The House of Favourite Newspapers

Wanne Mbaroni kwa Kuzusha Vifo vya Corona

0

 

POLISI Mkoa wa Pwani inawashikilia watu wanne waliokamatwa ndani ya mkoa huo wakituhumiwa kutumia mitandao ya kijamii kueneza uvumi wa vifo vya watu wakidai wamekufa kwa corona na kutia hofu wananchi.

 

 

Kamanda wa Polisi Pwani, Wankyo Nyigesa, amesema: “Watuhumiwa hawa wanne tuliowakamata Pwani na wengine ambao tunaendelea kuwatafuta wanasambaza taarifa za uvumi za vifo vya watu wakidai wamekufa kwa corona na pia wanapendekeza majina ya viongozi wa serikali ambao walitamani wafe haraka kwa corona.

 

 

“Na wengine ambao tunawatafuta, licha ya kueneza uvumi wa vifo vya watu wakidai wamekufa kwa corona, pia wanatia hofu mitandaoni kwa kudai watanzania walio wengi watakufa kwa sababu serikali haichukui tahadhari dhidi ya wananchi wake.

 

 

“Zaidi sana watuhumiwa hawa wanaendelea kutaja baadhi ya viongozi wakuu serikalini ambao wao wanatamani wafe kwa corona haraka sana. Wanasema serikali haijachukua tahadhari kwa hiyo Watanzania wengi watakufa kwa corona.” amesema Nyigesa.

 

 

Amewataja waliokamatwa kuwa ni Frank Nyange (47), Moses Goodluck (34), Mohammed Abdallah Lutambi (45) na Bumija Moses (55) ambao ni viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

 

 

Amesema kama mwananchi au familia imefiwa, mwenye jukumu kutangaza kifo ni wanafamilia. Aidha, kama ni kiongozi mamlaka za serikali zitatangaza na si vinginevyo.

 

 

“Polisi mkoani Pwani tunatoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya corona kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya na kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ikiwemo kutoa taarifa za uvumi kuhusu vifo vya watu ambazo zinatia hofu wananchi wengi,” amesema.

Leave A Reply