na tukio la aina yoyote la kuwateka watu kufuatilia hivyo kusikika na kula mashavu ya kutosha.

Mfano mwingine ni Julai 12, mwaka jana, Diamond Platnumz alipoachia Wimbo wa Kidogo akiwa na Kundi la P-Square kutoka Nigeria, wimbo ambao nao ulifuatiliwa na mashabiki wengi na kufikia hatua ya kuangaliwa YouTube na watu zaidi ya milioni moja kwa siku nne tu. Mifano mingine ni Septemba 18, mwaka jana ambapo napo Diamond aliachia Wimbo wa Salome akishirikiana na mwanamuziki kutoka lebo yake ya WCB, Rayvanny.

Licha ya wimbo huo orijino yake kuimbwa na mwanamuziki wa nyimbo za asili, Saida Kalori kulimfanya kuliteka soko. Aliyefunga mwaka alikuwa Darassa na Wimbo wa Muziki uliotoka Novemba 23, mwaka huohuo.

Ukiangalia katika mifano hai niliyotoa hapo juu, wasanii wote waliweza kupenya kirahisi kwanza kwa kuachiana gepu la miezi kadhaa katika kutoa nyimbo zao, pia walisoma alama za nyakati kwa kuzichimbia na kuangalia muda muafaka wa kuzitoa bila kuwepo kwa tukio la kuteka hisia za watu wengi.

Tangu mwaka uanze yapo matukio ambayo yameteka hisia za wengi kiasi cha mashabiki wa muziki kuhamishia akili zao huko huku baadhi wakifuatilia muziki. Matukio hayo moja wapo ni lile la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutaja wasanii wanaotuhumiwa kujihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya, tukio la Wema kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenda Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na lingine ni lile linalomhusisha mkuu huyo wa mkoa kudaiwa kutumia vyeti ambavyo si vyake.

Pia tukio jingine limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita la mkuu huyo wa mkoa kuvamia Ofisi za Clouds Media akiwa na watu wenye silaha jambo ambalo licha ya kupingwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vingi vya habari nchini pia limekuwa gumzo kila kona.

Licha ya kuwepo kwa matukio hayo ndani ya miezi hii miwili (Februari na Machi), wapo mastaa ambao wameachia nyimbo zao lakini zimeonekana kutowashika mashabiki wengi wa muziki kutokana na kukosa timing ya kuziachia na katika makala haya yanawaanika baadhi ya mastaa hao;

BARAKAH THE PRINCE – ACHA NIENDE Mwaka jana alijiunga rasmi katika Lebo ya Rockstar4000 na kuwa pamoja na wakali wengine kama Lady Jaydee pamoja na Ali Kiba.

Tangu ameingia katika lebo hiyo ameshaachia nyimbo mbili ambapo ya kwanza ni Nisamehe aliyoitoa Septemba 13, mwaka jana na Acha Niende alioitoa mwezi huu. Acha Niende ni wimbo mzuri ila nao umeingia katika listi ya nyimbo zilizokosea timing ya kuachiwa.

JAY MOE – NISAIDIE KUSHARE

Alipotea kwenye gemu kwa kipindi kirefu lakini Juni mwaka jana akaibuka na Pesa ya Madafu. Mwezi huu ameibuka tena na Wimbo wa Nisaidie Kushare, ni wimbo mzuri na kama utaangalia hata video yake aliyofanyia Sauz utakubaliana nami kuwa imekosewa timing ya kuachiwa.

CHEGGE NA TEMBA – GO DOWN

Tangu waachie wimbo wao wa Kaunyaka mwaka 2015 wakishirikiana na staa kutoka Sauz, Uhuru hawajakutana tena kufanya kolabo ya pamoja zaidi ya kila mmoja kufanya kazi zake.

Mwezi huu wamerudi tena wakiwa pamoja katika Wimbo wa Go Down ni wimbo mzuri lakini nao umekosa timing ya kuachiwa.

HARMONIZE – NIAMBIE

Mwaka jana alifanikiwa kuwika kutokana na kufanya timing ya kuachia ngoma zake, kama utakumbuka Februari 29 aliachia Bado akimshirikisha Diamond Platnumz wimbo ukafanya vizuri zaidi ya sana. Mwaka huohuo tena Julai 4, akaachia wimbo mwingine uitwao Matatizo nao ukafanya poa.

Mwezi huu ameachia zaidi ya nyimbo tatu, Happy Birthday, Niache Nilewe pamoja na Niambie ambapo kideo chake yupo mwandani wake, Jacqueline Wolper. Licha ya kuendelea kufanya promo za kutosha bado inakosa nguvu kutokana kila kona mashabiki wengi kuonesha hisia zao kwenye matukio hayo.

PROFESA JAY – KIBABE

Ni mmoja kati ya waasisi wa Bongo Fleva nchini ambaye pia ni Mbunge wa Mikumi kupitia Chadema. Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu, aliibuka Septemba 15, 2014 akiwa na Wimbo wa Kipi Sijasikia akimshirikisha Diamond ukafanya poa. Kama hiyo haitoshi, Julai 29, mwaka jana akaibuka tena na Wimbo wa Kazi Kazi akimshirikisha Sholo Mwamba.

Wimbo ulipokelewa vizuri kutokana na aina ya muziki alioifanya ya Singeli. Machi mwaka huu ameibuka tena na Wimbo wa Kibabe ambapo kama utausikiliza ameamua kuchana kama alivyokuwa akifanya miaka ya nyuma.

Wimbo ni mzuri ila nao umekosa timing ya kuachiwa. Nyimbo nyingine ni Kwikwi ya Ruby, Vanessa Mdee akiwa na Orezi Wimbo wa Just Like That, G Nako akimshirikisha Jux Wimbo wa Go Low na nyingine nyingi.

Kama nilivyoeleza hapo juu, mastaa hawa wamekosea timing ya kuachia kazi zao kutokana na upepo uliopo lakini kama utaisha mapema ina maana zitaweza kusikika na kuwafikia watu lakini si kama walivyotarajia.

 

Comments are closed.