The House of Favourite Newspapers

Waziri Ummy Awataka Watanzania Kuchangamkia Fursa za Corona

0
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (wa pili kutoka kulia), akipokea hundi ya Sh bilioni 1.1 kutoka kwa Makamu Rais; Maendeleo Endelevu kutoka kampuni ya GGML, Simon Shayo (kulia), fedha hizo zimetolewa na kampuni hiyo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya Corona. Wengine ni Meneja Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya ubia, Manace Ndoroma(wa pili kutoka kushoto) na Mwenyekiti wa TPSF, Angelina  Ngalula (kushoto).

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa wito kwa wawekezaji wa viwanda ndani ya nchi kuchangamkia fursa za uzalishaji wa vifaa tiba na kinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kutokana na fedha zinazochangwa na makampuni mbalimbali kudhibiti maambukizi ya Corona nchini.

 

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo leo Mei 6, mwaka jijini Dar es Salaam, wakati akipokea hundi ya Sh bilioni 1.1 kutoka kampuni ya uchimbaji wa madini Geita (GGML).

GGML imekabidhi fedha hizo kwa lengo la kuunga mkono Serikali mapambano dhidi ya maambukizi ya Corona.

 

Alisema Serikali inaendelea kuthamini msaada mkubwa unaotolewa na wadau hao katika kuonesha jitihada za kuwalinda watumishi wa afya waliomstari wa mbele kudhibiti maambukizi ya Corona.

 

“Niwaombe wadau wanaotoa misaada kutoka nje ya nchi, kuzingatia muongozo wa upokea wa dawa na vifaa tiba kwa kuhakiki ubora. Tutaendelea kuelekeza TMDA, kuhakikisha wanaongeza umakini uhakiki ubora na usalama, kumekuwa na wimbi la uingizaji wa vifaa tiba hivyo lazima kuhakikisha ni salama na vina vigezo vinavyohitajika.

 

“Pia natoa wito kwa viwanda vya ndani kwamba tunahitaji sana barakoa, PPE, sanitizer, tungependa sana hela hii ielekezwe kununua vifaa vinavyozalishwa ndani ya nchi, mfano barakoa za ndani ya nchi, kuna kiwanda Pugu lakini uwezo bado mdogo,” alisema

 

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi hiyo, Makamu Rais, Maendeleo Endelevu GGML, Simon Shayo alisema GGML pia imezindua mikakati kadhaa ya kupambana na janga hili ambalo lilibisha hodi hapa nchini Machi 16 mwaka huu na kuathiri zaidi ya watu 400 hadi kufikia sasa.

 

Alisema mikakati hiyo inalenga kushirikiana na serikali pamoja na watalaam wa afya kuelimisha jamii kuhusu virusi vya Corona ikiwa ni pamoja na kugawa vifaa kwa jamii inayozunguka mgodi na wafanyakazi wa GGML kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

 

“Kwanza tumekabidhi hundi hii ya Sh bilioni 1.1 ni sehemu ya Sh bilioni 1.6 fedha ambazo GGML imetoa katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona nchini.

“Fedha hizi Sh bilioni 1.1 zitaelekezwa kwenye ngazi ya kitaifa kupitia Mfuko Maalum wa mapambano dhidi ya Covid – 19 ambao unasimamiwa na ofisi ya Waziri Mkuu.

 

Hata hivyo, Shayo alisema fedha hizo Sh bilioni 1.1 ni sehemu ya mpango wa GGML ambayo imetoa kiasi cha Sh bilioni 1.6 ambapo kati yake kiasi cha Sh milioni 500 zinatumika kwa ajili ya kusaidia juhudi zinazofanywa katika ngazi ya mkoa na jamii.

 

“Pia zitajumuisha ununuzi wa vifaa-tiba muhimu na vitendea kazi kama vile vifaa vya kujikinga, barakoa, mashine za kusaidia upumuaji,” alisema.

 

Pia alisema GGML ilikabidhi matanki 10 yenye ujazo wa lita 1000 kila moja yaliyowekwa kwenye sehemu za wazi za mji wa Geita ili uwawezesha wananchi kuosha mikono.

 

“GGML pia imetoa kimiminika cha klorini ambacho kinatumika kutakasa mikono badala ya sabuni.

“Mradi huo pia unawezeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mjini Geita (GEUWASA) ambayo itatoa maji kila mara ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inapatikana kwa umma wakati wote.

 

“Matanki hayo ambayo ni sehemu ya usambazaji wa msaada huo yamewekwa katika maeneo yafuatayo: Kituo cha mabasi (2), Kituo cha Mwatulole (1), Kituo cha Shilabela (1), Kituo cha Nyankumbuko (1), soko la Nyankumbuko (1), hospitali ya Geita (1), Soko la Dhahabu (2), na kituo cha Moyo watoto yatima cha Huruma (1),” alisema.

 

Aidha, aliongeza kuwa katika kujenga uelewa juu ya janga hili kwa jamii zinazozunguka mgodi, GGML imekuwa ikigawa vipeperushi vyenye taarifa za virusi ndani na nje ya mgodi.

“Vilevile kwa kupitia vyombo vya habari, GGML imeingia ubia na Rubondo fm ambacho ni kituo cha redio kinachomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa lengo la kuelimisha juu ya janga la Covid-19,” alisema

Alisema lengo la mikakati hiyo ni kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya janga hili ambalo limekwamisha shughuli mbalimbali za kiuchumi,” alisema.

 

NA MWANDISHI WETU

 Ameacha mke na watoto wanne.

Leave A Reply