The House of Favourite Newspapers

Yanga Yatua Kwa Mghana Fundi wa Pasi

0

KAMA ulifikiri mabosi wa Yanga wamemaliza kusajili basi unajidanganya, kuna mtu anaitwa Rashid Nortey, raia wa Ghana, yupo kwenye rada za timu hiyo.


Nortey ni kiungo mchezeshaji
anayekipiga Medeama FC inayoshiriki Ligi Kuu Ghana, anatajwa kuwa kwenye mipango ya mabosi wa Jangwani kwa ajili ya kukiimarisha kikosi hicho.

 

Nortey ambaye alizaliwa Novemba 21, 1995, anatajwa kuwa ndiye kiungo bora chipukizi kwa sasa kwenye nchi ya Ghana akitajwa kuwa ndiye fundi wa kupiga pasi, akiwa na wastani wa pasi 70 hadi 80 kwa mechi.

Nortey alitikisa vyombo vya habari vya Ghana baada ya kuweka rekodi ya kupiga pasi 112 kwenye mechi dhidi ya Asante Kotoko mwezi April na kumfanya aingie kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya kiungo bora wa msimu kupitia tuzo za Universal Awards.

 

Meneja na wakala wa mchezaji huyo, Abraham Nui Nortey alionekana akizungumza na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Eng. Hers Said, juzi Uwanja wa Mkapa wakati Yanga wakicheza na Altabara FC kwenye Kombe la Kagame.

 

Baada ya mchezo akaenda vyumbani kuzungumza na viongozi wengine wa Yanga akiwemo Mkurugenzi wa Mashindano, Thabit Kandoro.Championi Ijumaa likamdaka Abraham ili kujua nini kinaendelea ambapo alisema:

“Kuna kitu ‘Exclusive’ na Yanga, ambacho kwa sasa utaniwia radhi ila kwa kuwa umekuwa wa kwanza kuniuliza, utakuwa wa kwanza pia kujua kuna nini.”Championi ilitaka kujua kuhusu wachezaji wake akasema: “Nina wachezaji wengi ambao nawasimamia, na nimekuja Yanga kwa sababu kuna hizi timu ikiwemo Biashara zinahitaji wachezaji wangu.

 

“Kuna kijana wangu anaitwa Rashid Nortey, huyu kwa sasa ndiye ambaye nataka kufanya naye jambo kubwa. Fundi wa kupiga pasi akiwa na rekodi ya kupiga pasi 112 kwenye mechi moja.

 

Ndiye kiungo bora kwa sasa kupitia tuzo za Universal Awards, sifa yake kubwa ni utulivu na jicho la pasi sahihi, hana papara akiwa na mpira.

 

Kama unaona nakudanganya nenda google andika Rashid ‘Nortey record breaks’ utaona.” Championi halikulaza damu likamtafuta Kandoro ambaye alisema: “Kwa sasa naomba Wanayanga wawe watulivu, kila kitu kuhusu usajili na mambo mengine, uongozi utatoa taarifa rasmi.”

Stori: ISSA LIPONDA, Dar es Salaam

 

Leave A Reply