The House of Favourite Newspapers

Wasanii Chipukizi Wapewa Jukwaa Kutifuana, Mbabe Kutoboa

0
Baadhi ya wasanii chipukizi ambao video zao zimeingia 10 bora ya Shindano la ‘Toboa Kimuziki na Global TV Online’.

 

KAMPUNI ya Global Publishers, imezindua rasmi Shindano la Toboa Kimuziki na Global TV Online, ambalo litashindanisha video 10 za wasanii chipukizi wa muziki wa Bongo Fleva.

 

Shindano hilo limezinduliwa leo Alhamisi katika ofisi za Global Publishers, zilizopo Sinza-Mori jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho, waratibu wa shindano hilo, Kelvin Nyorobi, Kissa Daniel na YouTube moderator wa Global TV Online, Isri Mohamed.

 

Watangazaji wa kipindi cha Bongo 255 cha +255 Global Radio, Rashid Mbegani (kushoto) na Stewart George wakifuatilia uzinduzi huo.

 

Pia, walikuwepo waandishi wa Championi, Spoti Xtra, Magazeti Pendwa, watangazaji wa Global TV Online na +255 Global Radio na wasanii 10, ambao video za nyimbo zao zimepata nafasi ya kuingia kwenye 10 bora.

 

Toboa Kimuziki na Global Tv Online, ni Shindano ambalo litawahusu wasanii Chipukizi wa Bongo Fleva, ambao hawajawahi kupata nafasi kubwa ya nyimbo zao kuchezwa katika vyombo vya habari, hivyo Global TV imewapa fursa hiyo kwa kuweka kazi zao bure katika TV yao ya mtandaoni ili ziwafikie watazamaji na mashabiki wa wasanii hao, jambo ambalo litakuwa ni moja ya njia za mafanikio yao katika kazi zao hizo za muziki.

 

Baadhi ya wasanii chipukizi ambao video zao zimeingia 10 bora ya Shindano la ‘Toboa Kimuziki na Global TV Online’ wakifuatilia uzinduzi huo.

Wasani saba kati ya 10 waliopita walikuwepo katika uzinduzi huo, huku wengie watatu wakishindwa kuja kwa sababu mbalimbali.  Waliokuwepo ni Mwinyi Mohamed, (Mpoz), Sharafi Mhagama (Goweshan), David Deo (Refyd), Jumanne Shija (Juleiza), Jackson Lihiye, (Iva), Mavoice Killer na mwanadada pekee katika shindano hilo, Faidha Tagalile (Fetilicious).

 

Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi huo.

 

Akizungumzia uzinduzi huo, Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho amesema dhumuni la Global TV Online kuanzisha shindano hilo ni kutoa nafasi kwa wasanii chipukizi, ambao wameshafanya audio na video lakini hawana platform ya kuwawezesha kutangaza kazi zao na kuwafikia mashabiki wao na hawapewi nafasi ya kazi zao kupigwa kwenye vyombo vya habari, hivyo kupitia Global TV, yenye zaidi ya subscribers milioni 2.2, video zao zitaweza kuwafikia mamilioni ya watazamaji ndani na nje ya Tanzania.

 

Baadhi ya wasanii chipukizi (wenye fulana nyeusi) ambao video zao zimeingia 10 bora ya Shindano la ‘Toboa Kimuziki na Global TV Online’ wakiwa kwenye picha  na waratibu wa shindano hilo.

“Mshindi wa shindano hili atapata fursa ya kutangazwa na vyombo vyote vya habari vilivyopo chini ya Global Group, kuanzia TV, magazeti yote ya Global Publishers, Redio na mitandao yote ya kijamii ya Global Publishers, lakini mbali na hilo tutampa nafasi ya kuweza kutumbuiza katika jukwaa kubwa la Dar Live katika matamasha mbalimbali ambayo yatafanyika pale ili apate uzoefu wa shoo na kumkutanisha na wadau mbalimbali wa muziki ambao watamsaidia kutimiza ndoto zake.

Baadhi ya wasanii chipukizi ambao video zao zimeingia 10 bora ya Shindano la ‘Toboa Kimuziki na Global TV Online’ wakiwa kwenye picha ya pamoja na waratibu wa shindano hilo.

“Lengo letu si kufanya biashara bali ni kuwasaidia vijana wa Tanzania wenye vipaji na hawana mtu wa kuwashika mkono kufikia malengo yao, sisi hatuhitaji kitu chochote kutoka kwa msanii tunayemsaidia, akifanikiwa kimuziki atawasaidia wengine na wengine, na hii itasaidia hata kupunguza tatizo la ajira. Furaha yetu ni kuona vijana wanafanikia.

Baadhi ya wasanii chipukizi ambao video zao zimeingia 10 bora ya Shindano la ‘Toboa Kimuziki na Global TV Online’ wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya uzinduzi huo.

“Global Publishers, kazi hii tumeianza zamani, hatuwezi kutaja kila msanii tuliyemsaidia, kikubwa tunampa daraja avuke aende kule juu, ili na yeye aweze kuwasaidia wenzake.

 

“Kwa hiyo hakuna unyonyaji wowote kwa msanii, tumeshakaa nao tumekubaliana kisheria, hakimiliki ya wimbo utabaki kuwa ni wa msanii husika na anaweza kuupeleka media yoyote ukapigwa,” alisema Mrisho.

 

Mratibu wa Shindano hilo, Kelvin Nyorobi akizungumza na wanahabari.

 

Kwa upande wa mratibu wa shindano hilo, Kelvin Nyorobi, yeye alieleza namna mchakato ulivyofanyika hadi kupata video 10 bora na kuziingiza kwenye shindano.

 

“Tulipokea nyimbo zaidi ya 70, tulikaa kama kamati, tukaanza kupitia wimbo mmoja hadi nyingine, huku tukizingatia vigezo vyetu kama, ubora wa mashairi, picha, video, maadili, melody, ubora wa biti pamoja na kipaji cha msanii, mwisho tukafanikiwa kuzipata hizi 10 ambazo leo zinawania ushindi huo, lakini haikuwa jambo rahisi.

Moderator wa matukio YouTube, Isri Mohammed, akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi huo

Naye moderator wa matukio YouTube, Isri Mohamed, alieleza namna ambavyo mshindi atapatikana na lini video hizo zitakuwa hewani:

“Kwanza kabisa nyimbo zote zitawekwa kwenye chaneli leo saa sita usiku, (usiku wa kuamkia kesho). Tumetengeneza Play List ndani ya YouTube channel ya Global TV Online inayoitwa (Toboa Kimuziki na Global TV Online), hapo kutakuwa na nyimbo zote zilizoingia 10 bora, video itakayotazamwa mara nyingi zaidi, ndiyo ambayo itaibuka na ushindi.

 

“Hivyo wasanii wenyewe, watazamaji na mashabiki wao wanaruhusiwa kupiga kura kwa kutazama, ku-like na ku-comment. Shindano hili litadumu kwa siku 30, ambapo mshindi atapatikana kupitia wingi wa Views, Likes na Comments katika wimbo wake. Cha kuzingatia ni kufuata utaratibu ambao hauwezi kuharibu kanuni za kimatandao kama vile matusi, kejeli na vitu vinavyofanana na hivyo,” alisema Isri.

Mmoja wa wasanii wanaoshiriki shindano hilo, Goweshan,  akizungumza na wanahabari.

Kwa upande wa wasanii waliwakilishwa na Goweshan  na Fetilicious, ambapo alisema:

 

“Ilikuwa ni fursa ambayo ilikuwa adimu kuipata, tumekuwa tukifanya kazi lakini, tukiwa hatuna mwanga wa wapi tutapeleka kazi zetu.

 

“Tunaishukuru Global TV Online kwa kutupatia fursa hii tena bure kabisa, kwa niaba ya wenzangu nitoe shukrani kwa uongozi ambao umeandaa jambo hili, ambapo kwetu sisi kumi, tunajihesabu kama ni washindi tayari. Tunawaomba mashabiki mtusapoti, mtupige kura na muisapoti Global. Kwa kufanya hivyo mtakuwa mmetusaidia kufikia mafanikio yetu.

Wanahabri wakifuatilia tukio hilo.

“Inawezekana usishinde leo, lakini kitendo cha video yako kuwekwa kwenye YouTube channel ya Global TV Online, tayari ni ushindi, ni heshima kubwa na ni mwanzo mzuri wa kututambulisha na kutufanya tujulikane kwa mashabiki wetu. Niwaombe wasanii wenzangu chipukizi tuwe wabunifu na tufanye kazi kwa ubora, tuitumie platform ya Global Group, tutatoboa.

 

Mmoja wa wasanii wanaoshiriki shindano hilo, Fetilicious,  akizungumza na wanahabari.

Fetilicious ambaye ni mshiriki mwanamke pekee, naye alishukuru kwa niaba wenzake:

 

“Ninashukuru na nina furaha sana kwa kuwa mimi ni mwanamke pekee ambaye nimepenya kwenye hiki kinyang’anyiro.

 

“Haikuwa rahisi, kwangu mimi hadi hapa najihesabu kama mshindi kwani kupata nafasi ya wimbo wangu kukaa Global TV Online, ni zaidi ya kuwa msindi, lakini niwaombe wanawake wenzangu wanipigie kura ili niwe mshindi.”

Baadhi wa watangazaji wa +255 Global Radio wakifuatilia tukio hilo.

Uzinduzi huu upo pia katika Chaneli ya Global Tv Online, lakini pia endelea kufuatia +255 Global Radio na magazeti ya Global Publishers, mitandao ya kijamii Global Publishers kwa maelezo ya namna mchakato wa kumpata mshindi unavyoendelea.

Issa Liponda na Joel Thomas

 

 

Leave A Reply