The House of Favourite Newspapers

ZARI ATUMIKA UTAPELI MAMILIONI DAR!

DAR ES SALAAM: Bongo Dar es Salaam, huo ni wimbo wa mwanamuziki wa Bongo Fleva na Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ uliokuwa na ujumbe wa vijana wa mjini kucheza dili hata za hatari ilimradi mkono uende kinywani, ndivyo alivyoibuka mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja ambaye ametumia jina la mrembo Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kutapeli watu mamilioni ya fedha.

 

Mtu huyo ambaye anafanya utapeli huo kupitia njia ya mtandao wa kijamii wa Facebook, anadaiwa kuwaliza wengi kutokana na watu kuamini kwamba wanawasiliana moja kwa moja na mwanamama Zari ambaye alikuwa mpenzi wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

Kikizungumza na Risasi Jumamosi, chanzo ambacho jirani zake wawili, wakazi wa Boko jijini Dar ambao wametapeliwa, kilisema kuwa, mtu huyo amekuwa akifanya utapeli huo kwa muda mrefu na wanaotapeliwa wamekuwa wakifanya siri kwa kuogopa aibu.

 

“Huyu mtu ni mjanja sana, alichokifanya ni kwamba amefungua akaunti inayosoma jina la Zarinnah Hassan ambapo anajifanya ni taasisi ya mikopo. “Ukiingia kwenye hiyo akaunti yake, utaona watu mbalimbali wamechangia na kutoa ushuhuda wa kunufaika na mikopo wanayoitoa pamoja na wengine wakionekana kuuliza utaratibu wa namna ya kupata mkopo,” kilisema chanzo hicho.

Risasi Jumamosi liliutembelea ukurasa huo wa Facebook na kujionea namna ambavyo mhusika wa ukurasa huo alivyoweka namba zake za simu, kuelekeza namna ya kupata mikopo na kiasi unachotakiwa kutuma kama kianzio ili uweze kupatiwa mkopo. “Chukua Mkopo sasaivi Bila RIBA YOYOTE. Kwa 0653 – 78593…Mkopo unapata Sasaivi Muda huo huo.

TUMA AKIBA #ELFU 49, UNAPATA MKOPO LAKI 5.

TUMA AKIBA #LAKI_MBILI, UNAPATA MKOPO MILIONI 1.

TUMA AKIBA #LAKI 650, UNAPATA MKOPO MILIONI 10.

#Tuma_Majina yako KAMILI, #Namba yako ya Simu na hiyo #Akiba

#PIGA_SIMU 0653 – 78593… KUCHUKUA MKOPO SASAIVI.”

Kwenye akaunti hiyo, mbali na jina la Zari, mtu huyo aliyeifungua amewaweka pia viongozi wakubwa wa Serikali ili kuwaaminisha watu kwamba akaunti hiyo ni ya mtu makini na asiye na mzaha.

 

WANAVYOPIGWA

Wakizungumza kwa nyakati tofauti huku wakiomba hifadhi ya majina, wakazi hao wa Boko walisema, waliiamini akaunti hiyo ni ya Zari kutokana na kuona maoni mbalimbali ya watu hususan maarufu hivyo wakatuma kianzio.

“Kwa kweli tuliamini kabisa kwamba si longolongo, tukatuma hicho kianzio, lakini kila tulipoanza kuulizia lini tunapata mkopo, namba hiyo inakuwa haipokelewi wakati awali walikuwa wanapokea na kutoa maelekezo,” alisema mmoja wa waathirika wa ishu hiyo huku akiungwa mkono na mwenzake.

 

Mbali na wakazi hao wa Boko, Risasi Jumamosi lilifanya uchunguzi na kubaini wapo watu wengi ambao wametapeliwa kupitia akaunti hiyo kutokana na shuhuda mbalimbali zilizotolewa katika maoni yaliyopo kwenye ukurasa huo. Pamoja na shuhuda na tahadhari nyingi kutolewa, bado watu mbalimbali wameonekana kulalamika kuibiwa na wengine wakiendelea kuibiwa.

Risasi Jumamosi lilizungumza na mkazi mwingine wa Bunju aliyejitambulisha kwa jina la Zuhura ambaye alikiri kuibiwa shilingi elfu 49, akasema analifikisha suala hilo Polisi ili wahusika wachukuliwe hatua.

 

JESHI LA POLISI LINASEMAJE?

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Murilo Jumanne Muliro alipotafutwa na kuulizwa kuhusu malalamiko ya watu hao kama yamemfikia, alisema yanamfikia na wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kwa wahusika.

 

Alisema wapo watuhumiwa mbalimbali ambao tayari wameshawafikisha mahakamani kwa tuhuma za utapeli wa aina mbalimbali. “Tunawashughulikia, ninachoweza kusema tu, watu wakikutana na utapeli huo, watoe taarifa na wawe na vielelezo ili sisi tuweze kuwachukulia hatua wahusika,” alisema Muliro.

 

Kamanda Muliro aliongeza kuwa, watu wengi wamekuwa wakitapeliwa na kutotoa taarifa au wengine kukimbilia katika vyombo vya habari jambo ambalo kimsingi haliwezi kusaidia kutatua tatizo hivyo kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa Polisi haraka pindi wanapokutana na matapeli kama hao.

STORI: Mwandishi Wetu Risasi Jumamosi

Comments are closed.