The House of Favourite Newspapers

Waombolezaji wa Kulipwa Wazua Sekeseke Msibani, Mfiwa Ajifungia Chooni

0

 

TAHARUKI imeibuka katika maeneo la Lugari, Kakamega nchini Kenya baada ya vijana wanaolipwa ili kuomboleza msiba, kuzua sekeseke kwa mwenyeji wao (mfiwa) kuwaandalia ugali kwa kuku badala ya kuwalipa pesa yao.

 

 

Wapambe hao ambao jukumu lao ni kunogesha mazishi kwa densi maalum, nyimbo na shamrashamra za aina yake walidai mwenyeji wao aliwatapeli badala ya kutekeleza wajibu waliokubaliana.

 

 

“Huu ni uhuni! Tunafanyiwa uhuni mchana kweupe na hatung’atuki hapa hadi tupewe haki yetu,” mmoja wao alisikia akidai.

Ni kweli huyu ni tapeli mkubwa. Hajatimiza hata moja tuliloafikiana,” wa pili alieleza.

“Anafikiri kuruka ruka tukicheza na sarakasi zote hizi ni kazi rahisi? Kazi ni kazi jamani,” kijana wa tatu naye aliongea.

 

Taarifa zaidi zinaarifu kwamba siku ya kisanga ndugu na jamaa walijaa msibani, kutokana na maandalizi ya mazishi yalivyokuwa yamenogeshwa. Ulipofika wakati wa kutoa jeneza nje ya nyumba, wombolezaji hao walisakata ngoma kwa bidii huku wengine wakijiangusha kama majani wakiomboleza huku wakitiririkwa na machoni ungedhani ni wao waliofiwa.

 

 

Inasemekana hata wakati jeneza lilipokuwa likiteremshwa kaburini mmoja wao alitishia kujirusha ndani lakini akadhibitiwa na kutulizwa jazba zake na wenzake. Baada ya mazishi kukamilika, waliketi kwenye hema maalum na kula chakula cha yapata watu hamsini lakini baada ya kumaliza na kuanza kudai malipo hapo ndipo maneno yalianza kwenda mrama.

 

 

“Sijawahi kuona watu wenye hamu ya kula kama nyinyi. Mwajua mmekula robo ya chakula kilichopikwa?” mama mwenye aliwaulia mabarobaro.

 

“Usilete upumbavu hapa. Tujuavyo chakula ni cha kila mmoja aliyehudhuria. Tulipe pesa zetu na uwache upumbavu,” walidai.

 

Inasemekana kuwa mwenyeji alipokataa kuwalipa majamaa, kivumbi kikazuka ghafla. Vijana hao walianza kutupa mawe, kurusha viti kila mahali na watu kuumizwa. Mwenyeji alipoona mambo yamekuwa mabaya aliamua kujifungia chooni.

 

 

“Toka! Toka humo ndani wewe tapeli mkubwa. Leo utajua utapeli una mwisho,” mkubwa wa vijana hao aliwaka. Penyenye zinasema mama alipohisi maisha yake yamo hatarini aliamua kubadili msimamo na kutoka mafichoni.

 

 

Mama huyo ambaye alijulikana kuwa mkono wa birika alilazimika kuwalipia vija hao mara dufu ya pesa walizokuwa wameahidiana. Hadi leo mama anasikitika kukadiria hasara aliyosababisha kutokana na tamaa yake.

CHANZO – TUKO NEWS

Leave A Reply