The House of Favourite Newspapers

JPM: Hakuna Askari Atakayekatwa Pesa ya Nyumba – Video

RAIS  John Magufuli amesema katika nyumba zaidi ya 6,600 zilizojengwa nchi nzima ambapo mkataba wake ulisema askari watakaokaa wakatwe, amemhakikishia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini,  Jenerali Venance Mabeyo, kuwa hakuna askari yoyote atakayekatwa pesa hiyo, na kwamba deni litabebwa na serikali.

 

Ameyasema hayo leo Novemba 25, 2019 wakati akihutubia mara baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa makao makuu ya Ulinzi wa Taifa katika eneo la Kikombo jijini Dodoma.

Miongoni mwa masuala makubwa aliyezungumzia ni yafuatayo:

“Huu mkataba wa askari kulipa nyumba ulisainiwa kimakosa, sitakubali haya katika uongozi wangu. Nimeshamwelekeza Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha waanze kulipa deni hilo. Serikali tubebe dhamana kwa niaba ya vijana wetu ambao wanafanya kazi kubwa ya kulilinda taifa letu…

 

“Unapokuwa na makao makuu lazima vitu vyote vinavyotimiza neno makao makuu vifuate.  Moja ya vitu hivyo muhimu ni pamoja na kubadilisha makao makuu ya Jeshi la Wananchi.  Nawapongeza mmetimiza ndoto ya Baba wa Taifa ya kuhamia Dodoma…

 

“Kwa kuwa hapa ndio makao makuu pekee ya Jeshi Tanzania nzima, lazima pawe na sura ya makao makuu. Hatuwezi kuwa tunakuja hapa na barabara ya vumbi.  Kwa kuwa mimi ndiyo amiri jeshi mkuu,  na kama hutoi amri basi hufai kuwa amiri jeshi mkuu.  Naagiza TANROADS hakikisheni kuanzia wiki ijayo mnatangaza tenda, barabara hii ijengwe kiwango cha lami kuja makao makuu kwa kilomita zote 18…

 

“Sheria ya ardhi inasema wazi kuwa unapochukua ardhi ya mtu iwe kwa matumizi yako binafsi au ya serikali ni lazima ulipe fidia. Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma hakikisha hawa wananchi 1,500 ambao tumechukua eneo lao na kujenga makao makuu ya Jeshi ya Ulinzi wa Taifa wanalipwa fidia yao ya Tsh Bil. 3.399 kuanzia Desemba 1…”

 

MSIKIE MAGUFULI

Comments are closed.