The House of Favourite Newspapers

Yondani: Naachana na Yanga SC

0

BEKI mkongwe wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani, amesema kuwa hana muda mrefu katika soka, hivyo wakati wowote atatangaza kuachana na mpira wa miguu huku akipanga kujikita kwenye biashara zake binafsi.

 

Yondani ni kati ya wachezaji waliocheza kwa mafanikio makubwa tangu ajiunge na Yanga msimu wa 2011/2012 akitokea Simba. Tangu amejiunga na timu hiyo, amefanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu na Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) mara moja.

 

Mkongwe huyo anayeichezea timu ya taifa, Taifa Stars, hivi sasa hapati nafasi kubwa katika kikosi cha kwanza tangu kocha Mbelgiji Luc Eymael atue kukinoa kikosi hicho.

 

Kisa cha kupigwa benchi, inaelezwa ni kutoweka klabuni hapo bila idhini ya kocha, hivyo Eymael akaamua kumshikisha adabu kwa kumpiga benchi huku akimshinikiza kuendelea kufanya mazoezi.

 

Inaelezwa kuwa Yondani baada ya kuondoka, alizima simu zake zote hukuakiwa hapatikani hewani lakini baadaye alirejea wakati wakijiandaa na mchezo dhidi ya Singida United.

 

Aliporejea ndipo alipokutana na rungu la kocha huyo ambaye aliamua kuanza kumpiga benchi, akisisitiza suala la nidhamu kupewa kipaumbele.

 

Kabla ya mchezo wa jana, Yondani alikuwa amezikosa mechi dhidi ya Azam, Singida United na Prisons ambazo Yanga ilishinda mbili kati ya hizo.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Yondani alisema kuwa anataka astaafu kucheza soka kwa heshima kubwa aliyoijenga akiwa amezichezea klabu kubwa za Simba na Yanga kwa mafanikio.

 

Yondani alisema hivi sasa anajipanga kwa ajili ya kuandaa mazingira mazuri ya maisha ya baadaye akiamini muda wake unakaribia kufikia mwisho kucheza soka la ushindani ili kuepukana na maneno mabaya kutoka kwa mashabiki.

 

Aliongeza kuwa hakuna mtu asiyefahamu uwezo wake wa kucheza soka, lakini anavyoona ni muda muafaka wa kuwaachia wachezaji wengine wanaochipukia ili na wao wapate nafasi ya kucheza.

 

“Sina muda mrefu wa kucheza soka na kikubwa nilichokipanga ni kustaafu kwa heshima ambacho ndiyo muhimu kwangu, nafahamu maamuzi haya yatawashtua wengi lakini ndiyo nilivyopanga.

 

“Nimepanga kustaafu nikiwa ninaichezea Yanga ambayo ilitengeneza sehemu kubwa ya maisha yangu, kwa maana ya maendeleo, hicho ndiyo kitu ninachopanga kukifanya.

 

“Muda muafaka wa vijana kuwaacha na wao waonekane baada ya sisi wakongwe tuliowatangulia, ninaamini wameiga na kujifunza mengi kupitia kwangu,” alisema Yondani.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply