The House of Favourite Newspapers

Waziri Mkuu: Migogoro Ya Wakulima Na Wafugaji Haina Tija, Serikali Haitaki Kuiona – Video

0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kitendo cha wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima ni uvunjaji wa sheria na Serikali haitovumilia vitendo hivyo na amewataka wafugaji wafuge mifugo yao kulingana na ukubwa wa maeneo yao ya malisho.

“Kilimo ni maisha, kilimo ni biashara, kilimo ni fedha na vivyo hivyo ufugaji ni maisha, ufugaji ni biashara na ufugaji ni fedha hivyo kila mkulima alime kulingana na ukubwa wa eneo lake na mfugaji afuge mifugo kilingana na ukubwa wa eneo lake na malisho. Sisi sote ni Watanzania na tunataka utajiri. Wakulima na wafugaji waheshimiane kwani wote ni Watanzania.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo Jumanne, Novemba 14, 2023 wakati akizungumza na wananchi kwenye vijiji vya Nanjaru na Mkaranga vya Kata ya Nambilanje na kijiji cha Nankonjera kilichopo Kata ya Namichiga akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Waziri Mkuu amesema migogoro baina ya wakulima na wafugaji haina tija na Serikali haitaki kuiona ikiendelea na kwamba kati yao hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine, hivyo kila mmoja aweke mpango kazi ambao hautaathiri upande wowote.

Kadhalika Waziri Mkuu amewataka watendaji wa vijiji kabla hawajagawa maeneo kwa wafugaji wahakikishe idadi ya mifugo waliyonayo na washirikishe Serikali ya kijiji na wananchi. “Wafugaji badilikeni fugeni kisasa, msione fahari kuwa na idadi kubwa ya mifugo ambayo mnashindwa kuihudumia. Fugeni mifugo michache ambayo mtaihudumia vizuri na kuiuza kwa gharama kubwa.”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya Ushirika kuhakikisha wanausimamia vizuri na kwa uaminifu mkubwa. “Acheni kuwaibia wakulima na badala yake wasimamieni vizuri na vipimo viwe vya uhakika. Wanapoleta mazao yao maghalani msiwaibie.”

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka nguvu kubwa katika sekta ya kilimo lengo ni kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara, hivyo watendaji wahakikishe kinasimamiwa vizuri ili kuongeza tija.

Leave A Reply