The House of Favourite Newspapers

Wanasheria Simba Watafuta Kadi ya Fakhi

0
Beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi.

Said Ally | Championi Jumatano | Habari

LICHA ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) chini ya mwenyekiti wake, Hamad Yahaya kulitolea ufafanuzi suala la kadi tatu za beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi kwa kusema hana kadi hizo, uongozi wa timu ya Simba umesema bado wanampango wa kwenda Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ili kudai haki yao.

Hivi karibuni Bodi ya Ligi ilitoa ufafanuzi juu ya kutotambua kadi tatu za Fakhi kama ambavyo alikatiwa rufaa na Simba ambao walidai kuwa beki huyo alicheza mechi dhidi yao akiwa na kadi tatu za njano, kinyume na sheria na kanuni za ligi, lakini uongozi huo umesema wanasheria wake wamekusanyika sasa kutafuta ushahidi.

Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Simba, Said Tully ameliambia Championi Jumatano, kuwa licha ya kusikia maamuzi hayo lakini kwa sasa wanaendelea na suala la kukusanya ushahidi wao kwa ajili ya kuuwasilisha Fifa kwa ajili ya kudai warudishiwe pointi hizo ambazo walinyang’anywa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji.

“Watu wasione kama maamuzi hayo ya Bodi ya Ligi ya kusema Fakhi hana kadi tatu za njano kwamba yamebatilisha uamuzi wetu wa kwenda Fifa bali tuwaambie kwamba uamuzi huo upo palepale na tunachokifanya kwa sasa ni kukusanya baadhi ya data ambazo tutaziwasilisha Fifa.

“Hatutaki haki yetu ipotee kirahisi na tumepanga kukomaa na suala hili mpaka tuone haki imetendeka na niwaambie tu kwamba kwa sasa baadhi ya wanasheria wetu wanaendelea na masuala ya kutafuta ushahidi unaonyesha mchezaji huyo alikuwa na kadi tatu za njano,” alisema Tully.

Leave A Reply