The House of Favourite Newspapers

Yanga yavunja mkataba na Niyonzima

0
NIYONZIMANEW4Haruna Niyonzima.
Klaubu ya Yanga imetangaza kuvunja mkataba na kiungo wake wa kimataifa kutoka nchini Rwanda Haruna Niyonzima kutokana na utovu wa nidhamu ikiwemo kuchelewa kuripoti kambini na kutoipa kipaumbele klabu yake.
Nahodha huyo wa Rwanda alichelewa kurejea kwenye klabu yake mara baada ya kumalizika kwa fainali za michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CEFAFA Challenge Cup) iliyofanyika nchini Ethiopia.
Afisa Habari wa Yanga, Jerry Muro amewaambia Waandishi wa Habari katika Mkutano uliofanyika makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam kwamba Haruna pia anatakiwa kuilipa klabu.
Jerry Muro amesema uamuzi huo umefikiwa na kikao cha Kamati ya Nidhamu ya klabu, baada ya kulichunguza kwa umakini suala la mchezaji huyo na historia yake ya nidhamu pia ndani ya klabu tangu asajiliwe miaka minne iliyopita.
Sakata la sasa la Niyonzima linaanzia mwezi uliopita baada ya mchezaji huyo kuruhusiwa kwenda kuichezea Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki, CECAFA Challenge nchini Ethiopia na akachelewa kurejea baada ya mashindano.
Kufuatia hali hiyo, klabu ilimsimamisha kwa muda usiojulikana Niyonzima kabla ya suala lake kupelekwa Kamati ya Nidhamu, ambayo hatimaye imekuja na maamuzi magumu.
Pamoja na Niyonzima kuwasilisha vielelezo vyote vya kumsafisha, lakini uchunguzi wa Kamati ya Nidhamu ulijiaminisha kiungo huyo amedanganya ili kukwepa hatua za kinidhamu.
Ulibaini plasta gumu (PoP) alilofunga baada ya kurejea akiwa amechelewa ilikuwa ni ‘geresha’ na vielelezo vingine alivyowasilisha vilikuwa ‘feki’ pia.
Na ikamnasa kwenye picha za video siku za karibuni ‘akijirusha’ sehemu mbalimbali za starehe ikiwemo kwenye onyesho la mwanamuziki Ali Kiba.
Niyonzima ambaye alikuwa akikitumikia kikosi cha timu yake ya taifa aliwasili Dar es Salaam December 16 mwaka huu wakati michuano ya Challenge Cup ilimalizika December 6.
Baada ya kuwasili Niyonzima alitoa utetezi wake kwamba alikuwa akisumbuliwa na majeraha aliyoyapata kwenye michuano ya Challenge kwani alikuwa amefungwa bandage ngumu mguuni. Lakini Yanga ilihitaji uthibitisho wa ripoti ya daktari wake wa timu ya taifa.
December 17, Yanga ilitoa adhabu ya kumsimamisha mchezaji huyo kwa muda usiojulikana huku akiendelea kupokea nusu mshahara kwa muda wote huo aliosimamishwa kwa kipindi kisichojulikana.
Adhabu hiyo ilitangazwa na Katibu Mkuu wa Yanga Dkt. Jonas Tiboroha baada ya kamati ya mashindano kuazimia adhabu hiyo iwe ni ya awali wakati ikiendelea kujadili ni adhabu gani stahiki itolewe kwa Niyonzima ambaye amejijengea umaarufu mkubwa kwenye soka la Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
 Leo Jerry Muro ametangaza uamuzi uliofikiwa na klabu ya Yanga wa kuvunja mkataba na Niyonzima huku ikimtaka Niyonzima ailipe klabu hiyo zaidi ya dola za kimarekani 71,175 kama fidia inayotokana na mkataba mpya unaomalizika mwaka 2017.
Haruna aliyezaliwa Februari 5, mwaka 1990 Gisenyi nchini Rwanda, alijiunga na Yanga SC mwaka 2011 akitokea APR ya kwao, ambako aliwasili mwaka 2007 akitokea Rayon aliyoichezea kwa misimu miwili baada ya kujiunga nayo akitokea Etincelles iliyomuibua mwaka 2005.
PICHA NA MAKTABA
haruna 1 haruna 2
Leave A Reply