The House of Favourite Newspapers

Chuzi Ndo Hilo -23

0

ILIPOISHIA IJUMAA WIKIENDA:

Amwombeje samahani? Aliamua kumwandikia ujumbe wa simu badala ya kumpigia akiamini kwa kusoma atamwelewa vizuri zaidi kuliko kumwendea hewani. Kwanza anaweza asipokee hata hiyo simu yake. Aliandika:

“Baba Shua, najua kosa langu, nimekutenda vibaya sana mume wangu. Nakiri kosa moja kwa moja. Niko chini ya miguu yako mume wangu, nisamehe sana sana! Sitarudia tena, ni shetani tu alinipitia. Sasa nimejitambua ujinga wangu. Please mume wangu. Nisamehe saba mara sabini.” Akatuma.
JIACHIE MWENYEWE SASA…

Baba Shua hakujibu meseji hiyo. Ilifika mahali, mama Shua akaamini kuwa, mumewe alikuwa bize hivyo hajaona meseji yake, akaamua kubipu. Lakini licha ya kubipu, bado mumewe hakumpigia…

“Sijui kama nina ndoa tena! Ina maana baba Shua amebadilika kiasi hiki? Yaani ajue jambo zito kama la mimi kulala na mwanaume mwingine halafu aendelee na shughuli zake? Lazima kuna jambo baya sana anataka kunifanyia,” alisema moyoni mama Shua.

Siku hiyo aliamua asiende kazini. Aliamua kukaa nyumbani huku kazini kwake akiaga kwa uongo kwamba anasumbuliwa na kichwa.Kingine kilichokuwa kikimpa wakati mgumu mama Shua, aliamini kwamba mume wake atapeleka habari zake nyumbani kwao kijijini jambo ambalo anajua linaweza kusababisha kifo cha ghafla cha mama yake mzazi…

“Yaani afadhali haya mambo tuyaongee wenyewe, akisema anampigia simu mama kumwambia nimempoteza mama yangu. Lakini hivi mimi hii tabia nimerithi kutoka kwa nani? Kwa baba au mama?
“Mbona sijawahi kusikia hadithi yoyote inayosema mama alikuwa mhuni au baba alikuwa mhuni. Au wananificha? Au mimi nimeathiriwa na mazingira?” alijiuliza yote mama Shua.
***
Kule kazini, baba Shua muda mwingi alikuwa mwenye mawazo. Aliiona meseji ya mke wake, lakini hakutaka kumjibu. Na aliona alipobipu lakini pia hakutaka kumpigia.

Mara simu yake iliita, akaangalia skrini na kushtuka sana baada ya kuona jina la Maua.
Maua ni msichana aliyekuwa na uhusiano na baba Shua kabla ya kukutana na mama Shua.
Baba Shua alimpenda sana Maua kiasi kwamba, alikuwa tayari kwa ndoa naye lakini alipotokea mama Shua, alijikuta akitekwa na kumsahau Maua.

Uhusiano wao ulikufa polepole mpaka kila mmoja akajikuta akichukua hamsini zake. Baadaye, baba Shua akamuoa kwa ndoa mama Shua…
“Haloo,” baba Shua aliipokea simu ya Maua…
“Haloo…mzima wewe?”
“Mimi mzima. Sijui wewe?”

“Mimi pia mzima. Niko hapa kwenye mgahawa jirani na kazini kwako, nikasema nikupigie ili kama hutajali uje tushiriki kifungua kinywa cha pamoja.”
“Wapi? Hapo Bianca?”
“Ndiyo.”

“Nakuja Maua.”
“Karibu sana.”
Baba Shua alifunga mlango wa ofisi, akaenda Mgahawa wa Bianca na kukutana na Maua.
Ni Maua bila kujali kuachwa, alipomwona baba Shua alisimama, akamkumbatia na kumpiga mabusu mawili ya nguvu…

“Mmm…mwaa….mmmwaa.”
“Asante Maua…za siku nyingi?”
“Njema, sijui wewe?”
“Mi mzima sana Maua.”
“Nakuona umenawiri mpenzi…ni hiyo ndoa au nini?”
“Ah! Maua…nadhani ni wakati wa mwili wenyewe tu. Ndoa si sababu…”
“Kwa nini Benny?”

“Ah! Nimeingia chaka Maua.”
“Umeingia chaka! Kivipi Benny?”
“Maua…nimeoa malaya.”

“Ha..! Benny…unajua hilo neno ni zito sana…umeoa malaya?”
“Niamini mimi Maua…ngoja nikupe mkasa mzima,” alisema baba Shua na kuanza kumsimulia mkasa mzima Maua kuhusu mke wake, mama Shua.
Baba Shua alitumia kama nusu saa nzima kusimulia kisa cha mama Shua na Musa. Hata alipomaliza, alihema kwa kasi kubwa ya kusimulia…

“Lo! Asee! Kwa hiyo huyo kijana Musa ndiyo mwiba kwenye ndoa yako? Sasa umeamuaje?” aliuliza Maua.
“Maua, ungekuwa wewe ndiye umekumbana na kisanga hiki hata kwa jinsia yako ungeamuaje?”
“Ningeamua kusamehe.”

“Hapana! Ni ujinga wa hali ya juu. Haiwezekani.”
“Sasa wewe unataki kufanyaje?”
“Hakuna ndoa Maua. Mwanamke anakuletea mwanaume mpaka ndani, wewe upo. Unamsema lakini bado anaendelea tu!?”

“Niachie mimi, nitaamua,” alisema baba Shua uso wake ukionekana kuwa makini sana.
“Da! Pole sana Benny. Mambo mengine vipi lakini?” Maua aligeuza kibao cha mazungumzo…
“Poa sana. Sikutegemea kama leo utanipigia, nimefurahi sana.”
“Kweli? Hata mimi nimefurahi sana wewe kukubali mwaliko wangu. Maana bwana, mtu akishakuwa kwenye ndoa, hataki tena ahadi, hataki mtoko.”

Baba Shua alicheka, akamuuliza…
“Bado unaishi Temboni?” baba Shua alimuuliza Maua…
“Kulekule lakini nyumba kama ya tano toka pale nilipokuwa nikikaa zamani. Karibu sana Benny…”
“Nitakuja siku moja…”
“Lini nijiandae.”

“Ujiandae kwa kufanyaje? Umfukuze shemeji uliyenaye sasa hivi?”
“Ha! Wala! Mimi pale haingii mwanaume labda awe ndugu yangu.”
“Mbona mimi unaniruhusu nije kuingia?”
“Sasa wewe historia yako kwangu ni tofauti na wengine. Wewe ni kama mtalaka wangu. Kwa hiyo una nafasi yako ya pekee.”

“Basi nitakuja wikiendi hii,” alisema baba Shua…
“Mimi sitaki uje wikiendi hii…”
“Unataka lini?”
“Leo!”

“Mh! Mbona ghafla sana Maua?”
“He! Jamani! Kwani nyie wanaume mna ghafla?”
Je, nini kitaendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, siku ya Jumatatu.

Leave A Reply