The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-21

0

ILIPOISHIA IJUMAA:
“Kumbe huyu bwana halali usiku na anavuta!” nikajiambia kimoyomoyo huku nikimkodolea macho bila yeye kuniona.

Kwa vile nilimkuta mwenyewe yuko macho, nisingeweza kumuwangia mbele yake, nikarudi nje ya mlango. Hapo nikaanza kucheza ngoma yangu ya kichawi ya kumuwangia. Punde tu waziri mkuu akaanza kusinzia.

Nilipogundua kuwa nilikuwa nimeshamtia usingizi ndipo nilipoingia tena sebuleni. Nilimfuata waziri mkuu aliyekuwa akisinzia bila kuizima laptop yake. Nikamzunguka mara saba huku nikimputia kwa mwengo wangu wa kichawi niliokuwa nimeushika kwa mkono wangu wa kushoto.SASA ENDELEA…

Nilipomaliza mchezo huo nilimwambia.
“Nimekumaliza baba, wewe si waziri mkuu tena. Waziri mkuu sasa ni mimi.”
Nikaondoka na kurudi nje ya mlango ambako ilikuwa ni lazima nikite kimba.
Wakati nimechutama nikifanya hivyo, nilimuona polisi mmoja akinifuata. Bila shaka lile geti walikuwa wakilifunga na kulifungua wao.

Nilishtuka sana kwa sababu sikutarajia kuwa polisi hao niliowaacha mbele ya geti wangeingia ndani na kuniona. Niliamini kuwa yule polisi aliyekuwa akinifuata alikuwa amekingwa sawasawa huko kwao kwani kwa macho makavu asingeweza kuniona pale.
Nikajiambia: “Siku ya kuadhirika ni leo.”

Nilijua kuwa ningekamatwa na nitakapotambulika kuwa mimi ni waziri wa serikali, ningeumbuka sana.Taarifa zangu si tu zingefikishwa kwa waziri mkuu, zingefikishwa pia kwa rais wa nchi. Ingekuwa aibu ilioje!

Ningeueleza nini umma wa Watanzania kuhusu hali niliyokutwa nayo mahali hapo na pia ningewaeleza nini polisi nitakapoulizwa niliwezaje kujipenyeza hadi kufika katika mlango wa nyumba ya waziri mkuu bila kuonekana na polisi waliokuwa kwenye geti.
Bado ningetakiwa kueleza nilikuwa ninafanya nini mahali pale na kwa nini nilikita kimba langu kando ya mlango wa nyumba ya waziri mkuu.

Lakini kubwa ambalo lingewashangaza polisi hao pamoja na wananchi watakaosikia habari zangu ni vile nilivyokutwa nikiwa uchi wa mnyama nikiwa pamoja na mkoba wangu ambao una vitu vya ajabu ukiwemo mkono wa mtoto mchanga uliokaushwa.
Wakati yule polisi ananifuata nilikuwa bado nimechutama nikimaliza kujisaidia.
Sikuwa na hakika moja kwa moja kuwa alikuwa ananiona mpaka aliposimama karibu yangu na kuniuliza.

“Wewe nani na unafanya nini hapa?”
Sikumjibu kitu, nilisimama nikamgeukia na kumtazama. Sasa aliniona wazi kuwa nilikuwa uchi wa mnayama.

Polisi huyo alipata hofu akageuka haraka na kurudi mbio kwenye geti. Bila shaka alitaka kumuita mwenzake ili washangae kile kioja cha mimi kuwepo pale nikiwa uchi.
Vile alivyonipa mgongo tu akanipa nafasi ya kukimbilia kwenye ukuta, mahali palepale nilipoingilia. Nilijigandamiza na ukuta huo na kuibukia nje ya ukuta.

Kama yule polisi alirudi na mwenzake, sikuweza kuyajua tena kwani nilipotokeza nje nilitembea harakaharaka kulifuata gari langu.

Ule ulionikuta pale ulikuwa ni mtihani. Lilikuwa tukio ambalo sikulitegemea. Kama nisingekuwa na ujasiri wa kumuelekea yule polisi na hivyo kumtishia, ningekuwa na njia nyingine ya mwisho ya kumputia polisi huyo na mwengo wangu ili apotewe na fahamu.
Kama asingepotewa na fahamu kutokana na mizizi aliyokula huko kwao, nisingekuwa na njia nyingine zaidi ya kuumbuka.

Nilipolifikia gari langu nilijipakia nikaliwasha moto na kuliondoa nikiwa bado nipo uchi. Sikuwa na muda wa kuvaa nguo zangu kwa vile nilishuku wale polisi wangeweza kunifuatilia na kunikamata nikiwa kwenye gari.

Wakati naendesha gari hilo nikapata wazo lingine lililonitia hofu. Nilishuku kwamba huenda yule polisi aliniona sura yangu na kunitambua kuwa ni waziri nimekwenda kumuwangia waziri mkuu na kukita kimba mbele ya mlango wa nyumba yake.
Kama itakuwa hivyo, nilijiambia, taarifa itafikishwa kwa waziri mkuu usiku uleule na huenda nikachukuliwa hatua.

Hatua pekee ambayo ningechukuliwa ni kutumwa polisi waje wanikamate nyumbani kwangu na kesho asubuhi rais akishafahamishwa nilichokifanya atanifuta kazi.Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Leave A Reply