The House of Favourite Newspapers

Watu 53 Wafariki kwa Ajali ya Lori

0

TAKRIBANI watu 53 wamefariki dunia na wengine 58 kujeruhiwa kufuatia lori walilokuwa wakisafiria kupata ajali mbaya baada ya kugonga daraja na kupinduka katika jimbo la Chiapas Kusini mwa Mexico.

 

Imeelezwa kuwa takribani watu 100, waliohusika kwenye ajali hiyo wanadaiwa kuwa ni wahamiaji kutoka Marekani ya kati waliokuwa ndani ya lori hilo wakati likipata ajali.

 

Picha kutoka eneo la ajali zinaonesha waathiriwa wakiwa wametapakaa barabarani karibu na lori hilo lililopindukia huku kukiwa na miili iliopangwa ardhini ikiwa imefunikwa.

 

Luis Manuel Garcia, Mkuu wa Kitengo cha Utetezi wa Raia wa Chiapas amesema kwamba waathiriwa ni wanaume, wanawake, na watoto ambao uraia wao haujathibitishwa, lakini maafisa wa eneo hilo wanasema kwamba wengi wa waliokuwa ndani ya lori hilo ni wahamiaji kutoka mataifa ya Honduras na Guatemala.

 

Taarifa zaidi zinasema kuwa chanzo cha ajali hiyo mwendokasi mkubwa ambao ulisababisha gari kupoteza mwelekeo katika kona na kugonga daraja la Raia katika barabara kuu inayoelekea katika mji mkuu wa jimbo la Chiapas, Tuxtla Gutierrez, jimbo linalopakana na Guatemala ambapo pia ni kituo cha wahamaji wengi wasio na vibali wanaoelekea Marekani.

Mamia ya maelfu ya wahamiaji wanaotoroka umasikini na ghasia Marekani ya kati hujaribu kuvuka kupitia Mexico kila mwaka kwa lengo la kuingia Marekani.

Leave A Reply