The House of Favourite Newspapers

Wanawake wenye vigezo hawaingii kwenye ndoa

0

NI Jumanne nyingine yenye neema itokayo kwa Mungu wetu, Mungu aliyeumba mbingu na nchi na vyote vilivyomo!
Baada ya kumaliza mada yangu ya wiki iliyopita ya; unataka kuolewa, kuoa au kufunga ndoa ambayo ilivuna wasomaji kibao, walioniponda na kunipongeza, leo nina mada nyingine moto kama kawaida yangu.

Mada ya leo inawahusu wanawake tu! Kwamba utafiti wangu wa kimtazamo umebaini kuwa wanawake wenye sifa nyingi za kuingia kwenye ndoa hawakumbwi na bahati hiyo.

NILICHOZINGATIA
Katika utafiti wangu huu nilizingatia wanawake wenye utulivu, heshima, kuthamini wengine, aibu ya kuchepuka, kusomwa vizuri na watu na uwezo wa kulea familia. Kusomwa vizuri namaanisha watu wengi wanamsifia kwa tabia njema.
Wapo wanawake wana sifa zote hizo nilizozitaja lakini hawapo kwenye ndoa, wengi wao wanaishi majumbani kwa wazazi wao au wamepanga kutokana na kupata uwezo wa kuendesha maisha lakini wanaume wa kuwaingiza kwenye ndoa wanakosekana.

SIKIA USHUHUDA HUU
Hivi karibuni nilibahatika kuzungumza na mrembo mmoja ambaye aliniambia kwamba yeye ameolewa kwa ndoa, huu mwaka wa pili sasa, lakini dada yake yupo nyumbani na hajabahatika hata kuchumbiwa.

“Kinachonisikitisha ni kwamba, mimi kama mimi nakiri kuwa dada yangu ni bora sana kama ataingia kwenye ndoa. Ana vigezo vyote, lakini sijui hata ni kwa nini wanaume wanamkwepa!
“Mimi kusema ule ukweli nimeingia kwenye ndoa kwa vile tu bahati imenidondokea lakini sina sifa. Sina sifa hata wazazi wangu, hasa mama alikuwa akiniambia mimi sina sifa ya kuwa mke hata wa ngedere achilia mbali binadamu.

“Mimi nina mdomo mrefu, napenda kushindana. Jambo dogo kwangu huwa kubwa, naweza kusema hata siku mbili.

“Lakini ngoma nzito ambayo mume wangu anakumbana nayo kwangu ni kunilalamikia kwamba simpi heshima yake. Ni kweli, mimi akinitibua sijali pana mama mkwe sijali pana mjomba’ake, nampelekea tu mambo ambayo sista hana,” anasema Anna Lukanika, mkazi wa Sinza Mugabe, Dar.

LAWAMA KWA WANAUME?
Pia katika utafiti wangu huu nilibaini kwamba, wanaume ndiyo wanabebeshwa lawama kwa sababu walio wengi wanaoa kwa kufuata uzuri wa sura ya mwanamke na maumbile bila kuzingatia tabia.

“Mimi kwanza nakubaliana na wewe mwandishi wa mada zako kwenye Gazeti la Uwazi. Lakini kwa mada hii uliyoniuliza lawama kubwa nawapa wanaume.

“Wanaume wengi siku hizi wakitaka kuoa, kigezo chao cha kwanza ni je, mwanamke ni mzuri wa sura? Kigezo cha pili je, ana umbo la kuvutia? Akikubali kichwani mwake au marafiki zake wakimsifia, anatangaza ndoa.
“Matokeo yake ndani ya ndoa kunakwenda kuwa na kasheshe kwa sababu kumbe tabia siyo kabisa,” anasema mama Mkanda, mkazi wa Mabatini- Mwanza.

MUNGU ALIUMBA HIVI?
Mama Mkanda anaendelea kusema: “Bahati mbaya sana, sijui ni akili zangu au ndivyo ilivyokuwa tangu kuumbwa kwa dunia, wanawake wenye tabia nzuri wana sura mbaya maumbile mabaya, wenye sura nzuri, maumbo mazuri wana tabia mbaya.”

NI DHANA
Mimi kama mwandishi wa mada hii, sikubaliani moja kwa moja na mama Mkanda, naamini ni mtazamo wake tu. Wapo wanawake wana sura nzuri, maumbo mazuri na tabia nzuri lakini pia wapo wenye kinyume cha hapo. Pia wapo mchanganyiko.

WANACHOPENDA WANAUME
Naamini wanaume wengi siku hizi wanapenda wanawake wachakaramu ndiyo waingie nao kwenye ndoa. Mwanamke mtulivu, mkimya sana, asiyependa starehe, heshima mpaka anaboa, wao wanaona hawaendani. Hapa penye sehemu ya wanaume ndipo pa kujiangalia vizuri. Kwaherini.

Leave A Reply