The House of Favourite Newspapers

Yamkuta Baada ya Kurithi Mke wa Jamaa Aliyezushiwa Kufa

0

SEKESEKE limezuka katika nyumba moja eneo la Aboloi Teso, nchini Kenya, baada ya jamaa kurejea nyumbani kwake na kumshambulia jirani yake aliyemkuta “amemrithi” mkewe.

 

 

Duru zinaarifu kwamba jamaa alipandwa na hasira alipofika kwake na kukuta jirani yake huyo akiwa amehamishia makazi katika nyumba yake.

 

Imeelezwa kuwa, kisa hicho kimetokana na jamaa huo aliyeoa miaka minne iliyopita, kwenda mjini kutafuta kazi na akamuacha mkewe kijijini, ambako jirani yake aliamua kumrithi mke wa jamaa baada ya tetesi kuibuka kijijini hapo kuwa jamaa huyo huenda alikuwa ameaga dunia.

 

Taarifa zaidi zinasema kwamba hivi karibuni mwenye mke alifunga safari kutoka mjini kurejea kijijini bila kumjulisha yeyote na alipofika alimkuta njemba akiwa amejiachia kwenye nyumba yake.

 

“Unafanya nini nyumbani kwangu na mke wangu?” jamaa alimchimba mkwara jirani yake.

Jirani alishindwa apitie wapi ili akimbie kichapo kilichokuwa kimemkodolea macho.

“Nilipata habari kuwa umemrithi mke wangu. Ulimrithi kama nani?” jamaa alimuuliza jirani yake.

 

Habari ziliwafikia majirani kuhusu kisanga hicho nao wakatoka mbio kwenda nyumbani humo kuthibitisha ni kweli jamaa waliyedhani amefariki dunia alikuwa amerejea.

 

“Hauwezi kumrithi mke wangu na mimi mwenyewe ningali hai. Leo utajua mimi ni nani,”  aliapa huku akirudi nyuma kuokota mpini wa jembe atwange jirani.

 

 

Katika harakati ya jamaa kurudi nyumba kuokota mpini, jirani alipata mwanya akachomoka mbio kukimbilia kusikojulikana.

 

“Hata ukitoroka uende wapi lazima nitakutafuta. Kwako ni hapa tu,” jamaa aliwaka huku majirani wakiangua kicheko.

 

“Kazi ya huyu jamaa ni kunyemelea wanawake wa watu. Leo amekipata. Na bado!” jirani mmoja alisikika akisema.

 

 

Inasemekana jamaa hakukomea hapo kwani aliwatahadharisha waliokuwa wakieneza uvumi eti alifariku dunia.

 

“Waliotangaza kuwa mimi nimekufa sasa aibikeni. Ninajua huyu jirani yangu ni mmoja wa wale wenye kueneza porojo hizo. Atanitambua. Sijamalizana na yeye,” jamaa aliapa.

Chanzo – Tuko News

Leave A Reply