The House of Favourite Newspapers

Watoto walemavu Arusha Wampa Mrisho Gambo Changamoto Zao

0
Baadhi ya watoto walemavu wakiwa kwenye eventi hiyo.
Mmoja wa watoto walemavu kutoka Sweden (kushoto) akiongea na watoto walemavu wa Arusha.
Mtoto mlemavu akizungumzia changamoto zao.
Mtoto mlemavu kutoka Arusha akizungumzia changamoto wanazopitia.
Watoto walemavu kutoka Sweden wakisikiliza changamoto za wenzao wa Arusha.
Watoto walemavu kutoka Sweden wakitoa ushuhuda wao.

Hivi karibuni lilifanyika kongamano kubwa la watoto wenye ulemavu mkaoni Arusha ambalo lilihudhuriwa na watu mbalimbali na hivyo watoto hao kutumia fursa hiyo kumueleza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo changamoto zinazowakumba.

Katika eventi hiyo, walikuwepo pia watoto walemavu na walimu wao kutoka nchini Sweden ambao walipata fursa ya kubadilishana mawazo na wenzao wa Tanzania hivyo kuimarisha ushirikiano wao.

Wakizungumzia changamoto zinazowakabili mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Gabriel Daqqaro ambaye alimuwakilisha Gambo, mmoja wa watoto walemavu akiwawakilisha wenzake alizisoma kama ifuatavyo;

  1. Upungufu wa vifaa na nyenzo za kufundishia na kujifunzia na upungufu wa walimu wenye utaalamu wa elimu jumuishi.
  2. Kukataliwa, kubaguliwa na kutengwa watoto na vijana wenye ulemavu kuanzia katika familia zao hadi kitaifa na matokeo yake kukosa huduma stahiki na maendeleo ya malezi na makuzi yao.
  3. Baadhi ya familia kuwaua watoto wao pindi wanapogundua kwamba mtoto aliyezaliwa ana ulemavu wa aina fulani na kisha husema ‘bahati mbaya!’
  4. Uelewa mdogo wa jamii kuhusu uwezo, mahitaji na vipaji vya watoto wenye ulemavu na hivyo kusababisha mitazamo hasi ya familia na jamii kwa ujumla na matokeo yake ni watoto wengi wenye ulemavu kufungiwa ndani na hivyo kukosa huduma na haki zao za msingi kama vile upendo, elimu na afya.
  5. Miundombinu mingi kutokuwa rafiki kwa watoto wenye ulemavu mfano shuleni, barabarani, hospitalini na katika majengo ya umma na binafsi na hivyo kuwanyima fursa ya kupata huduma mbalimbali.
  6. Kubakwa kwa watoto wenye ulemavu na hivyo kupelekea kupata mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa ikiwemo maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
  1. Changamoto za usafiri wa kuwapeleka shuleni na kuwarudisha nyumbani watoto na vijana wenye ulemavu wanaoishi na kusoma katika shule zinazotoa huduma kwa wanafunzi wenye ulemavu.

Aidha, watoto hao ambao pia walitoa burudani mbalimbali walitumia kongamano hilo kutoa shukrani kwa taasisi ya kuhudumia watu wenye ulemavu kutoka nchini Sweden, FUB kupitia Mradi wa Pamoja (Come Together Concrete) ambao wamekuwa wakitoa msaada mkubwa kwao.

Pia walilishukuru Kanisa la The Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwajengea uwezo watoto wenye ulemavu katika kuzijua na kuzitetea haki zao.

Akizungumzia kongamano hilo, mratibu wa masuala ya watoto wenye ulemavu kutoka Free Pentecostal Church of Tanzania, Lucas Mhenga alisema kuwa, wamekuwa wakifanya makongamano hayo mara kwa mara katika mikoa tofauti lengo likiwa ni kuwajengea mazingira mazuri watoto hao wanaohitaji sapoti kubwa kutoka kwa jamii.

“Matukio kama haya tumekuwa tukiyafanya mara kwa mara kwenye mikoa tofauti. Kwa mfano hivi karibuni tumefanya pia Mwanza na Dodoma na lengo ni kuwakutanisha watoto hawa na kuwapa nafasi ya kueleza changamoto zao ili jamii, taasisi na serikali iwasikie na kuwasaidia,” alisema Mhenga.

Leave A Reply