The House of Favourite Newspapers

Y -TONY: MUDA UKIFIKA LAZIMA ‘NITUSUE’

0
Msanii wa Bongo Fleva, Y-Tony

WIMBI la vijana wenye uwezo wa kweli katika Muziki wa Kizazi Kipya linazidi kuchipua. Orodha yao ni ndefu lakini hapa yupo dogo ambaye kama utasikiliza nyimbo zake, unakubali kwamba ni kifaa hasa, ambacho ili kiweze kuingia katika levo zao, anachohitaji ni muda tu! Jina lake halisi ni Elly Michael Kilema, ingawa ulimwengu wa kiburudani, unamtaja kwa nomino ya Y-Tony, ikiwa utambulisho wake rasmi kimuziki.

Kiasili, Y Tony ni mwenyeji wa Mkoa wa Morogoro, ambaye alianza harakati za muziki tangu mwaka 2007, licha ya kukutana na misukosuko mingi iliyomkatisha tamaa, lakini akakomaa na hadi kusimama, amekutana na mengi.

“Nilianza kutamani kuimba nikiwa kijana mdogo sana, kila wakati nilipenda sana kuimba nyimbo mbalimbali, lakini pia hata watu wangu wa karibu walikuwa wakiniambia naweza kuimba, sauti yangu ina mvuto na nzuri kusikiliza,” anaanza kueleza Y-Tony. Ilipofika mwaka 2007, alibahatika kurekodi Wimbo wa Roho Juu, akimshirikisha mkongwe Mr. Blue.

“Wakati huo nilikuwa nasoma, hivyo sikuwa na pesa kabisa, lakini kuna rafiki yangu anaitwa Clinton Filipo, yeye alikuwa akifanya biashara, akanisaidia shilingi laki mbili na kumtafuta jamaa yetu mmoja, ambaye yeye alikuwa akijuana na HK, mmoja wa wadau wakubwa sana wa burudani, hivyo akatupeleka kwake.

“HK alitutafutia studio, lengo likiwa tuimbe wawili na huyo mwenzangu lakini mwenzangu ikawa ngumu sana kuingiza sauti kwenye beat, mwisho kabisa akakata tamaa na kuniacha niendelee, hapo ndipo nikaimba Wimbo wa Roho Juu, nikamwambia HK kuwa nampenda sana Mr. Blue, hivyo ningefurahi sana kufanya naye kazi, kweli HK akamtafuta na akaingiza voko kwenye ngoma yangu,” anasema Y-Tony.

“Sikuishia hapo, mwaka 2011 niliachia tena Wimbo wa Mama Zopilo, ingawa haukufanya poa sana, lakini pia sikukata tamaa, ingawa nilisimama na kuondoka tena kwa HK, maisha yakasonga lakini baadaye nilirudi tena kwa jamaa na kuachia Wimbo wa Pendo.

“Januari Mosi, Mwaka 2013 niliachia Wimbo wa Masebene, lakini haukubamba, rafiki yangu mmoja ambaye kwa sasa ni marehemu anaitwa Bony, alinisaidia sana kwa kunipeleka kwa Maneke, nikaimba Wimbo wa Nice Cake, hadi hapo bado sijajulikana sana na kiukweli nilikuwa sijatusua,” anasema Y- Tony.

“Kitu cha ajabu sana ni kwamba, Wimbo wa Masebene uliotoka mwaka 2013, lakini ulikuja kubamba mwaka 2014, ukawa gumzo kupindukia kiasi kwamba watu wakaanza kunifahamu sana, shoo zikaanza kumiminika, lakini lipo kosa moja ambalo nilikuwa nalifanya,” anasema na kuongeza; “Nikawa napata shoo za kila mara, lakini eti kwenye malipo nikawa natamka hata laki mbili au tatu mpaka tano, watu wakawa wananilipa hata kwa miamala ya mtandao wa simu tena yote, sasa sijui ulikuwa ni utoto, nilipishana sana na pesa, lakini kwa sasa nahangaika sana kutafuta pesa, nilichezea wakati wa Masebene, utoto bwana,” anajilaumu Y-Tony.

Msanii huyo anasema kiasi hicho cha pesa, ingawa kilikuwa kidogo lakini kilimsaidia kumuuguza mama yake mzazi, ambaye ni mgonjwa wa miguu asiyejiweza kutembea, ugonjwa ambao amekuwa nao kwa zaidi ya miaka saba na bado anaendelea kumhudumia kwa kila anachokipata kwa sababu bila mzazi wake huyo hakuna ambaye angemjua.

Y-Tony anaweka wazi kuwa baada ya Masebene, aliachia ngoma ya Wivu Wangu, ambayo ilibamba vilivyo na kwa sasa ameachia wimbo mpya alioupa jina la Safina. “Nimetoa Safina, maudhui yake yanazungumzia maumivu ya kimapenzi, unajua hata Masebene ilitokana na kuumizwa sana na msichana niliyempenda, kifupi ni kwamba nyimbo zangu zote zinatokana na kuumizwa kihisia na mapenzi,” anasema Y-Tony.

NA : BRIGHTON MASALU | RISASI JUMAMOSI | MAKALA

Leave A Reply