JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limesema limewakamata watuhumiwa 267 wa makosa mbalimbali ya uhalifu wakiwemo wa madawa ya kulevya kipindi cha kuelekea sikukuu ya Pasaka kati ya Aprili 13 na 17 mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Saalam, Simon Sirro, amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na juhudi kubwa za wananchi kutoa taarifa kwa jeshi hilo na kusababisha kufaniksha kunaswa kwa watuhumiwa hao.
Ameleza kuwa baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa kutokana na makosa ya unyang’anyi na kutumia silaha, nguvu, utapeli, wizi kutoka maungoni, kucheza kamari, kuuza pombe haramu ya gongo na kupatikana na bangi.
Aliongeza kwamba katika operesheni hiyo pia jumla ya kete 366 za dawa za kulevya zimekamatwa huku puli zikiwa 150, misokoto ya bangi 51 na pombe haramu ya gongo lita 200.
Amewaomba raia wema kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kurahisisha kukamatwa kwa wahalifu. Watuhumiwa wote waliokamatwa bado wanaendelea kuhojiwa kulingana na makosa yao na pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.