The House of Favourite Newspapers

Wizara ya Afya: Toboa Barakoa Kabla Hujaitupa

0

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imetoa wito kwa wananchi kuteketeza barakoa baada ya kumaliza matumizi yake ili kuepusha kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko hususan virusi vya corona.

 

Mkuu wa Kitengo cha Maji na Usafi wa Mazingira katika Wizara ya Afya, Anyitike Mwakitalima, amesema wale ambao wamevaa barakoa zinazotakiwa kutupwa baada ya kutumika, wakumbuke kuitoboa ili mtu mwingine asiweze kuiokota na kuitumia.

 

Aidha, kwa wale ambao wanatumia barakoa za kitambaa, wahakikishe wanabadilisha kila baada ya saa nne ili kuepusha kupata magonjwa mengine na ni muhimu kabla ya kuivaa zifuliwe kwa maji na sabuni kisha ipigwe pasi ili kujiweka salama.

 

“Mnaovaa barakoa zile ambazo zinatakiwa kutupwa baada ya kutumika, mkumbuke kabla hujaitupa uitoboe ili mtu mwingine asiweze kuiokota na kuisafisha akairudisha katika mzunguko, jambo litalosaidia kuepusha magonjwa ya mlipuko hasa corona.

“Kwa mnaovaa barakoa za kitambaa basi mkumbuke zinatakiwa zivuliwe kila baada ya saa nne mpaka sita, na hakikisha unaifua kwa maji na sabuni, umeinyoosha ili kama kuna virusi humo waweze kufa. Msivae barakoa ambazo ni chafu,” amesema Mwakitalima.

 

Katika baadhi ya nchi imethibitika kuwa, mgonjwa mmoja wa Covid-19 anaweza kuambukiza mpaka watu kumi kwa wakati mmoja, hii inatokana na mwingiliano uliopo baina ya watu.

 

Ofisa wa Jeshi la Polisi, Staff Sergeant Valentine Ngowi, amewataka wazazi kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya corona kwa watoto wao. Wawahimize kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka. Pia wasiache watoto wakizurura mitaani kuepusha kuokota barakoa zilizotupwa ovyo.

 

Leave A Reply