Wanigeria Wairahisishia Kazi Simba kwa Yanga

MABOSI wa Simba wameweka wazi kuwa na imani kubwa kwenye mchezo wao wa leo dhidi ya Yanga wa Ngao ya Jamii kutokana na mbinu ambazo wamezinasa kitaalamu kupitia mchezo wa wapinzani wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United.

 

Taarifa kutoka Simba zimeeleza kuwa benchi la ufundi la Simba halikuacha kuwafuatilia wapinzani wao kwenye mechi zao mbili za kimataifa dhidi ya Rivers United jambo ambalo linawapa nguvu ya kushinda mchezo wao.

 

“Yanga ni timu nzuri hivyo kuifuatilia pia inahitaji mbinu nzuri zitakazosaidia kupata ushindi, mechi zao mbili za kimataifa zinatoa picha kamili kwa sababu huwezi kuficha mbinu ya kusaka ushindi kwenye mechi kubwa, kuzitazama mechi zile kuna maana kubwa kwetu,” ilieleza taarifa hiyo.

 

Alipotafutwa Kaimu Ofisa Habari wa Smba, Ezekiel Kamwaga aliliambia Championi Jumamosi kuwa maandalizi yapo vizuri na kuhusu kuwafuatilia wapinzani wao hilo ni jukumu la benchi la ufundi.

 

“Kuangalia mpinzani wako nini anafanya hilo lipo kwenye benchi la ufundi ila tunajua kwamba Yanga ilikuwa inawakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa. Wachezaji wetu wapo tayari na imani yetu ni kuona kwamba tunafanya vizuri,” alisema Kamwaga.

LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam


Toa comment