The House of Favourite Newspapers

Watanzania Waliokwama India Watua Bongo

0

UBALOZI  wa Tanzania nchini India, kwa kushirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania [Air Tanzania] pamoja na diaspora wa Tanzania nchini India wamefanikisha safari ya kwanza ya kuwarejesha nchini Watanzania waliokuwa wamekwama katika miji mbalimbali nchini India kutokana na zuio la kuingia na kutoka ndege za kimataifa lililowekwa na Serikali ya India kama hatua mojawapo ya kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.

 

Ndege maalum ya Boeng 787-8 ya Dreamliner ya Air Tanzania ilitumwa na Serikali jijini Mumbai kwenda kuwachukua watu hao  tangu Machi  22,  2020,  lilipowekwa zuio hilo.

 

Ndege hiyo iliondoka India jana Mei 15, 2020,  saa 2 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji International Airport, Mumbai,  ikiwa imebeba jumla ya raia wa Tanzania 246, miongoni mwao ni waliokuwa wameenda India kwa ajili ya matibabu, wahitimu kutoka vyuo mbalimbali na wanafunzi ambao wanalazimika kurudi nyumbani kwa kuwa vyuo vimefungwa hadi mwezi Agosti/Septemba 2020.

 

Ndege hiyo imewasili  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere [JNIA]  saa 6 mchana leo Ijumaa tarehe 15 Mei 2020.

Takriban Watanzania 410 walijiandikisha katika Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, na kuelezea utayari wao wa kuchangia gharama.

 

Kwa kuwa idadi yao ilikuwa kubwa zaidi ya walioweza kusafiri katika awamu hii ya kwanza, Serikali inaangalia uwezekano wa kutuma ndege nyingine maalum ya Air Tanzania kwendakuwachukua waliosalia ndani ya mwezi huu.

 

Gharama ya tiketi ya ndege hiyo, namna ya kulipa, mahali ambapo ndege itatua pamoja na tarehe za kuwasili kwa ndege hiyo nchini India zitatangazwa na ubalozi mapema iwezekanavyo.

 

Ubalozi unapenda kuwashukuru diaspora wa Tanzania nchini India kwa kufanikisha zoezi hili kwa weledi mkubwa na uongozi wa Wizara za Mambo ya Nje za India na Tanzania na serikali, kwa ujumla, kwa miongozo mbalimbali wakati wa zoezi hili.

 

Kabla ya ndee hiyo kuwasili katika uwanja wa ndee wa JNIA wazazi, ndugu na jamaa watu hao walionekana wakiwa na nyuso za furaha wakiwasubiri ndugu zao.

 

Mmoja wa wanafunzi waliokuwa wanasoma India, Sulemani Khalidi, ameishukuru serikali kwa kuwarejesha.

“Kwa kweli naishukuru sana Serikali yangu kwa kusirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini India kwa kutusaidia sisi sote hadi kufika hapa nchini leo,” amesema .

Leave A Reply