The House of Favourite Newspapers

Watu 22 Mbaroni kwa Mauaji Mbeya

0

KUFUATIA kuwepo kwa wimbi la matukio ya mauaji jijini Mbeya, Jeshi la Polisi mkoani humo limewatia nguvuni watu 22 kwa tuhuma za kuhusika na vitendo hivyo, huku likitoa mwelekeo wa namna ya kumaliza matukio hayo.

 

Hivi karibuni kumekuwapo na matukio kadhaa ya mauaji, yakiwamo ya aliyekuwa mwalimu mstaafu, Edward Ndonde aliyeuawa na mwanaye Mussa Edward, Januari 12, Justine Namwinga aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Hasanga naye aliuawa na watu wasiojulikana Januari 31 huku Gloria Kibira aliyekuwa Afisa Ustawi mwandamizi aliyekutwa amenyongwa nyumbani kwake Februari 3, mwaka huu.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Februari 8, 2022, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, Ulrich Matei amesema katika operesheni na msako mkali uliofanywa maeneo mbalimbali jijini humo, limewakamata watuhumiwa hao kwa makosa ya kuhusika na matukio hayo.

 

Amesema katika upelelezi uliofanywa na Jeshi hilo, umebaini vyanzo vya mauaji hayo ni ulevi, wivu wa kimapenzi, imani potofu (ramli chonganishi), migogoro ya ardhi, kuwania mali na kujichukulia sheria mkononi.

 

“Watuhumiwa 16 kati ya 22 wamefikishwa mahakamani na wengine watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa mashauri yao kukamilika,” amesema Matei.

 

Matei amesema ili kukomesha matukio hayo, wananchi wanapaswa kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwafikisha watuhumiwa Polisi, viongozi wa serikali za Mitaa watendaji wa Kata kutumia mabaraza ya usuluishi kutatua migogoro ya ardhi na kuwatumia wataalamu waliopo katika kamati za ulinzi na usalama kutoa elimu ya namna ya kudhibiti msongo wa mawazo.

Leave A Reply