LIGI ya Mabingwa Afrika inatarajiwa kuanza wikiendi hii, ni michuano ya 25 tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ligi hiyo unaotumika kwa sasa.
Simba ni timu pekee kutoka Tanzania Bara inayoshiriki katika michuano hiyo, huku Zanzibar ikiwakilishwa na Mlandege katika michuano hiyo.
Simba ambao waliondoka nchini Jumanne hii, wanatarajiwa kukipiga dhidi ya Plateau United FC ya Nigeria katika Hatua ya Awali.
Wapinzani hao wa Simba ni timu ya muda mrefu lakini katika michuano na ligi ngazi ya juu haina rekodi kubwa kama ilivyo kwa wababe hao wa Msimbazi.
Plateau United FC Kuanzishwa: 1975 Uwanja: New Jos Idadi ya siti: 40,000 Makazi: Jos, Nigeria Mwenyekiti: Pius Henwan Meneja: Abdu Maikaba Jezi ya nyumbani: Njano Jezi ya ugenini: Kijani Jezi ya tatu: Nyeupe
Jina kamili la timu hii ni Plateau United Football Club lakini kwa ufupi inajulikana kwa jina la Plateau United. Kabla ya mwaka 1991 ilikuwa ikijulikana kwa jina la JIB Strikers FC.
Taji lao la kwanza kubwa walilipata mwaka 1999, hiyo ni baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Iwuanyanwu Nationale katika Nigerian Cup.
Mara yao ya kwanza kushiriki katika michuano ya Afrika ilikuwa mwaka 2000, lakini waliondolewa mapema tu katika hatua ya awali.
Baada ya hapo walipotea na kurejea katika Nigeria Premier League kwa mara ya kwanza msimu wa mwaka 2010/11, bahati mbaya walishuka daraja mwaka mmoja baada ya kupanda.
Mwaka 2015 walirejea katika ligi kuu hiyo baada ya kufanikiwa kupata pointi siku ya mwisho ya msimu husika.
Skendo nzito
Mwaka 2013, timu yao ya pili yaani ambayo mara nyingi inatumika kukuza wachezaji ambao baadaye wanapelekwa kikosi cha kwanza ikiwa watafanya vizuri, iliingia katika skendo nzito ya upangaji matokeo nchini Nigeria.
Timu hiyo iliyojulikana kwa jina la Plateau United Feeders ilishinda kwa mabao 79-0 dhidi ya Akurba FC, siku ya mwisho ya msimu ambapo walitakiwa kupanda daraja, huku matokeo ya upande wa pili ambayo nayo yalihusisha wapinzani wao waliokuwa wakiwania nao kupanda daraja wakipata matokeo ya ajabu.
Ilikuwa Julai 22, 2013, ambapo upande wa pili mchezo uliokuwa ukichezwa pamoja na huo wa Plateau, timu ya Police Machine FC ilishinda mabao 67 dhidi ya Bubayaro FC.
Kabla ya michezo hiyo miwili, Plateau United Feeders na Police Machine ziliingia uwanjani zikiwa zinalingana pointi, ushindi na wastani mzuri wa mabao ungeipa timu moja nafasi ya kupanda daraja.
Hadi kipindi cha kwanza Plateau ilikuwa ikiongoza 7-0, kipindi cha pili ikaongeza mabao 72 huku Police Machine wao walikuwa wakiongoza 6-0 hadi mapumziko, kipindi cha pili wakafunga mabao 61.
Kwa matokeo hayo, Plateau wakawa na nafasi ya kupanda kwa kuwa walikuwa na wastani mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Police Machine.
Kwa matokeo hayo, timu hizo zote zilizohusika katika upangaji matokeo ambazo ni Plateau Feeders, Akurba FC, Police Machine FC na Bubayaro FC zote zilifungiwa kwa muda wa miaka 10 huku wachezaji na maofisa walioshiriki na kuhusika katika kupanga matokeo nao wakifungiwa maisha kutojihusisha na mchezo wa soka.
