The House of Favourite Newspapers

Winga Mzambia Mambo safi Yanga

0

ACHANA na uwezo mkubwa aliouonyesha starika Muivory Coast, Yikpe Gnaimen, unaambiwa yupo winga Mzambia, Eric Kabamba, huyu ni hatari na tayari benchi la ufundi la Yanga limepitisha jina lake ili asajiliwe kwa ajili ya kukipiga Jangwani.

 

Winga huyo aliyewahi kuichezea Buildcon ya Zambia, alitua nchini tangu wiki iliyopita kwa ajili ya kufanya majaribio ili asajiliwe na timu hiyo kwenye usajili huu wa dirisha dogo unaotarajiwa kufungwa Januari 15, mwaka huu.

 

Yanga hadi hivi sasa chini ya udhamini wa Kampunmi ya GSM, tayari imefanikiwa kuwasajili wachezaji watano ambao ni Haruna Niyonzima, Yikpe Gnaimen, Ditram Nchimbi, Tariq Seif na Adeyum Saleh huku ikiendelea kumjaribu Owe Bonganya aliyewahi kuichezea TP Mazembe.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, tayari benchi la ufundi la Yanga chini ya Charles Boniface Mkwasa, limekabidhi jina la winga huyo kwa mabosi wa GSM ambao ndiyo wanaofanya michakato yote ya usajili.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa benchi la ufundi la timu hiyo wamelipitisha jina la winga huyo baada ya kuvutiwa na kiwango kikubwa ambacho amekionyesha kwenye majaribio tangu ajiunge na timu hiyo kabla na baada ya kwenda Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi.

 

“Benchi la ufundi tayari wamelipitisha jina la huyo winga wa Zambia kwa ajili ya kusajiliwa. Mkataba wake utakuwa ni wa miaka miwili.

 

“Hivyo kilichobakia ni GSM kufanya mchakato wa kukamilisha usajili wake ili asaini mkataba wa kuichezea Yanga, pia washughulikie vibali vyake vya kufanya kazi na ITC itakayomuwezesha kucheza ligi.

 

“Benchi la ufundi tayari wenyewe wamevutiwa na kiwango chake ambacho amekionyesha akicheza nafasi zote za winga wa pembeni namba 7 na 11,” alisema mtoa taarifa huyo. Alipotafutwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said kuzungumzia hilo, alisema kuwa:

 

“Sisi ni kama wadhamini tunaofanikisha usajili kwa kutoa fedha pekee, masuala mengine yote yanayohusu majaribio ni benchi la ufundi, hivyo kama wao wamekubali uwezo wake basi hamna shida, tutahakikisha tunafanikisha usajili wake.”

 

Ikumbukwe kuwa, Mkwasa alikuwa kaimu kocha mkuu wa Yanga kabla ya ujio wa Mbelgiji, Luc Eymael ambaye anakuja kuchukua mikoba ya Mwinyi Zahera raia wa DR Congo.

Leave A Reply