The House of Favourite Newspapers

Yanga SC Yatua Usiku Kuwasubiri Prisons Taifa

0

Wilbert Molandi | Championi Jumatano | Habari

MSAFARA wa wachezaji 22 na viongozi wa Yanga, umepanga kutua jijini Dar es Salaam kesho Alhamisi saa 2:10 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Fastjet, ukitokea Geita timu hiyo ilipoweka kambi.

Timu hiyo, iliweka kambi Geita kabla ya wikiendi iliyopita kuvaana na Mbao FC katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la FA iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mchezo uliomalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0.
Mara baada ya mchezo huo kumalizika, Yanga ilirejea Geita ilipoweka kambi yake ya pamoja kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja Mkuu wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema timu hiyo itaondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa moja kamili usiku wakitokea Geita. Saleh alisema, kambi hiyo wameitumia vema kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo na Prisons na mingine minne inayofuata kuhakikisha wanashinda yote ili wautetee ubingwa wa ligi hiyo.

“Kwa ujumla kikosi chetu chote kipo fiti na tayari kwa ajili ya mechi zote tano za ligi kuu zinazofuata ikiwemo ya wikiendi hii tutakapokutana na Prisons. “Hivyo basi tunatarajia kuondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa moja kamili usiku na tunatarajia kufika huko Dar saa 2:10 usiku na ndege ya Fastjet. “Tukifika tu moja kwa moja tutaingia kambini kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya kucheza na Prisons,” alisema Saleh.

Leave A Reply