The House of Favourite Newspapers

Yanga: Manji Arudi Tu, Tunamkaribisha

0

UONGOZI wa Yanga, umesema kuwa umezisikia taarifa za kurejea kwa aliyekuwa mwenyekiti klabu hiyo, Yusuf Manji na kuzipokea kwa mikono miwili, huku wakiamini kwamba akiungana na wadhamini wao, Kampuni ya GSM watafanikisha malengo yao.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu zienee taarifa za Bosi wa Makampuni wa GSM, Gharib Said Mohamed zikidai kumkaribisha Manji katika klabu hiyo kwa ajili ya kuongeza nguvu.

 

Awali, zilikuwepo taarifa za Manji kurejea klabuni hapo kwa ajili ya kuweka mambo sawa kama ilivyokuwa zamani baada ya kuona hivi sasa inapitia kipindi kigumu katika kupata mafanikio.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa, alisema wao kama uongozi, wanafurahi kuona wapo baadhi ya watu wanaoitakia mema klabu hiyo na wapo tayari kuwekeza kwa ajili ya kuirudisha Yanga katika levo zake.

Mfikirwa alisema, Yanga ni klabu kubwa na yenye malengo, hivyo uongozi umefurahishwa na taarifa hizo za kurejea kwa Manji wakiamini wakiungana kwa na GSM, basi watafanya mengi makubwa.

 

Aliongeza kuwa, katika kuelekea mfumo wa mabadiliko, anaamini watafikia malengo mazuri katika kuitengeneza Yanga ya kisasa itakayotikisa.

 

“Sisi kama uongozi wa Klabu ya Yanga, kwanza tunafurahi kuona kuwa wapo watu ambao wanaitakia mema klabu yetu, na wapo radhi kuwekeza kwa ajili ya kuirudishia Yanga nguvu, tumezisikia habari za aliyekuwa Mwekezaji wetu Manji kurudi na kwetu hizi ni taarifa njema.

 

Arudi tu, tunamkaribisha.“Yanga ni timu ya wananchi na tunapoelekea katika mfumo wa mabadiliko kila mtu aliye na uhitaji wa kuwekeza kwenye kikosi cha Yanga anakaribishwa, na jambo zuri ni kwamba bosi na mdhamini wetu Kampuni ya GSM chini ya bosi, Gharib Said, naye ameonekana kutokuwa na tatizo na hilo.

 

“Yanga ni timu kubwa na malengo ya uongozi wetu ni kutaka kuijenga taasisi imara zaidi hasa kiuchumi kupitia uwekezaji, hiyo ndiyo sababu unaona tumesimama imara katika kuhakikisha tunausimamia mchakato wa mabadiliko ukamilike haraka na kwa usahihi, ili tuanze mchakato wa uwekezaji,” alisema Mfikirwa.

 

Ikumbukwe kuwa, chini ya utawala wa Manji, Yanga ilikuwa juu kiuchumi na hata uwanjani ikiwazidi wapinzani wao wa jadi, Simba ambao kwa sasa ndio vinara wakionekana kuwa klabu yenye mafanikio makubwa kuanzia ndani hadi nje ya uwanja.

 

Wakati Manji anajiweka kando na kuendelea na shughuli zake binafsi, mashabiki wengi wa Yanga walimuomba abadilishe maamuzi lakini haikuwa hivyo na tangu kuondoka kwake wamekuwa wakidai kuwa kuna pigo kubwa na pengo lake limekuwa halizibiki kiasi kwamba Simba wamekuwa wakitawala soka la Tanzania kwa muda wote huo.

WILBERT MOLANDI NA JOEL THOMAS, DAR

Leave A Reply