Ubingwa mmoja tu
Plateau United ilifanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Nigeria kwa mara ya kwanza na pekee mwaka 2017, ikiwa chini ya Kocha Kennedy Boboye.
Walivyopata uwakilishi Caf
Inaweza kukushangaza kuona wamebeba ubingwa mara moja tu mwaka 2017 lakini msimu huu wanaiwakilisha Nigeria katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ipo hivi, wakati msimu uliopita wa 2019/20 ukiendelea, ndipo kulipoibuka janga la maambukizi ya Virusi vya Corona, ligi nyingi zilisimama ikiwemo ya nchi hiyo.
Mamlaka husika wakashindwa kuirejesha ligi hiyo na kuamua kuipa ubingwa timu iliyokuwa kileleni ambayo ni Plateau United. Hivyo, siyo mabingwa kama ilivyo kwa Simba ambao walibeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania.
Ilifukuza wachezaji 9 kwa mkupuo
Mbali na skendo hiyo, pia Plateau United FC hii yenyewe sasa ya wakubwa iliwahi kufukuza wachezaji tisa kwa wakati mmoja katika kile walichosema ni kuiokoa timu hiyo isishuke daraja katika Ligi Kuu ya Nigeria mwaka 2011.
Kulikuwa na sababu mbalimbali za kuwafukuza wachezaji hao ikiwemo utoro, nidhamu, kiwango duni na kutowajibika katika majukumu.
Wachezaji waliowahi kuichezea timu hiyo na kufanikiwa:
John Obi Mikel
Umri: 33
Nafasi: Kiungo mkabaji
Timu vijana:
2002-2004 Plateau United
Timu za wakubwa
2004-2006 Lyn
2006-2017 Chelsea
2017-2018 Tianjin TEDA
2019 Middlesbrough
2019-2020 Trabzonspor
2020-sasa Stoke City
Nigeria
2005-2019
Mechi 91
Mabao 6
Chris Obodo
Umri: Miaka 36
Nafasi: Kiungo mkabaji
Timu ya vijana:
Plateau United
Tumu za wakubwa
2001-2004 Perugia
2004-2005 Fiorentina
2005-2012 Udinese
2010-2011 → Torino (mkopo)
2011-2012 → Lecce (mkopo)
2013 Dinamo Minsk
2014 Olhanense
2014–2016 Skoda Xanthi
2016 Concordia Chiajna
2016 Pandurii Târgu Jiu
2017 Apollon Smyrnis
Nigeria
2004-2008
Mechi 21
Mabao 4
Celestine Babayaro
Umri: Miaka 42
Nafasi: Beki wa kushoto
Timu ya vijana
1994 Plateau United
Timu za wakubwa
1994-1997 Anderlecht
1997-2005 Chelsea
2005-2008 Newcastle United
2008 LA Galaxy
Nigeria
1995-2004
Mechi 27
Mabao 0
Victor Obinna
Umri: Miaka 33
Nafasi: Straika
Timu za vijana
2003 Plateau United
2004 Kwara United
2005 Enyimba
2005 Internacional
Timu za wakubwa
2005-2008 Chievo
2008-2011 Internazionale
2009-2010 → Málaga (mkopo)
2010-2011 → West Ham United (mkopo)
2011-2015 Lokomotiv Moscow
2014 → Chievo (mkopo)
2015-2016 MSV Duisburg
2016-2017 Darmstadt 98
2017-2018 Cape Town City
Nigeria
2005-2014
Mechi 48
Mabao 12
Shehu Abdullahi
Umri: Miaka 27
Nafasi: Kiungo
Timu ya vijana
2011 Plateau United
Timu za wakubwa
2012–2014 Kano Pillars
2014–2015 Qadsia
2015–2016 União da Madeira
2016–2018 Anorthosis
2018–2020 Bursaspor
2020– Omonia
Nigeria
2014-sasa
Mechi 31
Mabao 0
John Joseph na mtandao