The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaikandamiza Singida (Picha +Video)

0

IKIWA imetoka kuchapwa mabao 4-1 na Simba wikiendi iliyopita, Yanga jana Jumatano ilipoza machungu ya mashabiki wake baada ya kuikandamiza Singida United mabao mabao 3-1.

 

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar, timu zote zilianza zikiwa na hamu kubwa ya kupata ushindi.

Singida United ambayo haina tena chake katika Ligi Kuu Bara baada ya kuwa timu ya kwanza kushuka daraja msimu huu, hivi sasa inakamilisha ratiba tu, huku Yanga ikipambana kwa nguvu zote kuhakikisha inamaliza nafasi ya pili na kuipiku Azam FC.

Singida ilianza vizuri ambapo hadi dakika ya 25, ilikuwa imelishambulia lango la Yanga mara tano, huku mashuti matatu yakilenga lango.Dakika ya 33, Paul Godfrey ‘Boxer’ aliiandikia Yanga bao la kwanza akimalizia mpira uliokuwa ukizubaa.

 

Kabla ya hapo, Mrisho Ngassa alifanya kazi kubwa ya kuwahadaa walinzi wa Singida ndiyo likapatikana bao hilo.Dakika nne baada ya kuingia kwa bao hilo, Ngassa alifunga bao la pili akipokea pasi ya Deus Kaseke huku akiwazidi maarifa walinzi wa Singida, kisha kuuinua mpira uliopita juu kidogo mwa kipa, Owen Chaima na kujaa wavuni.

 

Kuingia kwa bao hilo, kukawaamsha zaidi mashabiki wa Yanga ambao tangu Jumapili walikuwa na hasira za kufungwa na watani wao, Simba.

Kabla ya Yanga haijafunga bao la pili jana, ilishuhudia kiungo wake, Rapahel Daud akitolewa mapema uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Ditram Nchimbi dakika ya 36.

Wakati watu wakiamini timu zitaenda mapumziko matokeo yakiwa 2-0, Singida United walijipanga vizuri na kupata bao la kwanza dakika ya 45+2 likifungwa na Stephen Sey kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona.

 

Wakaenda mapumziko Yanga 2-1 Singida.Kipindi cha pili ambacho kilikuwa na mashambulizi ya hapa na pale huku kila upande ukilisakama lango la mwenzake, Yikpe Gnamien wa Yanga aliongeza bao la tatu dakika ya 64 akifunga kwa ufundi mkubwa. Hadi mwisho, Yanga 3-1 Singida.

 

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 67 katika nafasi ya pili, huku Azam ikiwa ya tatu na pointi zake 65.Matokeo mengine ya mechi za jana ni; Mtibwa 1-0 Azam, Namungo 1-0 Mbeya City, Kagera 1-0 Coastal, JKT TZ 1-1 Alliance na Ndanda 2-1 Prisons.

Leave A Reply